1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi mkuu Israel leo

Aboubakary Jumaa Liongo/AFP10 Februari 2009

Wananchi wa Israel leo wana piga kura katika uchaguzi mkuu ambapo ushindani uko kati ya Waziri wa Mambo ya Nje Tzipi Livni na Waziri Mkuu wa zamani Benjamin Netanyau.

https://p.dw.com/p/GqZg
Kiongozi wa Chama cha Likud Benjamin Netanyahu )Picha: AP

Kwa wiki kadhaa kura za maoni zimekuwa zikimpa nafasi Waziri huyo mkuu wa zamani kutoka chama cha Likud cha mrengo wa kulia, ambaye katika kampeni zake amekuwa akijinadi kama mtu mwenye uwezo wa kulinda usalama wa nchi hiyo.


Lakini katika siku za hivi karibuni Bi Livni amekirejeshea heshima chama chake cha Kadima cha mrengo wa kati ambacho bado kinajaribu kujinasua kutoka katika kashfa za rushwa zilizomlazimisha Waziri Mkuu Ehud Olmert ajiuzulu.


Mshangao mkubwa katika kampeni za uchaguzi huo wa leo huko Israel ni kuchomoza kwa nyota ya Avigdor Lieberman muahamiaji kutoka Urusi ambaye amekuwa akijinadi kwa sera za kuwashambulia maadui wa Israel kwa mkono wa chuma.


Lieberman na chama cha Yisrael Beitenu amejivuta hadi na fasi ya tatu na kukipiga kumbo chama cha Labour cha Waziri wa Ulinzi Ehud Barak.


Kura za mwisho za maoni zimekipa nafasi chama cha Likund cha Benjamin Netanyau viti kati ya 25 na 27, huku chama cha Kadima cha Bi Tzipi Livni viti kati ya 23 na 25.