1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi katika jimbo la North-Rhine Westphalia, Ujerumani

Kabogo Grace Patricia10 Mei 2010

Chama cha CDU cha Kansela Angela Merkel kimepoteza viti katika uchaguzi huo uliofanyika jana Jumapili.

https://p.dw.com/p/NK3b
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, akipiga kura katika uchaguzi wa jimbo la North Rhine-Westphalia mjini, Bonn, Jumapili ya Mei 9, 2010.Picha: AP

Chama cha Kansela Angela Merkel wa Ujerumani CDU na kile cha FDP vimepoteza wingi mkubwa wa viti katika baraza la wawakilishi, baada ya CDU kupoteza viti vingi katika uchaguzi wa jimbo la North-Rhine Westphalia uliofanyika jana. Matokeo ya awali yanakipa CDU asilimia 34.5 ya kura, ikiwa ni chini ya zaidi ya asilimia 10 ikilinganishwa na uchaguzi wa mwisho miaka mitano iliyopita.

Mbunge wa CDU, Wolfgang Bosbach amesema matokeo hayo ni pigo kwa chama hicho. Chama cha SPD kimepata asilimia 34.6, na kukipa ushindi mdogo sana. Chama cha Kijani kinaonekana kuwa mshindi mkubwa katika uchaguzi huo baada ya kuongeza sehemu yao ya kura mara mbili kwa asilimia 12.1.

FDP kimepata asilimia 6.8. Chama cha mrengo wa Shoto kitawakilishwa katika bunge la majimbo kwa mara ya kwanza baada ya kupatia asilimia 5.6. Matokeo hayo yanaonyesha kuwa chama cha upinzani SPD na kile cha Kijani vinaweza kuunda muungano katika jimbo hilo lenye wakaazi wengi nchini Ujerumani, lakini kikiungwa mkono tu na chama cha mrengo wa Shoto.