1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tymoshenko kumaliza mgomo wa kula

Andreas Noll9 Mei 2012

Kufuatia shinikizo la kisiasa kutokana na kutendewa vibaya kwa kiongozi wa upinzani aliye gerezani Yulia Timoschenko, sasa Ukraine imeahirisha mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya uliokuwa ufanyike mjini Jalta hapo Ijumaa

https://p.dw.com/p/14s54
Waziri Mkuu wa zamani wa Ukraine, Yulia Timoschenko
Waziri Mkuu wa zamani wa Ukraine, Yulia TimoschenkoPicha: picture-alliance/dpa

Kabla ya hapo viongozi kadhaa wa taifa walisema wataususia mkutano huo wa kilele. Wakati huo huo kiongozi huyo wa upinzani amesema ataacha rasmi mgomo wake wa kula kuanzia leo.

Kwa takribani wiki tatu, waziri mkuu wa zamani wa Ukraine, Yulia Timoschenko, amekuwa katika mgomo wa kula, akilalamikia namna anavyotendewa na maafisa wa magereza. Mgomo huo ulioanza muda mfupi kabla ya kuanza kwa mashindano ya Kombe la Ulaya, ulimuweka Rais Viktor Yanukowic na serikali yake chini ya mbinyo mkali wa kimataifa.

Sasa Ukraine inakabiliwa na vitisho vya kususiwa na mataifa kadhaa. Mkutano wa wakuu wa Umoja wa Ulaya uliokuwa umepangwa ufanyike hapo Ijumaa mjini Jalta, umehamishwa, kwa sababu viongozi wengi wamefuta safari zao huko. Miongoni mwao ni Rais Joachim Gauck wa Ujerumani anayelalamikia namna serikali ya Ukraine inavyomtendea kiongozi wake wa zamani.

Nia ya kumaliza mgomo wa kula

Timoshenko anasema anataka kumaliza mgomo wake wa kula, ambao umekuwa ukihatarisha afya yake, ingawa kwa masharti. Kwa miezi kadhaa sasa, kiongozi huyo aliyegeuka mfungwa, amekuwa akisumbuliwa na mshipa wa tumbo, na mgomo wake wa kula umesababisha apoteze uzito mwilini.

Baada ya kuhamishiwa mara kadhaa katika kliniki za nchini Ukraine, Timoshenko amefanya mazungumzo na mtaalamu wa masuala ya mishipa wa Ujerumani, Dokta Hams, ambaye hivi sasa yuko mjini Charkiv. Binti wa Timoschenko, Eugenia, anatoa muhtasari wa mazungumzo hayo:

"Dokta Harms amemuambia mama yangu kwamba ni muhimu kwa matibabu kuanza ili kuondoa matatizo ya kiafya. Matibabu hayo hayawezi kuendana na mgomo wa chakula. Dokta Harms atamuongoza kidogo kidogo mama yangu kutoka kwenye hali ya njaa aliyonayo sasa. Hilo linaweza kuchukuwa hadi siku kumi."

Hata hivyo, suala la kumuondoa Timoshenko kutoka kliniki ya jela halionekani kuwa rahisi. Daktari wa Kijerumani Harms, anataka Timoshenko apelekwe kwenye kliniki nyengine. Wiki iliyopita madaktari bingwa katika hospitali ya Charite walikubaliana kumuhamishia kiongozi huyo wa upinzani katika hospitali nyengine ndani ya Ukraine. Lakini wakili wa Timoshenko, Sergei Wlassenko, anataja masharti ya mteja wake katika hilo:

Yulia Timoschenko wa Ukraine
Yulia Timoschenko wa UkrainePicha: Reuters

"Daima Yulia Timoschenko amekuwa akisisitiza mambo mawili: Kwanza lazima atibiwe kama wanavyoshauri madaktari wa Kijerumani na pili lazima madaktari hao wawe huru. Daktari wa Kijerumani, Harms, ndiye daktari bora zaidi wa kufanya matibabu haya."

Kwa siku kadhaa, Timoshenko alikuwa akichagizana na serikali ya Ukraine, ambayo hatimaye ilikubali kumtuma daktari huyo wa Kijerumani kama alivyoomba, ingawa naye alikataa kumuona kabla ya kukutana na daktari wake. Binti wa Timoschenko anasema mama yake amepoteza kilo 10 hadi sasa na kwamba joto lake la mwili limeshuka sana, kiasi ya kumfanya apauke.

Serikali ya Ukraine inashutumiwa na mataifa mengine ya Ulaya kwa kumbambikizia kesi Timoschenko, kutokana na maslahi ya kisiasa.

Mwandishi: Stephan Laack/DW Kiev

Tafsiri: Mohammed Khelef

Mhariri: Oummilkheir Hamidou