1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi Ivory Coast

31 Oktoba 2010

Uchaguzi nchini humo uliahirishwa kwa muda mrefu na unatarajiwa kuunganisha nchi hiyo iliyogawika katika sehemu mbili kutokana na vita na kuifufua nchi iliyokuwa na uchumi bora katika Afrika magharibi.

https://p.dw.com/p/PusL
Rais aliye madarakani Laurent Gbagbo anapigiwa upatu kushinda uchaguzi huo.Picha: AP

Wapiga kura nchini  Ivory Coast wanapiga kura leo, katika uchaguzi wa urais ulioahirishwa  kwa muda mrefu, na ambao ni wa kwanza tokea kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe 2002 katika taifa hilo la Afrika Magharibi.

Kiasi ya watu milioni 5.7 wana haki ya kupiga kura. Rais aliyoko madarakani Laurent Gbagbo ambaye aliingia madarakani mwaka 2000 ni mmoja wa wagombea anayepigiwa upatu kushinda, miongoni mwa  wagombea 13.  Wapinzani wake wakuu ni rais wa zamani Henri Konan Bedie, ambaye alipinduliwa mnamo mwaka wa 1999 na Waziri Mkuu wa zamani  Allasane Outtara. Kupinduliwa kwa Bedie ndiko kulikozusha mapigano na umwagikaji mkubwa wa damu nchini humo na kuligawa taifa hilo pande  mbili, serikali ikiongoza eneo la kusini na eneo la Kaskazini likiwa chini ya uogozi wa waasi huku wanajeshi wa kulinda amani kutoka Ufaransa na Umoja wa Mataifa wakiwa kati kati ya pande hizo mbili. Hata hivyo mkataba wa amani wa 2007 kwa kiasi kikubwa ulifanikiwa kutekelezwa.