1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Kiongozi wa Chama cha Upinzani Afrika Kusini

8 Mei 2015

Chama rasmi cha upinzani nchini Afrika Kusini, Democratic Alliance-DA, ambacho pia kinaendelea kuwavutia vijana ambao ni Waafrika weusi, kinamchagua kiongozi wake wikendi

https://p.dw.com/p/1FN5R
Wahlkampf aus Südafrika von Helen Zille
Picha: picture alliance/AP Images

Haya yanafuatia uamuzi wa ghafla wa kiongozi wa kitaifa wa chama hicho mwenye bidii-Helen Zile, wa kung'atuka baada ya kushikilia nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka minane. Wagombea wawili wakuu-Mmusi Maimane na Wilmot James wanachuana kuchukua nafasi hiyo.

Helen Zile, aliyekuwa kiongozi wa Democratic Alliance amenukuliwa akisema kila mara watu walimuuliza ataendelea hadi lini kuwa kiongozi wa chama hicho. Jawabu lake likawa:

"Nitafahamu wakati ukifika, na ninaamini, wakati huu ni mwafaka, na hii ndiyo sababu sitajitokeza kuwania kuchaguliwa tena Mei 9. "

Wakati Helen Zille mwenye umri wa miaka 64 alipoteuliwa kukiongoza chama rasmi cha upinzani, Democratic Alliance mwaka 2007, chama hicho kilipewa jina la, chama cha asimilia mbili kwa vile kilivutia asilimia mbili tu ya wapigakura, wengi wao wakiwa raia wenye asili ya Kizungu.

Lakini miaka minane baadaye, chama cha DA kimeimarika kwa kiasi kikubwa kutokana na uongozi wa Zille chama hicho kilivutia zaidi ya asilimia 23 ya wapigakura kutoka upande Waafrika weusi na Wazungu kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana. Chama cha DA vilevile kinadhibiti Mkoa wa Western Cape, eneo la pekee miongoni mwa mikoa tisa ambayo chama tawala cha ANC hakina ushawishi.

Bunge la Afrika Kusini mjini Cape Town
Bunge la Afrika Kusini mjini Cape TownPicha: picture-alliance/AP Photo

Mmojawapo wa wagombea wawili wa nafasi inayoshikiliwa na Zile ni mwanasiasa chipukizi mwenye umri wa miaka 35, Mmusi Maimane, ambaye amekuwa kiongozi wa DA bungeni kuanzia mwaka jana. Maimane tayari ameshajipatia umaarufu kwakukosoa vitendo vya rushwa pamoja na kuitangaza Afrika Kusini kama taifa la watu wote. Maimane anasema:

Changamoto kuu ni kwamba tuna vyama vingi vya siasa vinavyoangazia yaliyopita. Yetu ni kusema namna tunavyoboresha hali siku zijazo. Ni vipi tutakavyohakikisha kuwa watu wa Afrika Kusini watafahamu kuwa tuna uchumi jumlishi, wanakuwa na mfumo wa elimu unaowapa nguvu, kwamba kuijenga jamii isiyo na ubaguzi kwa kigezo cha asili na DA kinapigania masuala hayo kwa vile wapo wanaojaribu kuturejesha nyuma.

Maimane anaamini kwa dhati kuwa Afrika Kusini itafikia mabadiliko ya uongozi wa kisiasa ndani ya kipindi cha miaka 10 ijayo .Na binafsi yuko tayari kuongoza mchakato huo punde atakachochaguliwa. Amesema ikiwa jamii itakosa uthabiti, mabadiliko yanachapushwa. Mashambulizi dhidi ya wageni, kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira, yate yanaashiria kuwa taifa linakabiliwa na taharuki kubwa. Ameongeza kusema kuafikiwa kwa mabadiliko kunawategemea raia wa nchi hiyo akisema anaamini kuwa Afrika Kusini litakuwa eneo tofauti akisema anamini ama mwaka wa 1919 au 2014, yatakuwapo mabadiliko ya siasa nchini humo.

Profesa Wilmot James mwenye umri wa maiaka 62, aliyekuwa mmoja wa wanaharakati waliopinga ubaguzi wa rangi, ni mgombea mwengine aliye na matumaini ya kuchaguliwa kuwa kiongozi mpya wa chama cha Democtaric Alliance. James ambaye ni mbunge na mwenyekiti wa Baraza la Kishirikisho la chama cha DA anasema lengo lake la kukiongoza chama hicho ni kusitisha kudorora kwa hali nchini humo. Anasema:

"Nina ufahamu kuhusu madhara ya ubaguzi wa rangi, nilikuwa mmoja wa waliopigania kutokomezwa kwa ubaguzi wa rangi, nilikuwa miongoni mwa waliohakikisha kuwa demokrasia hii inakuwa endelevu. Imewakosea raia wa Afrika Kusini na ninaamini kuwa DA ndicho chama cha pekee nikichosalia na chenye uwezo wa kukabili ufisadi. "

Huku zikisalia saa chache tu kabla ya kuchaguliwa kwa kiongozi mpya wa chama hicho, inaonekana kwamba huenda Mmusi Maimane akampiku Wilmot James. Amepokea uungwaji mkono ulio wazi kutoka kwa viongozi kadhaa wakuu katika chama cha DA, ikiwa ni pamoja na Meya wa Cape Town, Patricia De Lille, aliyekuwa mwanaharakati kupinga ubaguzi wa rangi na mwanachama wa Umoja wa Afrika.

Wachanganuzi wa siasa na wanachama wa DA wanasema yeyote atakayechukua nafasi ya Zille, atatarajiwa kushirikiana na wanachama wengine ili kukifanya chama hicho cha Democratic Alliance kuongoza katika kipindi cha miongo kadhaa ijayo.

Mwandishi: Geoffrey Mung'ou

Mhariri: Saum Yusuf