1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baba amnajisi bintiye na kumzalisha watoto saba

Mwadzaya, Thelma28 Aprili 2008

Mtuhumiwa wa unajisi na ubakaji nchini Austria amekiri kuwa alimzalisha binti yake watoto saba.Polisi wanaendelea na uchunguzi wa kisa hicho .

https://p.dw.com/p/Dq1q
Nyumba ya mtuhumiwa wa unajisi na ubakajiPicha: AP

Mwanamume huyo aliye na umri wa miaka 73 alimfungia binti yake kwenye chumba cha chini kwa muda wa miaka 24 katika eneo la Amstetten walikoishi.Kisa hicho kiligunduliwa pale mtoto mkubwa wa uhusiano huo usiokuwa halali alipougua na kulazimika kupelekwa hospitali.

Mwanamume huyo Josef Fritzl alikamatwa hapo jana na polisi nao uchunguzi wa nyumba yake unaendelea.Polisi wanachunguza jengo alikomficha binti yake na kumtesa kwa muda wote huo.Josef Fritzl aliyekuwa mhandisi anatuhumiwa kwa kumzuia bila hiari binti yake Elisabeth aliye na umri wa miaka 42 na kumzalisha watoto 7.


Kwa mujibu wa ripoti za mwanzo vyumba hivyo vilivyokuwa chini ya nyumba yao vilikuwa vidogo ila vilikuwa na sehemu ya kupikia na kufua nguo. Eneo hilo aidha lilikuwa na jela ndogo inayozuia kelele na sauti kusikika.Mtuhumiwa huyo Josef Fritzl aliwataarifu polisi kuhusu namna ya kufungua milango ya nyumba hivyo.Kesi hiyo ilibainika pale msichana aliye na umri wa miaka 19 alipoumwa na kulazimika kupelekwa hospitali.Madktari walitoa wito kwa mamake msichana huyo kujitokeza ili kutoa maelezo zaidi kuhusu ugonjwa wa bintiyake.Mama huyo anaaminika kuwa alikuwa hajulikani aliko.


Elisabeth alinajisiwa na babake hata kabla ya kizuizi chake kuanza mwaka 84 na kujifungua watoto saba.Mtoto mmoja anaripotiwa kufariki muda mfupi baada ya kuzaliwa.Watoto watatu kati ya wote saba walio na umri wa kati ya miaka mitano na tisa waliishi naye kama wafungwa muda wote huo. Wengine watatu waliosalia waliishi na bibi na babu yao aliye pia baba yao na kuhudhuria shule za mtaa huo.

Josef aliwaeleza polisi kuwa binti yake aliyetoweka muda mrefu aliwaachia watoto mlangoni mwake miak mingi iliyopita.


Uongozi unaendelea na uchunguzi wa shanga za urathi za DNA unaolenga kubaini mbivu na mbichi hii leo.Kwa sasa Elisabeth na wanawe wake watano wanapewa huduma za usaidizi na madaktari vilevile wahudumu wa afya.Binti yake mkubwa kwa jina Kerstin aliye na umri wa miaka 19 anaaminika kuugua ugonjwa nadra sana na anahudumiwa katika kitengo cha wagonjwa mahututi.

Elisabeth alipelekwa hospitali na babake pamoja na wanawe wawili.Wakati huo ndipo babake alimueleza mamake kuwa binti yao aliyepotea karudi.Elisabetha aliandika taarifa alipofika polisi kuelezea yaliyomsibu baada ya kuhakikishiwa kuwa hatukuwa karibu na babake tena maishani mwake.Kwa mujibu wake babake alimnajisi tangu alipokuwa na umri wa miaka 11.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha uchunguzi katika Mkoa wa Lower Austria Franz Polzer mwanamke huyo hakumkimbia mwanawe aliyepelekwa hospitali ila alizuiliwa bila hiari kwa kipindi cha miaka 24.

''Huyu si mwanamke aliyemkimbia mwanawe aliyelazimika kufikishwa hospitali kwani anaugua.Tunajua kuwa amezuiliwa bila hiari na babake mzazi kwa miaka 24 vilevile bila shaka alinyanyaswa kijinsia na kubakwa.''


Taarifa zinaeleza kuwa mke wake mtuhumiwa Bi Rosemarie hakujua kilichomsibu bintiyake baada ya kutoweka mwaka 84.Mama huyo aliamini kuwa Elisabeth aliondoka kwa hiari yake pale walipopokea barua iliyoeleza kuwa wasmitafute.


Magazeti nchini humo yanaelezea kisa hicho kuwa uhalifu uliotendwa na mtu katili vilevile kuhoji jukumu la uongozi na wakazi wa eneo la Amstetten.Wakazi hao wanaaminika kuwa hawakujua kilichokuwa kikitendeka katika mtaa wao ulio umbali wa maili 80 kutoka mji mkuu wa Vienna.

Kisa hicho kilishangaza kwavile kilifanana na chengine cha awali ambapo Natasha Kampusch msichana mmoja raia wa Austria alizuiliwa bila hiari yake katika chumba kisichokuwa na madirisha kwa muda wa miaka minane kwenye eneo la Strasshofen.Natasha alifanikiwa kutoroka mwezi Agosti mwaka 2006.