1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ubelgiji kugawika ?

16 Julai 2008

Uhariri wa magazeti ya leo ya Ujerumani ulichambua hatari ya kugawika Ubelgiji.

https://p.dw.com/p/EdZi

Uchambuzi wa wahariri wa magazeti ya leo ya Ujerumani umetuwama zaidi juu ya kuporomoka kwa serikali ya Ubelgiji kutokana na mvutano kati ya wavaloni wanazungumza kifaransa na waflamish wanaozungumza kidachi.Pia hukumu ya magaidi waliotaka kumuua waziri mkuu wa zamani wa Irak ,Allawi, mjini Berlin imechambuliwa sawa na msukosuko wa fedha nchini Marekani .

Gazeti la THÜRINGER ALLGEMEINE kuhusu msukosuko wa hatari ya kugawika Ubelgiji kufuatia kujiuzulu kwa waziri mkuu aliechanganya damu zote mbili laandika:

"Akiwa mama yake ni mflamish na baba mvaloni,Yves Leterme,alionekana mwaka mmoja uliopita, ni waziri mkuu aliefaa sana kuponesha donda la makabila hayo 2 ya Ubelgiji.

Eneo la Flandern la wabelgiji wa asili ya kidachi linataka kujitenga na wavaloni wanaozungumza kifaransa ambao wanaonekana ni masikini na walio nyuma nchini Ubelgiji.

Waziri mkuu Leterme alipanga mageuzi katika dola hili ili kurejesha amani na utulivu nchini Ubelgiji.Lakini wapi,kwani, pande hizo mbili zinazobishana zamani ziliunda serikali zao wenyewe,mabunge yao,hazina na idara zao za elimu.

Sasa -laandika gazeti-ishara zote zaelekeza kufanyika uchaguzi mpya nchini Ubelgiji,lakini lauliza gazeti-uchaguzi huo utabadili kitu gani ?

Gazeti la NÜREMBERGER ZEITUNG likiendeleza mada hii,laandika:

" Waziri mkuu ni wa kabila la waflame,jina lake lakini la kivaloni na akijitahidi kutunga mfumo mpya wa dola ambalo kwa kweli halipo kabisa.Yote hayo yadhihirika yamemchanganya Yves Leterme na badala ya kuitikia wimbo wa taifa wa Ubelgiji amewahi kusikiliza wimbo wa taifa wa Ufaransa .Kwa namna mbali mbali mchristian democrat huyu aliefadhahika anatoa sura halisi ya nchi yake ilivyo.

Wale walioweka matumaini kuwa mizizi yake katika makabila hayo 2 ya Ubelgiji ingeweza kuponesha donda,wamegundua walikosea."

Ile njama ya 2004 kumuua waziri mkuu wa zamani wa Irak,Allawi mjini Berlin,inaonekana kama zilikua ni kelele za bure tu.Gazeti la Kölner Stadt-Anzeiger laandika:

"Yule ambae jioni ya kuamkia siku ya kufanyika kitendo hicho,anakagua mahala palipokuwa pafanyike njama hiyo na hakuti alao silaha au mripuko wowote,huyo hafai kutiwa maanani.Ukweli ni kwamba, polisi hawakuzima njama ya kuua bali imezima jaribio lililokwishashindwa kufanyika.

Adhabu iliotolewa kwa walioandaa njama hiyo ya hadi miaka 10 korokoroni si kubwa hivyo.Kwani wairaki hao 3 waliungamkono vitendo vya kigaidi vya kundi lao la Ansar-al-Islam nchini Irak.Huko watu wanauliwa kweli na kukatwakatwa.Na kwavile katika vitendo vya kigaidi haviwezi kuandaliwa bila ya fedha, fedha kutoka Ujerumani zilichangia mno.

Likitugeuzia mada na kutuchukua katika msukosuko wa fedha nchini Marekani, gazeti la Westfälische Nachrichten kutoka Münster laandika:

"Hali ya mambo inaanza kuwa mbaya: Foleni ndefu mbele ya INDYMAC BANK zinabainisha walioweka akiba zao nchini Marekani wameingiwa na wasi wasi mkubwa kutokana na habari zilizotoka kutoka soko la fedha.Wameingiwa na hofu hizo licha ya kuwa 99% ya fedha zao walizoweka akiba watazipata kwa kufidiwa na mfuko wa raslimali.

Endapo hofu hizi zikizagaa n a kutapakaa hadi nchi nyengine ,mfumo wa fedha duniani utajikuta hatarini.Kuingilia kati kwa serikali ya Marekani kuzitia jeki banki hizo zinazopepesuka, ili kuwa dawa m ujarabu.Dawa hii iendelee kutolewa ili kuponesha maradhi..."