1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tuzo ya fasihi ya Nobel yaenda kwa Doris Lessing

Maja Dreyer11 Oktoba 2007

Tuzo ya fasihi ya Nobel safari hii ametunikiwa mwandishi Doris Lessing wa Uingerenza. Mwenyewe aliwahi kusema: “Mimi sitaipata tuzo hii.” Basi leo atashtuka, kwani huko Stockholm imetangazwa kuwa mwandishi huyu ndiye atazawadia tuzo hiyo muhimu zaidi katika fasihi.

https://p.dw.com/p/C7ru
Doris Lessing
Doris LessingPicha: AP

Saa saba kamili, katibu wa chuo cha Sweden Bw. Horace Engdahl, alitoka ofisi mwake na kuarifu uamuzi juu ya tuzo ya fasihi ya Nobel.

Licha ya kupiga makofu kwa muda mrefu na hivyo kuonyesha kuwa vitabu vya mwandishi Doris Lessing wa Uingereza vinajulikana na kuheshimika, bado uamuzi ulishtusha wengi. Mara nyingi katika miaka 30 iliyopita, Bi Lessing ambaye leo ana umri wa miaka 87 alisemekana kuwa ataipata tuzo hii lakini muda huu wote wengine walimshinda. Hata yeye mwenyewe hakuamini kwamba mwaka huu mshindi ndiyo yeye, kwani wakati katibu Horace Engdahl alipotaka kumpigia simu dakika 15 kabla ya kutangaza uamuzi rasmi, Bi Lessing hakupokea simu, alisema Bw. Engdahl: “Sijazungumza naye, hakuwepo, huenda alikuwa akitembea nje.”

Kweli, Bi Lessing alikuwa madukani wakati habari zilipotolewa. Baadaye alikutana na waandishi wa habari nje ya nyumba yake na alisema tuzo hii ni kama kuwa na karata ya turufu mikononi katika mchezo wa karata.

Doris Lessing alizaliwa mwaka 1919 akiwa mtoto wa afisa wa jeshi la Uingereza nchini Iran. Baada ya hapo alihamia pamoja na familia yake katika koloni la Uingerenza la Rhodesia ya Kusini ambayo leo ni Zimbabwe. Maisha yake barani Afrika yalikuwa na umuhimu mkubwa kwake na kwa uandishi wake. Kutokana na kukosoa vikali sera za ubaguzi wa rangi alipigwa marufuku kutembelea Rhodesia na Afrika Kusini kwa muda mrefu.

Aliporudi Uingereza mnamo mwaka 1949 alichapisha kitabu chake cha kwanza juu ya upenzi kati ya Mwafrika na Mzungu ambao haukuruhusiwa. Baadaye aliolewa na Mjerumani Mkomunisti Gottfried Lessing na mwenyewe alikuwa Mkomunisti. Leo lakini hajali tena vyama vya kisiasa.

Kinyume na nia yake alikuwa mfano halisi kwa tapo la kupigania haki na usawa wa wanawake pale alipochapisha kitabu chake “The Golden Notebook” ama “Daftari ya dhahabu” ambacho pia kinaaminika kumpatia umaarufu. Katika kutoa sababu kwa tuzo hii, chuo cha Sweden kilisema, kitabu hiki kinaangaliwa kuwa cha umuhimu kwa haki za wanawake na ni kimoja kati ya vitabu vichache vinavyotoa picha halisi ya mahusiano kati ya wanawake na wanaume katika karne ya ishirini.

Bi Lessing mwenyewe alikuwa na mashaka juu ya wanaharakati wa haki za wanawake. Miaka michache iliyopita alisema katika mahojiano: “Ikiwa maisha ya wanawake yalibadilika ni kutokana na sayansi na teknolojia na siyo kwa sababu ya wanaharakati wanawake. Ni mashine na dawa zilizobadilisha maisha ya wanawake na si wito. Hutafika popote kwa kuenda barabarani na kuimba wimbo. Inabidi ujenge kamati, uandikie magazetini, uwapigie kura wawakilishi wako waende bungeni – ni vigumu na njia ni ndefu, lakini inakufikisha kwenye lengo lako.”