1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi nchini Msumbiji

28 Oktoba 2009

<p>Huko Msumbiji, nchi ilioko kusini mashariki ya Afrika, leo karibu watu milioni kumi wanakwenda kupiga kura kuchagua rais na wabunge wa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/KHQ4
Rais Armando Guebuza akizungumza wakati wa kampeni ya uchaguzi huko Mutarara, Jimbo la TetePicha: picture alliance/landov
Kwa vile upande wa upinzani umegawika, yaonyesha ni hakika kwamba chama tawala cha Frelimo kitashinda. Chama hicho kimekuwa kikiitawala Msumbiji tangu  ilipopata uhuru kutoka kwa Ureno mwaka 1975. Pia inatarajiwa kwamba rais wa sasa na mtetezi wa Chama cha Frelimo, Armando Guebuza, atarejea madarakani. Na huo utakuwa muhula wa pili wa urais kwa mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 66. Pia wa bunge wa mikoa watachaguliwa upya. Inatarajiwa kwamba matokeo ya uchaguzi huu yatatangazwa hapo Novemba 12. 

Rais Armando Guebuza alikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kupiga kura leo, akitumbukiza kura yake saa moja baada ya vituo vilipofunguliwa saa 12 za asubuhi. Chama tawala cha Frelimo kinachuana na  chama cha Ki-Conservative cha Renamo, na vyama hivyo viwili vilipigana vita vya kienyeji vilivodumu miaka 16 baina yao kati ya mwaka 1976 na 1992. Renamo ilikuwa inasaidiwa na serikali ya kibaguzi ya Afrika Kusini ya wakati huo pamoja na Rhodesia ambayo sasa ni Zimbabwe.

Watu milioni 10.3 wana haki ya kupiga kura hii leo kwa ajili ya uchaguzi wa urais na wa bunge la wajumbe 250. Licha ya hayo, mabunge mepya ya mikoa 10 yanachaguliwa wakati huo huo. Mpiga kura Vasco Munguambe ambaye amekuwa leo asubuhi akingojea kupiga kura, alisema: " ni muhimu kupiga kura kwa vile mustakbali wa nchi unaamuliwa; nataka kutoa maoni yangu juu ya vipi hali ya baadae ya nchi iwe."

In this photo taken Sunday, Oct. 25. 2009, supporters attend a ruling Frelimo party election rally in Nampula city, Mozambique. President Armando Guebuza,
Mashabiki wa chama cha Frelimo wakati wa Kampeni ya uchaguzi huko Nampula.Picha: AP

Katika  miaka michache iliopita, Msumbiji yenye wakaazi milioni 20, moja wapo ya nchi maskini kabisa duniani, imekuwa moja wapo ya nchi inayosifika sana barani Afrika kwamba imepata mafanikio. Uwekezaji mkubwa wa kutoka ng'ambo katika sekta za gesi ya ardhini, makaa, umeme wa kutoka  nguvu za maji, madini pamoja na nyinginezo zimeufanya uchumi wa nchi hiyo kupanda, na ukuuaji huo unatarajiwa kufikia asilimia tano mwaka huu.

Armando Guebuza, mfanya biashara aliye tajiri, anatazamiwa kwa urahisi kushinda kwenye uchaguzi huu na kuwa rais kwa kipindi cha pili.  Katika mkutano wa hadhara wa kampeni yake, rais Gebuta alisema:

" Chama cha Frelimo kitafanya kile ambacho maisha kimefanya nchini msumbiji. Hakika ushindi ni wetu."

Na kwa nafasi ya pili, kiongozi wa Renamo, Alfondo Dlakama, anakabiliana na ushindani mkali kutoka kiongozi wa chama kipya, Daviz Simango, ambaye ni meya wa mji wa Beira ulioko katikati ya nchi hiyo. Yeye alikiacha chama cha Renamo mwaka jana  baada ya kutokea kutofahamiana ndani ya chama  hicho, na akaamua kuunda chama cha Democratic Movement, MDM. Amekuwa na miezi sita kutayarisha kampeni ya  uchaguzi ya chama chake kipya. Chama hicho, ambacho kimezusha hamu miongoni mwa wapiga kura vijana, kimezuiliwa na tume ya uchaguzi, ilio na wanachama wa Frelimo na Renamo, kushindania baadhi ya wilaya za uchaguzi kwa ajili ya uchaguzi wa bunge.  Kwa ujumla, vyama 19 vinashindana katika uchaguzi huu, lakini ni Frelimo na Renamo tu vilivokubaliwa kuweka watetezi katika kila wilaya ya uchaguzi.

Ardio Evaristo, msemaji wa Chama cha MDM, alikuwa na haya ya kusema kabla ya  siku ya leo ya uchaguzi:

"Demokrasia ya Msumbiji iko katika hali  mbaya. Vyama vya zamani vya Frelimo na Renamo maisha vimefikiri vimeiletea Msumbiji demokrasia, lakini vyama hivyo havitendi  kwa njia ya kidemokrasia. Vinawadharau wananchi na vinafanya kama vile vinaimiliki nchi nzima. Hakuna demokrasia ya kweli, wanalitumia tu midomoni neno demokrasia ili kuwaweka gizani sehemu ya wananchi."

Matokeo ya mwanzo kutoka vituo 12,000 vya kupigia kura yanatarajiwa kuanza kumiminika baada ya vituo hivyo kufungwa jioni ya leo, lakini ni Novemba 2 ambapo matokeo ya mwisho yatatangazwa.

Mwandishi: Othman Miraji /AFP

Mhariri:M.Abdul-Rahman