1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UAE yashutumiwa kuidukua Qatar

Daniel Gakuba
17 Julai 2017

Mzozo wa Ghuba ya Kiarabu umechukua sura mpya, baada ya ripoti kudai kwamba Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ulidukua tovuti ya Qatar, na kupachika ripoti ambayo ilitumiwa kama kisingizio kuiwekea vikwazo nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/2geP1
Katar - Doha Skyline im Sandsturm
Picha: picture-alliance/Photoshot/Nikku

Ripoti ya udukuzi huo unaodaiwa kufanywa na Umoja wa Falme za Kiarabu imechapishwa na gazeti la Washington Post la nchini Marekani, ikimnukuu afisa wa upelelezi wa Marekani ambaye jina lake halikutajwa, aliyesema kuwa maafisa wakuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu walikutana tarehe 23 Mei kupanga njama dhidi ya Qatar.

Siku iliyofuata, hii ikiwa ni kwa mujibu wa afisa huyo aliyenukuliwa na Washington Post, ripoti ilionekana kwenye tovuti ya serikali ya Qatar, ikiwa na maneno yaliyodaiwa kutamkwa na Emir wa nchi hiyo Sheikh Tamim Bin Hamad al-Thani katika hotuba yake, akiisifu Iran na kuzungumzia mahusiano mema kati ya Qatar na Israel.

Ripoti hiyo ilidai Sheikh al-Thani alisema Iran ni nchi muhimu ya Kiislamu na yenye nguvu katika kanda, ambayo haiwezi kupuuzwa, na isingekuwa jambo la busara kuifanyia ugomvi. Maneno kama hayo vile vile yalitolewa katika ukurasa wa twittter wa tovuti hiyo ya Qatar.

Kujikosha kwa Qatar kwaambulia patupu

Katar US-Truppen und katarischen Truppen bei gemeinsamen militärischen Übungen
Jeshi la Marekani linayo kambi kambi kubwa nchini QatarPicha: Reuters/N. Zeitoon

Qatar ilikanusha haraka ripoti hiyo ikisema tovuti yake imedukuliwa, na kuiondoa ripoti hiyo iliyosababisha mvutano. Hata hivyo hatua hiyo haikutosha, kwani Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain na Misri zilivifungia matangazo vyombo vya habari vya Qatar, na baadaye kukatisha uhusiano wa kidiplomasia na nchi hiyo.

Umoja wa Falme za Kiarabu umekanusha ripoti hiyo iliyochapishwa na Washington Post, ikisema ni uongo mtupu. Ubalozi wa nchi hiyo mjini Washington umetoa tangazo ukisema nchi hiyo haikuhusika kwa vyovyote vile na ripoti ambayo gazeti hilo limedai iliipachika katika tovuti ya Qatar.

Siasa za Marekani kuhusu Ghuba zajikuta njia-panda

Mzozo unaoendelea baina ya nchi hizo tajiri za Ghuba ya Kiarabu ambazo siku za nyuma zilikuwa washirika, umeziweka katika hali tete harakati zinazoongozwa na Marekani kupambana na kundi linalojiita Dola la Kiislamu, kwa sababu wanaohusika katika mzozo huo wote ni washirika wa Marekani.

Karte Countries that severed ties with Qatar ENG
Qatar, nchi ndogo lakini tajiri imejikuta katika mbinyo, baada ya kutengwa na majirani zake

Nchini Qatar ipo kambi ya kijeshi ya Marekani yenye wanajeshi zaidi ya 10,000, ambayo ni makao makuu makuu ya jeshi la Marekani, na nchini Bahrain ipo kambi ya wanamaji ya Marekani.

Rais wa Marekani Donald Trump ameegemea wazi wazi upande wa Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu katika mzozo huo, na ameunga mkono madai yao kwamba Qatar inayafadhili makundi yenye itikadi kali za kiislamu na kutishia utengamano wa Kanda ya Mashariki ya Kati.

Wiki iliyopita waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson alifanya ziara katika Ghuba ya Kiarabu na kubaki huko kwa siku nne akifanya juhudi za usuluhishi, lakini aliondoka kurejea mjini Washington bila dalili za kupiga hatua yoyote ya maana.

Mwandishi: Daniel Gakuba/ape, dpae

Mhariri:Yusuf Saumu