1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ubelgiji yamtimua kocha Marc Wilmots

15 Julai 2016

Ubelgiji imefuta kocha wa timu ya taifa Marc Wilmots baada ya timu yake iliyopigiwa upatu na yenye wachezaji wengi nyota kushindwa kusonga mbele zaidi ya robo fainali katika dimba la ubingwa wa Ulaya – Euro 2016

https://p.dw.com/p/1JPeU
Interaktiver WM-Check 2014 Trainer Belgien Wilmots
Picha: imago/VI Images

Rais wa shirikisho la kandanda la Ufaransa amesema malengo yaliyowekwa kwa michuano ya euro hayakutimizwa, na sasa wanahitaji msukumo mpya. Mchakato umeanza wa kumtafuta kocha mpya mwenye ujuzi wa kimataifa kuchukua usukani kabla ya mchuano wa kirafiki dhidi ya Uhispania Septemba mosi kabla ya kuanza michuano ya kufuzu katika Kombe la Dunia la 2018 nchini Urusi.

Kwingineko, aliyekuwa mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ukraine Andriy Shevchenko ameteuliwa kuwa kocha wa timu ya taifa kuchukua nafasi ya Mykhailo Fomoneko anayeondoka.

Shevchenko mwenye umri wa miaka 39, anayeshikilia rekodi ya ufungaji mabao mengi Ukraine, ambaye pia alivichezea vilabu vya Dynamo Kiev, AC Milan na Chelsea, amezinduliwa rasmi hapo jana katika kikao cha wanahabari.

El Classico kuchezwa Desemba

Michuano ya El Classico ya kandanda la Uhispania baina ya Barcelona na Real Madrid itachezwa Desemba na Aprili. Ni michuano miwili inayosubiriwa kwa hamu kubwa katika msimu wa 2016/17 wa ligi kuu ya Primera Division ambayo ratiba yake ilitolewa jana.

Mabingwa watetezi Barca watawaalika Real Desemba 4 uwanjani Camp Nou. Mchuano wa marudio utachezwa Aprili 23, uwanjani Santiago Bernabeu. Wakati msimu mpya wa La Liga unang'oa nanga, Barca itaanza kutetea taji lake nyumbani kwa Real Betis mnamo Agosti 21.

Kabla ya hapo miamba hao wa Catalan watachuana na Sevilla katika fainali ya mikondo miwili ya Kombe la Uhispania maarufu kama Spanish Super Cup. Kombe hilo ni kati ya mabingwa wa ligi na washindi wa Kombe la Mfalme, au katika hali hii, makamu bingwa kwa sababu Barca walishinda taji hilo pia.

Mkondo wa kwanza utachezwa Agosti 14 nyumbani kwa Sevilla kabla ya marudiano kuchezwa siku tatu baadaye.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri:Iddi Ssessanga