1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa DRC upo mlangoni

23 Novemba 2011

Wakongo milioni 32 wanachagua rais na wabunge 500 hapo Novemba 28 katika uchaguzi wa pili tangu uhuru wa Kongo mwaka 1960, ambao ikiwa utafaulu utaimarisha demokrasia.

https://p.dw.com/p/13BdP
Bendera ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Bendera ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya KongoPicha: Fotolia/ferkelraggae

Wagombea 11 wanawania kiti cha urais, wengine 18, 000 wanapigania viti  500. Kampeni ya uchaguzi ya mwezi mmoja inamalizika Novemba 26, lakini mazingira ya kuanza kwa kampeni hizo yalikuwa ya wasiwasi na visa vya umwagaji damu.

Kura inatarajiwa kupigwa Novemba 28, matokeo rasmi ya uchaguzi yatatangazwa Disemba 6, na kuapishwa kwa rass mpya kutafanyika Disemba 20.

Umoja wa Ulaya umewatuma waangalizi 147, huku Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ikituma waangalizi  2000, na Kanisa Katoliki na mashirika ya kiraia yakiwa na waangalizi 30, 000 wa uchaguzi.

Wagombea wa Urais


Kati ya wagombea 11 wa nafasi ya uraisi, wanne kati yao ndio wanaopewa nafasi kubwa zaidi ya kupata kura nyingi. Wagombea hao ni Joseph Kabila Kabange, Etienne Tshisekedi wa Mulumba, Leon Kengo wa Dondo na Vital Kamerhe Lwa Kanyinginyi.

Joseph Kabila Kabange
Joseph Kabila KabangePicha: AP

Joseph Kabila Kabange: Anatoka kwenye chama tawala cha PPRD na ndiye rais wa sasa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Kabina ana umri wa miaka 40, akiwa ameingia madarakani akiwa na miaka 30 tu hapo mwaka 2001, baada ya kuuliwa kwa baba yake, Laurent Désiré Kabila, aliyekuwa rais. Alichaguliwa mwaka wa 2006 kwenye duru ya pili dhidi ya mpinzani wake, Jean Pierre Bemba. Joseph Kabila anatoka jimbo la Katanga, lakini alizaliwa mwaka wa 1971 mtaani Fizi jimboni Kivu ya Kusini, ambako baba yake alikuwa msituni akiendesha harakati za kijeshi dhidi ya utawala wa Mobutu Sese Seko. Kabila amegombea kiti cha urais kama mgombea huru.

Etienne Tshisekedi wa Mulumba: Ana miaka 79, mpinzani mkongwe tangu mwaka wa 1982 dhidi ya utawala wa Mobutu. Anaongoza chama cha UDPS na anashiriki kwa mara ya kwanza kwenye uchaguzi, baada ya kususia ule wa 2006. Tshisekedi anatoka jimbo la Kasaï-Oriental, katikati mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Léon Kengo wa Dondo
Léon Kengo wa DondoPicha: flickr/on Third World Conference of Speakers of Parliamen

Leon Kengo wa Dondo: Waziri Mkuu wa zamani wa muda mrefu wa Sese Seko Mobutu. Akiwa na miaka 76, Léon Kengo wa Dondo ni kiongozi wa chama cha UFC, ni mwanasheria na pia Spika wa Baraza la Seneti ya Kongo toka mwaka wa 2007. Kengo anatoka jimbo la Equateur, kaskazini magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Kengo ameongoza chama cha UFC.

Vital Kamerhe Lwa Kanyinginyi: Ukimuacha Joseph Kabila, Vital Kamerhe ndiye 'kijana' zaidi miongoni mwa wagombea wanaopewa nafasi kwenye uchaguzi huu, akiwa na miaka 52. Alikuwa mshirika mkubwa wa Rais Joseph Kabila na aliongoza chama tawala cha PPRD kabla ya kuunda chama chake mwenyewe cha UNC, mwishoni mwa mwaka 2010. Vital Kamerhe alikuwa Spika wa Bunge tangu 2007-2009. Anatoka jimbo la Kivu ya Kusini.

Mbali na wagombea hawa wanne, kuna wagombea wengine saba, ambao ni paomoja na Nzaga Mobutu, mtoto wa rais wa zamani, Mobutu Sese Seko, na Antipas Mbusa Nyamwisi, ambaye ni kiongozi wa zamani wa kundi la waasi la RCD/KML. Mbusa Nyamwisi anatokea mkoa wa Beni, katika jimbo la Kivu ya Kaskazini.

Mwandishi: Saleh Mwanamilongo

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman