1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Israel kufanyika Januari 22

MjahidA16 Oktoba 2012

Bunge la Israel limeridhia mswada wa serikali mapema hii leo wa kuvunja bunge na kujiandaa kwa uchaguzi wa mapema

https://p.dw.com/p/16QgU
Bunge la Israel
Bunge la IsraelPicha: picture-alliance/dpa/dpaweb

Uchaguzi huo mkuu uliokuwa umepangwa kufanyika baada ya miezi tisa, sasa utafanyika January 22.

Upinzani uliokuwepo wakati wa kupitisha mswada huo uliopigiwa kura mara tatu ulikuja wakati ulipokuwa unasomwa kwa mara ya pili, na mbunge aliyekuwa ameupinga muswaada huo alikiri kuwa aligusa alama ya kuupinga kwa bahati mbaya wakati walipokuwa wanatumia kifaa cha elekroniki kuupigia kura mswaada huo.

Awali katika hotuba yake wakati alipokuwa anafungua bunge, waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliwaomba wabunge kuidhinisha Januari 22 kama tarehe ya uchaguzi mkuu ujao.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: dapd

Waziri mkuu huyo aliitisha uchaguzi wa mapema kufuatia mgawanyiko uliopo ndani ya serikali yake ya muungano, juu ya bajeti ya nchi. Sasa baada ya mswada huo kupitishwa na bunge kuvunjwa, bunge hilo litakuwa katika mapumziko ya kujitayarisha kwa uchaguzi lakini wakati wowote linaweza kuitwa tena iwapo kutakuwa na jambo la dharura.

Netanyahu amesema yeye pekee ndiye aliye na uwezo wa kuiongoza Israel, huku akitoa mifano ya mafanikio ya serikali yake tangu alipoingia madarakani mwezi Marchi mwaka wa 2009. Matamshi hayo ya Netanyahu yaliwakasirisha wabunge wa upinzani.

Aidha kuhusu maswala ya silaha za nyuklia, Netanyahu amesema mtu yeyote ambaye hachukulii kwa umakini kitisho cha silaha za Nyuklia za Iran, kwa taifa la Israel hapaswi kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo hata siku moja, akisema kwamba kwa sasa Israel ina uwezo wa kuchukua hatua dhidi ya iran jambo ambalo awali lilikuwa haliwezekani.

Upinzani haufurahishwi na uongozi wa Netanyahu

Kwa upande wake kiongozi wa upinzani Shaul Mofaz, aliyezungumza jukwaani baada ya Netanyahu, alimkashifu waziri mkuu huyo, akimshutumu kwa kushindwa kufanya kazi yake na kuwa Israel imetumbukia mahali pabaya zaidi haswaa baada ya serikali ya Netanyahu kuingia madarakani.

Kiongozi wa Upinzani Israel Schaul Mofas
Kiongozi wa Upinzani Israel Schaul MofasPicha: AP

Uchaguzi wa Israel ulikuwa ufanyike October mwaka ujao. Hata hivyo kura ya maoni iliofanywa wiki iliopita imeonesha kuwa iwapo uchaguzi utafanyika hii leo Benjamin Netanyahu na chama chake cha Likud kitashinda kwa kuchukua viti vingi bungeni.

Huku hayo yakiarifiwa inaaminika kuwa siasa za Israel huenda zikachukua mkondo mpya iwapo waziri mkuu wa zamani Ehud Olmert ataamua kurudi kwenye ulingo wa kisiasa.

Mwandishi Amina Abubakar/dpa

Mhariri Yusuf Saumu