1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi utaitishwa Machi 17 nchini Israel

3 Desemba 2014

Wabunge wa Israel wamekutana kuupigia kura mswaada wa sheria itakayoruhusu kuitishwa uchaguzi wa kabla ya wakati kufuatia mzozo katika serikali ya muungano inayoongozwa na Benjamin Netanyahu.

https://p.dw.com/p/1DydK
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akizungumza na waandishi habariPicha: Reuters/G. Tibbon

Kwa mujibu wa Radio Israel wabunge wamekubaliana uchaguzi mpya uitishwe Marchi 17 mwakani.Uamuzi huo lakini ni hatua ya mwanzo tu.Hatua ya pili inatarajiwa wiki inayokuja pale wabunge watakapaoamua bunge livunjwe,miaka miwili kabla ya tarehe iliyopangwa.

Serikali ya sasa iliyoingia madarakani mapema mwaka jana inazongwa na matatizo na tofauti za maoni kuhusu mada muhimu zinazoikabili nchi hiyo.

Mivutano ilizidi makali wiki iliyopita pale Netanyahu alipohimiza iidhinishwe kanuni inayoitaja Israel kuwa "Taifa la kiyahudi" sheria ambayo wakosoaji wanahisi inawabagua waisrael wenye asili ya kiarabu.

Jana waziri mkuu Benjamin Netanyahu aliwafukuza kazi mawaziri wawili waasi,waziri wa fedha Yair Lapid na waziri wa sheria Tsipi Livni.Netanyahu anawatuhumu mawaziri hao wanaoongoza kila mmoja chama cha siasa za wastani,kutaka "kuandaa njama ya mapinduzi" akisema "hawezi kuvumilia upinzani ndani ya serikali yake."

Netanyahu ndie chanzo cha kuitishwa uchaguzi

Utafiti wa maoni ya umma uliosimamiwa na vituo vya televisheni umeonyesha chama cha kihafidhina cha waziri mkuu Netanyahu,Likud kingeibuka na ushindi kwa mara nyengine tena na kudhibiti wingi wa viti bungeni pindi uchaguzi ungeitishwa hii leo na kwa namna hiyo kumhakikishia mhula wa nne kama waziri mkuu madarakani.

Israel Koalition Justizministerin Livni
Aliyekuwa waziri wa sheria Tsipi LivniPicha: Gali Tibboni/AFP/Getty Images

Wakosoaji wa waziri mkuu Netanyahu wanamtuhumu kuchochea makusudi mvutano serikalini ili aachane na wafuasi wa siasa za wastani na kupalilia njia ya kuibuka na ushindi vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia.

Wakati huo huo wabunge wa Ufaransa wamepiga kura kuunga mkono kutambuliwa dola la Palastina -uamuzi uliozusha ghadhabu nchini Israel ambako viongozi wa serikali wanasema "hatua za upande mmoja zitavuruga juhudi za kusaka amani ya mashariki ya kati."

Laurent Fabius atoa muda wa miaka miwili

Wabunge 339 dhidi ya 151 wa Ufaransa wameungwa mkono mswaada unaoihimiza serikali iitambue dola ya Palastina kama njia mojawapo ya" kufikia ufumbuzi wa kudumu wa mzozo wa mashariki ya kati."Hata hivyo ubalozi wa Israel mjini Paris unasema kura hiyo inapunguza uwezekano wa kufikiwa makubaliano kati ya Israel na Palastina."

Symbolbild Frankreich Nationalversammlung Palästina
Bunge la Ufaransa lapiga kura kutaka serikali iiitambue dola ya PalastinaPicha: picture-alliance/dpa/Yoan Valat

Kura hiyo ambayo haiilazimishi serikali ya Ufaransa kuitekeleza imesadifu wakati ambapo nchi za Umoja wa Ulaya zinasaka njia mbadala ya kuufufua utaratibu wa amani wa mashariki ya kati.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Laurent Fabius alisema hapo awali Paris itaitambua dola ya Palastina ikiwa juhudi zote za kidiplomasia zitashindwa kwa mara nyengine tena na kuhimiza ufumbuzi upatikane mnamo muda wa miaka miwili inayokuja.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AP/AFP/Reuters

Mhariri:Yusuf Saumu