1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi Afghanistan kuendelea hata baada ya kujitoa Abdullah

2 Novemba 2009

Mgombea urais nchini Afghanistan, Abdullah Sbdullah ametangaza kujitoa katika duru ya pili ya uchaguzi utakaofanyika Jumamosi ijayo

https://p.dw.com/p/KKgK
Abdullah AbdullahPicha: AP

  Abdullah alitangaza kujitoa baada ya matakwa yake ya kutaka kubadilishwa kwa mkuu wa tume ya uchaguzi, kukataliwa na Rais Karzai.

Hata hivyo mataifa makubwa ya magharibi yamesema kujitoa kwake huko hakutaathiri harakati za kuisaidia nchi hiyo kurejesha amani.

Hatua hiyo inaonakana kumhakikishia Rais Hamid Karzai ambaye alikosa ushindi wa moja kwa moja katika duru ya kwanza, nafasi ya kuongoza tena kipindi cha cha urais nchini humo.Hata hivyo lakini uamuzi huo pia unatishia udhibiti wa utawala wake.

Tume huru ya uchaguzi ambayo viongozi wake waliteuliwa na Rais Karzai imesema kuwa uchaguzi huo utaendelea kama ulivyopangwa Jumamosi ijayo.

Hata hivyo inaonekana kuna uwezekano suala la uchaguzi huo kufikishwa mahakamani, na msemaji wa umoja wa mataifa mjini Kabul Aleem Siddique amesema kuna ugumu uliyoko mbele katika kufanyika kwa duru hiyo ya pili kwa mgombea mmoja tu kusimama pekee hususani katika kipindi hiki ambacho hali ya usalama nchini humo inazidi kuwa tete.

Lakini mataifa ya magharibi yameelezea kushirikiana na serikali mpya itakayochaguliwa bila kutilia maanani hatua ya kujiondoa kwa bwana Abdullah katika uchaguzi huo.

Guido Westerwelle Symbolbild Koalitionsvertrag
Waziri wa Nje wa Ujerumani Guido WesterwellePicha: AP

Waziri mpya wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle amesema suala muhimu kwa sasa ni duru hiyo ya pili kufuata taratibu na sheria.

´´Kile kilichomuhimu kwa sasa ni kuona shughuli nzima ya uchaguzi huo inafuata sheria na taratibu.Tunatayarisha serikali nchini Afghanistan ambayo ni halali, ya kidemokrasia na yenye kufuata sharia na katiba´´

Kwa upande wake,Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, bibi Hillary Clinton amesema ni jukumu la wananchi wa Afghanistan kuamua njia ya kufuata itakayohakikisha uchaguzi unafanyika kwa misingi ya katiba ya nchi hiyo.

Marekani pia imesema kuwa itashirikiana na Rais Hamid Karzai, pamoja na wasi wasi kwamba rais huyo imani na heshima yake itapungua kutokana na kuwa mgombea pekee katika duru hiyo ya pili.

Naye Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown alimpigia simu Rais Karzai mara baada ya bwana Abdullah kutangaza kujitoa, ambapo alimtaka rais huyo kutojitangaza mshindi na badala yake utaratibu mzima uendelee wa uchaguzi.

Lakini pia Gordon Brown alisema muhimu kwanza ni suala la usalama.

´´Umuhimu wetu wa kwanza ni suala la usalama wa majeshi yetu na tunahitaji pia demokrasia changa ya Afghanistan iimarishwe na kushirikishwa´´

Afghanischer Präsident Hamid Karsai mit UNO-Generalsekretär Ban Ki-moon
Ban Ki-moon akisalimiana na Rais Karzai mjini New York wakati wa mkutano wa Umoja wa MataifaPicha: AP

Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amewasili katika mji mkuu wa Afghanistan Kabul leo hii katika ziara ya kushtukiza, ambapo mchana huu anatarajiwa kuwa na mazungumzo na Rais Karzai, kabla ya kukutana na bwana Abdullah Abdullah.

Ban Kin-moon amewasili nchini Afghanistan ikiwa ni siku sita tu tokea wanamgambo wa Taliban walishambulia makaazi ya wafanyakazi wa umoja huo mji Kabul na kuwaua watano pamoja na raia watatu wa Afghanistan.

Umoja wa Mataifa ndiyo unaosimamia uchaguzi huo nchini Afghanistan, ambapo duru ya kwanza ya uchaguzi huo uliyofanyika tarehe August 20, iligubikwa ni vitendo vya wizi wa kura, hatua ambayo ilizua wito wa kumtaka Rais Karzai amtimue mkuu wa tume ya uchaguzi Azizullah Ludin, pamoja na mawaziri wengine wanne waliyokuwa wakimfanyia kampeni rais huyo.

Rais Karzai alipata asilimia 49.67 ya kura, huku mpinzani wake akipata asilimia 30 na hivyo kulazimika kuingia katika duru ya pili baada kushindwa kufikisha asilimia 50 ya kura.

Mwandishi:Liongo Aboubakary Jumaa AFP/Reuters

Mhariri:Hamidou Oummilkhheir.