1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UChaguzi wa Kenya magazetini Ujerumani

Oummilkheir2 Januari 2008

Wahariri watetea hikma na busara

https://p.dw.com/p/Cj9L
Machafuko ya umwagaji damu KenyaPicha: picture-alliance/ dpa

Mzozo unaozidi makali nchini Kenya unawashughulisha sana wahariri wa magazeti ya Ujerumani ,wanaomulika kwa jicho la hasira hali ya mambo katika nchi hiyo ya Afrika kusini iliyokua ikijivunia sifa hapo awali.

Tunaanhza na gazeti la TAGESZEITUNG la mjini Berlin linaloandika:

„Miaka mitano iliyopita pale wakenya walipomchagua Mwai Kibaki,mwanasiasa huyo aliahidi kupiga vita rushwa ,na kutumiwa vibaya madaraka .Alishangiriwa kupita kiasi.Hii leo hata kutoka nje hasubutu.Polisi na wanajeshi wanateremka majiani,maandamano yamepigwa marufuku na ripoti za waandishi habari kuwekewa vizuwizi:Kibaki anafanya yale yale aliyoyakosoa wakati mmoja,Kwa hivyo mtu asiwakosowe wakenya wanapolalamika kwamba wanahisi wamedanganywa.Wakivunjwa moyo na Kibaki,walipania kutompa kura zao safari hii-hawakuruhusiwa lakini kufanya hivyo.Ghadhabu ni kubwa zaidi miongoni mwa vijana wasiokua na kazi wanaohisi matumaini yao yamemwagiwa mchanga.Na hasira zao,zinaeleweka kwa njia moja au nyengine.“

Likimulika uchaguzi wa rais wa December 27 iliyopita,gazeti la ALLGEMEINE ZEITUNG la mjini Mainz linaongezea:

„Kwamba uchaguzi ni wa udanganyiifu na hadaa,hakuna ambae hakua akijua,hata wachunguzi wa kimataifa walitambua- kama sivyo,kwanini wamekwenda kwa wingi hivyo?Lakini kwamba ulaghai utakua wa aibu hivyo na bayana,hakuna aliyefikiria.“

Kutokana na hali hiyo gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU linajiuliza:

„Eti yote ya nini haya?Mwai Kibaki ameshakamilisha umri wa miaka 76,anatajikana kua mmojawapo wa matajiri wakubwa wa Kenya.Na angekubali kwamba ameshindwa,angeingia katika madaftari ya historia kama kiongozi bora anaestahiki kuigizwa Afrika Mashariki.Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita Kibaki ameiongoza Kenya vizuri zaidi kuwapita viongozi wote wawili waliomtangulia.Kibaki ,akitaka kujiepusha asiingie katika madaftari ya historia kama mtu aliyeichimbia kaburi nchi hiyo inayowavutia watalalii,anabidi azungimze na Odinga badala ya kung’ang’ania msimamo mkali.Pekee kushirikishwa upande wa upinzani madarakani ndiko kutakakosaidia kuzuwia damu isizidi kumwagika.Miaka 76,inamfanya mtu awe na hikma na busara ya kutosha kupima hali namna ilivyo.”

Gazeti la mjini Berlin TAGESSPIEGEL linaandika:

Serikali za Ulaya zinafanya vizuri zinaposita kumtambua Mwai Kibaki kama rais aliyechaguliwa kwa awamu ya pili.Na baada ya Marekani kustaghafiru,baada ya pupa za awali kumtambua mshirika wake katika vita dhidi ya ugaidi,na hilo pia linastahiki kusifiwa.Kwa sababu kwa namna hiyo nchi za magharibi zinaonyesha wazi wazi zinawaunga mkono wapenda demokrasia nchini Kenya.Na wako wengi tuu nchini humo.Idadi kubwa kupita kia-zaidi ya asili mia 70 ya walioteremka vituoni,wakipiga foleni kusubiri zamu yao na jinsi walivyopima kwa makini nani wampe kura zao, ni jambo linalostahiki sifa.Lakini ufumbuzi si rahisi kuupata.Na ikishindikana kuufumbua mzozo wa uchaguzi, basi kutakua na hatari ya Kenya kutumbukia katika janga la vita vya wenyewe kwa wenyewe.Na hapo balaa kubwa litalifika bara la Afrika.“