1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tymoshenko aachiliwa huru

23 Februari 2014

Waziri Mkuu wa zamani wa Ukraine Yulia Tymoshenko ameachiliwa huru kutoka hospitali ya gereza mjini Kharkiv Jumamosi(22.02.2014) wakati bunge likipiga kura ya kumuondowa madarakani Rais Victor Yanukovich.

https://p.dw.com/p/1BDuH
Waziri Mkuu wa zamani wa Ukraine Julia Timoschenko akiwapungia wafuasi wake baada ya kuachiliwa huru Kharkiv.(22.02.2014).
Waziri Mkuu wa zamani wa Ukraine Julia Timoschenko akiwapungia wafuasi wake baada ya kuachiliwa huru Kharkiv.(22.02.2014).Picha: picture-alliance/dpa

Rais Victor Yanukovich wa Ukraine amelaani kile alichokileezea kuwa mapinduzi yanayofanywa na wahuni ambao wamekuwa wakiitishia Ukraine na kusema kwamba hatoikimbia nchi hiyo au kuiacha igawike.

Katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Ukraine UBR rais huyo alionekana mchovu lakini hakuonyesha dalili za kujeruhiwa baada ya kisa ambacho amesema gari lake limeshambuliwa na risasi. Yanukovich amekaririwa akisema "Matukio yanayoshuhudiwa na nchi yetu leo hii na dunia nzima ni mfano wa mapinduzi."

Amesema wanashuhudia kurudi kwa Wanazi,wakati walipoingia madarakani katika miaka ya 1930 nchini Ujerumani na Austria ambapo ni sawa sawa na yale yanayotokea hivi sasa. Ameongeza kusema atafanya kila awezalo kuilinda nchi hiyo isigawike na kuzuwiya umwagaji damu.

Kituo hicho cha televisheni cha UBR hakikusema mahojiano hayo yamefanyika wapi juu ya kwamba inaaminika Yanukovich yuko katika mji wa kaskazini mashariki wa Kharkiv.

Rais Viktor Yanukovich wa Ukraine.
Rais Viktor Yanukovich wa Ukraine.Picha: picture-alliance/dpa

Siku moja baada ya kusaini makubaliano na upnizani kuutatua mzozo huo uliodumu kwa wiki kadhaa Yanukovich amepoteza makao makuu yake ya rais na wizara ya mambo ya ndani ambayo ndio yenye kudhibiti polisi imemgeukia.

Hatambui maamuzi ya bunge

Rais huyo ameongeza kusema kwamba hivi sasa atasafiri kuelekea kusini mashariki mwa nchi hiyo na kuendelea kukutana na wananchi na kwamba atabakia katika ardhi ya Ukraine na kutowa wito kwa waangalizi wa kimataifa na wapatanishi kuwazuwiya wahuni hao.

Bunge likipiga kura kumuondowa Rais Yanukovich mjini Kiev. (22.02.2014)
Bunge likipiga kura kumuondowa Rais Yanukovich mjini Kiev. (22.02.2014)Picha: Reuters

Akigoma kutambuwa uhalali wa sheria na maazimio yaliyopitishwa na bunge leo Jumamosi baada ya spika ambaye ni mtiifu kwake kujiuzulu kwa kutaja sababu za kiafaya,Yanukovich amesema hatosaini hatua zozote zilizopitishwa na bunge ikiwa ni pamoja na kumuachilia hasimu wake mkuu aliyoko gerezani Waziri Mkuu wa zamani Yulia Tymoshenko ambaye tayari ameachiliwa huru leo hii.

Amekiambia kituo cha televisheni cha UBR kwamba haogopi na anaisikitikia nchi yake.

Waandamanaji wadhibiti Kiev

Waandamanaji wanaopinga serikali wanaudhibiti kikamilifu mji mkuu wa Kiev na wamepiga kambi kwenye ofisi ya rais na kwenye eneo la jengo la kifahari linaloaminika linamilikiwa na rais licha ya kutokiri kwake.Upinzani ulilitaka bunge kumshinikiza Yanukovich ajiuzulu.

Waandamanaji wakisheherekea mjini Kiev wakati utawala wa Yanukoch ukikaribia kusambaratika. (22.02.2014).
Waandamanaji wakisheherekea mjini Kiev wakati utawala wa Yanukoch ukikaribia kusambaratika. (22.02.2014).Picha: LOUISA GOULIAMAKI/AFP/Getty Images

Maafisa wa ulinzi na jeshi wametowa wito wa kuwepo kwa utulivu nchini humo.Katika taarifa walizotowa Jumamosi Wizara ya Ulinzi na mkuu wa majeshi ya ulinzi wamesema hawatotumbukizwa katika mzozo wowote ule na kwamba watakuwa upande wa wananchi. Lakini hawakuainisha iwapo watamuunga mkono rais au upinzani.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier ameitaka serikali ya Ukraine na upinzani kuheshimu makubaliano ya amani waliyofikia Ijumaa kukomesha mzozo mbaya kabisa kuwahi kulikumba jimbo hilo la zamani la Muungano wa Kisovieti tokea lijipatie uhuru wake.

Fursa ya mwisho

Steinmeier amesema katika taarifa pande hizo mbili zinawajibika kutii kile walichokubaliana na kuanza kujenga uhusiano wa kuaminiana.Amesema hali inabakia kuwa tete sana na kwamba kipau mbele sasa ni kwa wahusika wote kuwa na mazungumzo ya kuunda serikali imara itakayokubalika na pande zote.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Stenmeier akiwa Kiev baada ya kusainiwa makubaliano ya amani.(21.02.2014).
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Stenmeier akiwa Kiev baada ya kusainiwa makubaliano ya amani.(21.02.2014).Picha: S.Supinsky/AFP/GettyImages

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani ameonya kwamba pengine hii ni fursa ya mwisho kufikia ufumbuzi wa amani kwa mustakbali wa Ukraine.

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema upinzani umeshindwa kutimiza wajibu wao chini ya makubaliano hayo na wamekuwa wakiwasilisha madai mapya kila mara kutokana na ushawishi wa makundi ya vichwa mchungu yenye silaha ambapo vitendo vyao moja kwa moja vinatowa tishio kwa haki ya kujitawala ya Ukraine na kuheshimiwa kwa katiba yake.

Makubaliano ya amani yaliofikiwa chini ya usimamizi wa mataifa ya magharibi yametaka kuitishwa kwa uchaguzi wa mapema ,kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa na kutowa msamaha kwa waandamanaji wanaopinga serikali waliokamatwa katika siku tatu za ghasia zilizogharimu maisha ya takriban watu 100.

Hofu imekuwa ikizidi kuongezeka kwamba nchi hiyo inaweza kugawika pande mbili ule unaounga mkono Umoja wa Ulaya na ule unaounga mkono Urusi.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AFP /AP

Mhariri : Amina Abubakar