1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tzipi Livni na Mpango wa amani wa nchi za Kiarabu

10 Mei 2007

Waziri wa mambo ya nje wa Israel Tzipi Livni amekutana leo hii na rais Hosni Mubarak kuzungumzia mpango wa amani wa nchi za kiarabu.

https://p.dw.com/p/CB4B
Waziri wa mambo ya nje wa Israel Tzipi Livni akutana na Hosni Mubarak wa Misri
Waziri wa mambo ya nje wa Israel Tzipi Livni akutana na Hosni Mubarak wa MisriPicha: AP

Huu ni mkutano wa kwanza wa viongozi wa ngazi ya juu kati ya Israel na nchi za kiarabu kuhusu suala hilo la amani.

Nchi za Kiarabu zimezitweka jukumu Misri na Jordan la kuishawishi Israel kukubali mpango wa amani wan chi za kiarabu na mazungumzo ya leo ndio ya kwanza kabisa juu ya suala hilo.

Katika ziara yake hii fupi Livni alikutana na rais Hosni Mubarak katika ikulu ya rais mjini Cairo.

Na baadae atakutana na mawaziri wenzake wa mambo ya nje wa Misri Ahmed Aboul Gheit na Abdul-Illah al Khatib wa Jordan.

Mwezi Marchi umoja wan chi za kiarabu uliufufua mpango wa amani uliofikiwa nchini Saudi Arabia.Mpango huo ulipendekeza mahusiano ya kawaida na Israel kwa sharti kwamba Israel kwa upande wake iondoke kwenye maeneo ya Palestina inayoyakalia tangu mwaka 1967 na paundwe dola la wapalestina pamoja na kuwarudisha wakimbizi wakipalestina.

Israel lakini ilikataa mpango huo mara ya kwanza kabisa ulipozinduliwa mwaka 2002. Hata hivyo katika siku za hivi karibuni taifa hilo la kiyahudi limesema pendekezo hilo linaweza kujadiliwa ikiwa inawezekana kuwepo marekebisho katika suala la wakimbizi wakipalestina.

Marekani pamoja na Israel zimesema mpango huu wa nchi za kiarabu unawezekana kupitia mazungumzo kufufua mpango wa amani kati ya Israel na mataifa ya kiarabu.

Katika mahojiano yaliyochapishwa hii leo kwenye gazeti maarufu la Misri ‘’Al-Ahram’’,mfalme Abdullah wa Jordan ameonya kwamba mpango huu wa amani ukishindwa basi kunaweza kukaibuka vita vipya kwenye eneo hilo.

Jordan na Misri ni mataifa pekee ya kiarabu ambayo yamekuwa na amani na Israel. Wakati huo huo vyombo vya habari vya Israel vimeripoti kwamba Tzipi Livni anapendekeza kufufua mazungumzo ya amani na Syria.

Itakumbukwa kwamba rais Bashar al-Assad wa Syria katika miezi ya hivi karibuni amekuwa akishadidia paweko mazungumzo ya mwanzo ya amani na Israel lakini Israel mpaka sasa imekataa pendekezo hilo ikisema lazima serikali ya mjini Damascus kwanza ikome kuyaunga mkono makundi ya wanamgambo nchini Lebanon na ukanda wa Gaza.

Kwa upande mwingine Marekani ambayo ni mshirika mkubwa wa Israel hivi karibuni ilibadili mwelekeo wa sera zake za kukataa kukutana na serikali ya mjini Damascus,na badala yake waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condolezza Rice alikaa kwa mazungumzo na Walid Muallem waziri wa mambo ya nje wa Syria.

Wakati hayo yakiarifiwa gazeti moja la Israel limechapisha taarifa hii leo inayofichua mipango ya ujenzi wa makaazi wa kiyahudi katika eneo linalozunguka Jerusalem kwenye ardhi ya wapalestina ya ukingo wa magharibi. Zaidi ya nyumba 20,000 zitajengwa.Mpango huo umependekezwa na kamati ya manuspaa na inabidi uidhinishwe na serikali.