1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi Ujerumani: Merkel, Schulz kumenyana mdahalo wa TV

Iddi Ssessanga
3 Septemba 2017

Wagombea wa ukansela wa Ujerumani kupitia vyama vya CDU na SPD watachuana katika mdahalo muhimu kwenye vituo vyote vinne vikuu vya televisheni unaotarajiwa kutazamwa na zaidi ya watu milioni 15. Merkel atabiriwa ushindi.

https://p.dw.com/p/2jHZN
Deutschland Wahlplakate Schulz Merkel
Picha: picture-alliance/F. May

Zikiwa zimesalia wiki tatu tu hadi kufanyika uchaguzi mkuu, mdahalo wa pekee na unaosuburiwa kwa hamu nchini Ujerumani kati ya wagombea wakuu wa juu wa nafasi ya kansela, Angela Merkel na Martin Schulz unaanza saa mbili kwa saa za Ulaya ya Kati (saa tatu za Afrika Mashariki) siku ya Jumapili, na kuonyeshwa katika vituo vikuu vya ARD, RTL, Sat.1 na ZDF. Mdahalo huo unatoa fursa kwa wagombea hao kuoneshana nguvu mbele ya umma, kuelekea kura itakayofanyika Septemba 24. Wagombea hao watahojiwa na watangazaji wanne.

Uchunguzi wa maoni uliofanywa na shirika la utafiti wa maoni la Forsa kwa niaba ya jarida la habari la Stern, umeonesha kuwa nusu ya wapiga kura wamepanga kutazama mdahalo huo -- na asilimia 20 ya waliohojiwa walisema mdahalo huo unaweza kubadili namna watakavyopiga kura siku ya uchaguzi.

Mdahalo huo wa dakika 90 utampa fursa Martin Schulz, mgombea wa chama cha siasa za mrengo wa wastani wa kushoto cha Social Democratic (SPD), kujaribu kuwashawishi Wajerumani kuachana na kansela wao kutoka chama kinacholemea mrengo wa kulia cha Christian Democratic Union (CDU), ambaye anaweza kumpiku Schulz kwa sababu amekuwepo madarakani kwa miaka 12, kipindi ambacho Ujerumani imefanikiwa kuvuka changamoto kadhaa bila kuyumba.

Wahlplakate in Berlin
Mabango ya wagombea wa vyama vikuu, Angela Merkel wa CDU na Martin Schulz wa SPD yakionekana katika mitaa wa mji wa Berlin.Picha: picture-alliance/dpa/C. Peters

Schulz amejaribu kujengea hoja zake juu kile kinachochukuliwa kama ukosefu wa haiba kwa upande wa Merkel, pamoja na shauku katika kampeni yake, akiangazia ujana wake uliokuwa umegubikwa na changamoto pamoja na uzoefu wake katika siasa za barani  Ulaya. Wakati huo huo amemshutumu Merkel kwa kutoonyesha hisia na kujitenga na wapigakura kupitia mwenendo wake usioyumba.

"Miaka minne ya mwisho ya zama za Kohl ilikuwa ni kipindi cha mkwamo na maumivu ya kisiasa. Nataka kuinusuru Ujerumani dhidi ya kutokea hayo tena," alisema Schulz, akimaanisha mhula wa nne madarakani wa Helmut Kohl, rekodi ambayo Merkel ataifikia iwapo ataibuka mshindi katika uchaguzi wa Septemba 24.

Merkel amezungumzia mafanikio ya Ujerumani wakati akijaribu kuwahakikishia wahafidhina kuhusu huduma za kipolisi na uhamiaji. Merkel aliliambia gazeti la Rheinische Post siku ya Jumamosi kwamba anataka kuendeleza ukaguzi wa polisi kwenye mipaka ya Ujerumani, ambao ulianzishwa Septemba 2015 na muda wake unatrajiwa kumalizika Novemba mwaka huu.

Vitisho kutoka ofisi ya kansela

Merkel amekosolewa pia na vyombo vya habari kutokana na muundo mkali uliochaguliwa kwa ajili ya mdahalo kupita vituo vya televisheni vya umma vya ARD na ZDF. Waongozaji hawana nafasi kubwa ya kutoka nje ya maswali yalioandaliwa kabla, na hakutakuwepo raia katika studio za Televesheni, licha ya waaongozaji wa kipindi kuomba uhuru zaidi wa kufanya mambo.

"Huu ndiyo mfumo sawa uliotumika mwaka 2009 na 2013, na umeonyesha kuwa mzuri," Merkel aliliambia jarida la habari la Der Spiegel. Merkel alishinda chaguzi zote mbili. Lakini mhariri mkuu wa zamani wa televisheni ya ZDF Nikolaus Brender aliutaja mfumo huo kuwa ni "vitisho kutoka ofisi ya kansela", akimaanisha kwamba vinginevyo Merkel asingeshiriki.

Infografik Deutschland Trend extra Direktwahl Merkel Schulz
Kulingana cha chunguzi za maoni ya raia za karibuni, Merkel anaongoza dhidi ya Schulz.

Umaarufu wa Merkel ni mzuri kuliko mwaka 2013

Licha ya ukosoaji huu wote, Ujerumani huenda tayari imeshafanya uamuzi wake. Uchunguzi wa hivi karibuni  kutoka kampuni ya Infratest dimap umeonyesha kuwa chama cha CDU kiko mbele zaidi ya SPD, ambapo Merkel ana asilimia karibu 37 ya uungaji mkono dhidi ya asilimia 23 ya SPD.

Wajerumani wanaonekana kushawishika na ushindi wa Merkel kabla ya mdahalo huo. Uchunguzi uliofanywa na shirika la utangazaji la umma la ARD ulionyesha kuwa asilimia 64 ya waliohojiwa walitabiri kuwa kansela huyo angeshinda mdahalo huo, huku asilimia 17 tu wakiamini Schulz atashinda.

Tarakim hizi zinavutia zaidi ikilinganishwa na za miaka minne iliopita, wakati asilimia 49 ya waliohojiwa waliamini Merkel angeshinda na asilimia 26 walitabiri ushindi wa mgombea wa chama cha SPD, Peer Steinbrück.

Mwandishi: Elizabeth Schumacher

Tafsiri: Iddi Ssessanga

Mhariri: Yusra Buwayhid