1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi mkuu kuitishwa mapema Ukraine

Elizabeth Shoo25 Februari 2014

Kampeni za uchaguzi mkuu zimeanza nchini Ukraine, wakati ambapo nchi hiyo inatarajiwa kutangaza serikali ya mpito Alhamisi. Wakati huo huo, rais aliyetolewa madarakani Viktor Yanukovych hajulikani alipo.

https://p.dw.com/p/1BEsT
Alexander Turtschinow
Picha: picture-alliance/Itar-Tass/Maxim Nikitin

Tume ya uchaguzi ya Ukraine imetangaza kwamba uchaguzi mkuu wa nchi hiyo utafanyika tarehe 25 Mei mwaka huu. Wagombea wamepewa nafasi hadi Aprili 4 kupiga kampeni. Uchaguzi mkuu unakuja baada ya kipindi kirefu cha maandamano katika mji mkuu wa Ukraine Kiev na kwenye miji mingine ya nchi hiyo. Wapinzani wa rais Viktor Yanukovych walitaka aachie madaraka na kuitisha uchaguzi mkuu wa mapema. Miongoni mwa wanaotarajiwa kugombea nafasi ya urais ni mpinzani mkuu wa Yanukovych, Yulia Tymoshenko, ambaye aliachiwa kutoka jela Jumamosi iliyopita. Wengine ni Arseniy Yatsenyuk aliyekuwa waziri wa mambo ya nje, billionea Petro Poroshenko pamoja na bondia Vitali Klitschko.

Hivi sasa Ukraine inatawaliwa na serikali ya mpito inayoongozwa na spika wa Bunge, Oleksandr Turchinov. Alhamisi waziri mkuu mpya pamoja na baraza la mawaziri litatangazwa. Rais Viktor Yanukovych bado hajulikani alipo. Vikosi vya usalama vinamsaka kwa mashtaka ya kuamuru vifo vya watu 82 katika siku zilizopita, wengi wao wakiwa waandamanaji.

Mvutano kati ya Magharibi na Urusi

Hali bado si shwari Ukraine. Kiongozi wa chama cha Walinda Mazingira katika bunge la Umoja wa Ulaya, Rebecca Hams, alitembelea Ukraine jana na alikuwa na haya ya kusema: "Mgogoro huu bado utawaathiri raia wa Ukraine kwa muda mrefu na kama vyombo vya habari vinavyoripoti, ni kweli kuwa watu hawa wanahitaji muda wa kuwa na majonzi."

Mgogoro wa Ukraine umeendelea kwa wiki kadhaa
Mgogoro wa Ukraine umeendelea kwa wiki kadhaaPicha: picture-alliance/dpa

Mbali na msukosuko wa kisiasa, Ukraine inakumbwa pia na tatizo la kiuchumi. Nchi hiyo imeziomba nchi za Magharibi msaada wa Dollar za Kimarekani billioni 35 zinazohitajika kuizuia Ukraine isifilisike.

Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton jana alikutana na waziri mkuu wa kipindi cha mpito kujadili msaada wa kifedha unaoweza kutolewa. Ukraine imekuwa ikiitegemea Urusi kwa msaada wa fedha, lakini sasa baadhi ya wanasiasa wanataka kujiondoa kuitegemea Urusi na kugeukia Umoja wa Ulaya. Waziri wa mambo ya nje wa Urusi, Sergei Lavrov ameonya kuwa ni hatari kuilazimisha Ukraine kuchagua kati ya Urusi na nchi za Magharibi.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/afp/ap

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman