1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi mkuu

Oumilkher Hamidou28 Septemba 2009

SPD yakaalia viti vya upinzani bungeni

https://p.dw.com/p/Jqdm
Bunge la Shirikisho-Bundestag mjini Berlin

Zilzala ya kisiasa imekipiga chama cha umma cha SPD.Katika uchaguzi mkuu wa jana,chama hicho cha Social Democratic kimepata pigo kubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa tangu vita vikuu vya dunia vilipomalizika. Katika wakati ambapo Wana Social Democratic wanajiandaa kukalia viti vya upinzani bungeni, kansela Angela Merkel, licha ya chama chake kupungukiwa pia na kura, anajiandaa kuunda serikali ya muungano pamoja na chama kidogo cha kiliberali-FDP,kilichoibuka kua mshindi mkubwa wa uchaguzi mkuu wa jana.

Tuanze basi na gazeti la mjini Cologne linaloandika:

Mshindi halisi wa uchaguizi mkuu ni Guido Westerwelle. Hakutetereka na wala hakutishika na dhana za wapinzani wake, amezielekeza karata zake moja kwa moja upande wa Angela Merkel na ameshinda.Yeye ndie wakushukuriwa kwamba muungano wa vyama vikuu hauko tena. Na hali hiyo inamaanisha mwenyekiti wa FDP ataingia katika mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano kifua mbele. Kwa kansela Angela Merkel hali hii mpya itamaanisha kuonyesha zaidi muelekeo kuliko hali namna ilivyokua hadi sasa. Wajerumani wanategemea zaidi kitu kimoja hivi sasa: hali bayana badala ya kubabaisha babaisha.

Gazeti la REUTLINGER GENERAL ANZEIGER linaandika:

Ujerumani imepiga kura kuleta mageuzi ya kisiasa-lakini kansela ndie yule yule. Kusema kweli wapiga kura wameuchagua mfumo badala wa muungano wa vyama vikuu uliokuwepo madarakani. Na kura kwa ajili ya muungano wa nyeusi na manjano ni bayana kabisa. Walioduwaa ni wana SPD- wamefikia kiwango cha chini kabisa katika historia yao. Hayo sio tuu ni machungu, bali pia ni pigo la kihistoria. Sababu ya pigo hilo haitokani hata kidogo na kampeni chapwa ya uchaguzi au uzembe katika shughuli za serikali. Mageuzi yaliyoanzishwa na SPD katika sekta ya jamii na uchumi yameinufaisha Ujerumani, lakini wakati huo huo yamekigawa chama cha SPD.

Gazeti la Abendzeitung la mjini Munich linaandika:

Kuna uchaguzi ambao matokeo yake mtu hushindwa kutambua wapiga kura wanataka nini hasa. Na kuna uchaguzi ambao mtu anatambua hapo hapo kinachotakiwa. Kama ilivyokua katika uchaguzi mkuu wa 2009. Wapiga kura wametamka. Wanasema-kwanza Angela Merkel aendelee kua kansela -pili; muungano wa vyama vikuu ukome.Na hayo ndio matokeo ya kufurahisha ya uchaguzi huu. Muungano wa vyama vikuu iwe njia ya dharura tuu.Tatu:FDP kama washirika wepya wanabidi wadhihirishe wanachokiweza. Haitokua rahisi kwa waliberali, na nne Wana SPD wakalie viti vya upinzani wapate kujirekebisha. Kwa jumla, mtu anaweza kusema matokeo ya uchaguzi mkuu ni ya maana kwa siasa ya nchi hii hata kama hali jumla inatazamiwa kuwa ngumu kidogo.

Deutschland Bundestagswahlen 2009 SPD Pressekonferenz Frank-Walter Steinmeier
Frank-Walter Steinmeier anapanga kuongoza SPD katika upande wa upinzaniPicha: AP

Gazeti la mjini DRESDEN pia SÄCHSISCHE ZEITUNG lina maoni sawa na hayo na linaandika:

Pengine hii ni fursa nzuri kwa wana Social Democrat wa Ujerumani. Wapiga kura wamewatimua vibaya sana madarakani. Hivi sasa wanaweza, wakiwa upande wa upinzani, kutafakari na kurejesha moyo wa kijamaa. Moyo wao ule ule wa jadi ambao wafuasi wa mrengo wa shoto, Die Linke, wameudaka na kufanikiwa.