1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi nchini Israel

T.Aßmann - (P.Martin)10 Februari 2009

Mashambulizi ya Israel hivi karibuni katika Ukanda wa Gaza,yamewaathiri hata Waarabu wenye uraia wa Kiisraeli wanaoishi ndani ya mipaka ya Israel inayotambuliwa tangu 1967,ambao ni kama milioni 1.2.

https://p.dw.com/p/GqdQ
** FILE ** In this Feb. 4, 2009 file photo Israeli Foreign Minister and Kadima Party leader Tzipi Livni speaks at a campaign event in Kfar Saba, Israel. Pre-election polls show Likud Party leader Benjamin Netanyahu with a lead over Israel's Foreign Minister Tzipi Livni. Elections are scheduled for Feb. 10, 2009. (AP Photo/Tara Todras-Whitehill)
Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel na kiongozi wa chama cha Kadima Tzipi Livni.Picha: AP

Operesheni hiyo ya kijeshi dhidi ya Hamas katika Gaza iliyoua Wapalestina 1,300 wengi wao raia, imewahamakisha wakaazi wa Kiarabu nchini Israel. Kufuatia vita hivyo vya Gaza,wakaazi hao sasa wanahofia mustakabali wao. Kwani wengi hawaamini kuwa hali yao itabadilika au kuwa bora baada ya uchaguzi wa hii leo nchini mwao.

Masuala ya kisiasa na hasa hali inayokutikana katika Ukanda wa Gaza hujadiliwa sana na Waarabu wa Israel kama vile kinyozi Mussa Abu Ali mwenye miaka 64.Lakini uchaguzi wa Israel si mada inayowashughulisha hasa kinyozi Mussa.Anasema familia yake haitopiga kura-si yeye,mkewe wala wanae.Hatompigia kura Myahudi wala Mwarabu. Anasikitika kuwa wote wanatoa ahadi wasizotimiza.Wanapiga porojo tu na hakuna kinachobadilika.

Wasimamizi wa uchaguzi wanatathmini kuwa asili mia 50 tu ya Waarabu wa Israel ndio watakaokwenda kupiga kura.Katika mwaka 2006 asilimia 56 ya kundi hilo walishiriki katika uchaguzi.Lakini tangu hapo,tafrani zao zimezidi kuongezeka amesema kinyozi Mussa huku akikumbuka chaguzi za miongo iliyopita.Anasema.

"Hakuna kilichobadilika tangu miaka sitini iliyopita.Hali ya Wapalestina inaendelea kuwa mbaya.Sitaraji cho chote katika uchaguzi huu.Yeyote yule atakaeshinda, ikiwa ni Netanyahu,Livni au Barak,hali ya mambo daima itabakia kama ilivyo."

Kiongozi wa chama cha Likud Benjamin Netanyahu anataka kusitisha majadiliano ya kuundwa kwa taifa la Palestina.Nae Waziri wa Mambo ya Nje Zipi Livni mgombea mkuu wa chama cha Kadima,alipokuwa akifanya kampeni ya uchaguzi alipendekeza kuwa ikifanikiwa kuundwa taifa la Palestina,basi kwa maoni yake hiyo pia itakuwa nchi ya Waarabu wanaoishi Israel.Matamashi kama hayo ya mrengo wa kulia yanachochea hofu miongoni mwa Waarabu wa Israel wapatao kama milioni 1.4 ambao ni asilimia 18 ya raia wote nchini Israel.

Mteja mmojawapo wa kinyozi Mussa anasema,anajua nani atakaeshinda uchaguzi wa leo.

"Netanyahu atashinda.Yeye anawachukia Waarabu.Miye nina miaka 75 na sioni faida yo yote katika uchaguzi huu.Netanyahu anatuchukia."

Waarabu wa Israel walio wachache wana wajumbe 13 katika bunge la Israel. Lakini uchunguzi uliofanywa unaonyesha kuwa katika siku zijazo idadi ya wajumbe wa kundi hilo dogo itapunguka sana.Sababu ni kwamba Waarabu wa Israel wengi,kama vile kinyozi Mussa hawataki tena kupiga kura kwa sababu ya kutafrika na kuvunjika moyo.