1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tuzo ya Amani ya Nobel 2022 yawaendea wanaharakati

Lilian Mtono
7 Oktoba 2022

Mwanaharakati wa nchini Belarus Ales Bialiastski, shirika la haki za binadamu la Memorial la nchini Urusi na Kituo cha Uhuru wa Kiraia cha nchini Ukraine wametangazwa kuwa washindi wa tuzo ya amani ya Nobel 2022.

https://p.dw.com/p/4Htje
Friedensnobelpreis für Ales Bialiatski | Nobelkomitee Oslo
Picha: Heiko Junge/AP Photo/picture alliance

Mkuu wa kamati ya Nobeli Berit Reiss-Andersen amewaambia waandishi wa habari muda mfupi uliopita kwamba washindi hao wamefanya juhudi kubwa za kurekodi visa vya uhalifu wa kivita, ukiukwaji wa haki za binadamu na matumizi mabaya ya madaraka na kuongeza kuwa kwa pamoja wanaonyesha umuhimu wa jumuiya ya kiraia kwa amani na demokrasia.

Amesema tuzo hiyo aidha, haimlengi rais wa Urusi Vladimir Putin, bali inailenga serikali yake inayowakilisha utawala wa kibabe na inyaowakandamiza wanaharakati wa haki za binaadamu.

Bi. Reis-Andersen amewasifu washindi hao akisema wanawakilisha vyema mashirika ya kiraia kwenye mataifa yao na kwa miaka mingi wamepaza sauti zao na kutoa miito ya kuwepo kwa haki ya kukosoa mamlaka na kulinda haki za kimsingi za raia. Hakusita pia kutoa mwito kwa mamlaka nchini Belarus kumwachilia mwanaharakati wa nchini humo Ales Bialiastski, akisema anatumai hilo litafanyika ili aweze kwenda Oslo kupokea tuzo aliyotunukiwa.

''Ales Bialiastsk alikuwa mmoja wa waanzilishi wa vuguvugu la demokrasia lililoibuka nchini Belarus katikati mwa miaka ya 1980. Alitoa maisha yake kukuza demokrasia na maendeleo ya amani katika taifa lake la nyumbani.''

Uamzi wa busara

Ales Bialiatski mwanaharakati wa Belarus
Ales Bialiatski mwanaharakati wa BelarusPicha: Tatyana Zenkovich/EPA/dpa/picture alliance

Mwanasiasa wa upinzani wa nchini Belarus, Pavel Latushko amesema mara baada ya washindi kutangazwa kwamba tuzo hiyo ya Nobeli kwa mwanahakati huyo wa haki za binaadamu wa Belarus haiendi kwake peke yake, bali pia kwa wafungwa wote wa kisiasa wanaoshikiliwa nchini Belarus. Amesema inaongeza motisha kwa watu wote wanaopambania haki za binaadamu kuendeleza juhudi zao na kuongeza kuwa wana hakika wataushinda utawala wa kiimla wa rais Alexander Lukashenko.

Washindi wa mwaka jana wa tuzo hiyo bado wanakabiliwa na mazingira maumu tangu walipotunukiwa tuzo hiyo. Waandishi wa habari Dmitry Muratov wa Urusi na Maria Ressa wa Ufilipino wamekuwa wakipambania mashirika yao ya habari, dhidi ya hatua za serikali za kuyanyamazisha. Walitunukiwa tuzo hiyo mwaka jana kutokana na juhudi zao za kulinda uhuru wa kujieleza, suala ambalo ni muhimu katika utekelezaji wa demokrasia na amani ya kudumu

Kamati ya tuzo za Nobeli ilianza kuwatangaza washindi siku ya Jumatatu, kwa kumtunuku Svante Paab, raia wa Sweden tuzo ya masuala ya dawa, wanasayansi watatu Alain Aspect, John F Clauser na Anton Zeilinger waliotunukiwa tuzo ya Fizikia huku tuzo ya Kemia ikienda kwa Carolyn Meldal na Barry Sharpless. Jana Alhamisi, mwanamama raia wa Ufaransa Annie Ernaux alitunukiwa tuzo ya Fasihi.

Tuzo ya Nobeli ya masuala ya uchumi kwa mwaka huu itatangazwa siku ya Jumatatu. Pamoja na tuzo hizi washindi wamezawadiwa vitita vya karibu dola 900,000 na watakabidhiwa fedha hizo Disemba 10. Feddha hizo zinatoka kwenye mfuko ulioachwa na mwanzilishi wa tuzo hizo raia wa Sweden Alfred Nobel mnamo mwaka 1985.