1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi nchini Afghanistan

17 Agosti 2009

Uchaguzi huu wa Afghanistan ni mtihani mkubwa kwa mkakati mpya wa Rais Barack Obama unaozingatia zaidi kuwaangamiza Wataliban baada ya vita vya miaka saba.

https://p.dw.com/p/JCdy
Rais Hamid Karzai wa Afghanistan katika kampeni zake za mwishoPicha: PA/dpa
Rais Hamid Karzai na mpinzani wake mkuu katika uchaguzi wa urais nchini Afghanistan leo wanafanya kampeni zao za mwisho kabla ya uchaguzi wa Alhamisi wiki hii. Hata hivyo tishio la mashambulizi na ushawishi wa viongozi wa makundi kadhaa ya wapiganaji inatilia shaka matokeo ya uchaguzi huo wa pili nchini Afghanistan. Kiongozi wa zamani wa kundi la wapiganaji la Uzbek, generali Abdul Rashid Dostum alirejea nchini Afghanistan jana kutoka uhamishoni nchini Uturuki katika kile kinachoonekana kuwashawishi wafuasi wake kumuunga mkono Rais Hamid Karzai ili apate idadi kubwa ya kura kuzima uwezekano wa kufanyika kwa duru ya pili ya uchaguzi. Kura za maoni zinaonyesha Karzai anaongoza kwa umaarufu, kwa kiasi cha asili mia 45 na iwapo hatopata asili mia 50 itabidi aingie tena debeni katika duru ya pili, na mpinzani wake mkuu Abdullah Abdullah ambaye alikuwa waziri wake wa zamani wa nchi za nje. Kuzuka kwa mashambulizi pia kunatishia kumharibia Karzai ushindi wa duru ya kwanza. Wapiganaji wa Kitaliban wameapa kuvuruga uchaguzi huo, na hili huenda likasababisha idadi ndogo ya watu kujitokeza kupiga kura hasa katika maeneo yanayokaliwa na kabila la Pashtun wanaomuunga mkono kwa dhati Hamid Karzai. Hapo siku ya Jumamosi Wataliban walikiri kuwa ndio waliotekeleza shambulizi kubwa la bomu katikati mwa mji mkuu Kabul. Wafghani saba waliuawa na raia wengine 90 kujeruhiwa. Wanajeshi 30,000 zaidi wa Marekani wamepelekwa nchini Afghanistan, na kuongeza idadi ya wanajeshi wa nchi za Magharibi nchini humo kufikia 100,000 kwa mara ya kwanza. Walid Karzai kakaake Rais Hamid Karzai anasema wamejaribu kuzungumza na viongozi wa Kitaliban wasichafue uchaguzi. Vikosi vya kijeshi cha Marekani na Uingereza vimefanya operesheni kali na hii imesababisha vifo vya wanajeshi wengi zaidi, tangu vita hivyi vilipoanza miaka minane iliyopita. Na wakati hayo yaliendelea huko Uingereza waziri mkuu wa nchi hiyo Gordon Brown anakabiliwa na wakati mgumu kutokana na kuongezeka kwa vifo vya wanajeshi wa Uingereza nchini Afghanistan. Jana wanajeshi wengine wanne waliuawa na kufikisha idadi ya wanajeshi wa Uingereza waliouawa nchini Afghanistan kufikia 204. Ingawa Gordon Brown amesisitiza mchango wa Uingereza Afghanistan ni muhimu- kura za maoni nchini humo zinaonyesha Wangereza wengi wanasema serikali yao imelemewa nchini Afghanistan. Mwandishi: Munira Muhammad/ AFPE Mhariri: Aboubakary Liongo