1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Marekani magazetini

5 Novemba 2012

Uchaguzi wa rais nchini Marekani, na mkutano wa viongozi wa vyama vinavyounda serikali kuu ya muungano mjini Berlin ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani .

https://p.dw.com/p/16crP
Wagombea wa kiti cha rais Barak Obama (kulia ) na Mitt RomneyPicha: picture-alliance/dpa

Tuanzie na uchaguzi wa Marekani.Wajerumani wengi wangependelea kumuona rais anaemaliza wadhifa wake,Barack Obama akiendelea na mhula wa pili madarakani.Gazeti la "Münchener Merkur" linaandika:

Kama mjerumani anapendelea kumuona rais wa Marekani akiendelea na wadhifa huo,sababu ni kwamba Obama amejaribu kwa dhati kutekeleza kivitendo kauli mbiu-"Mageuzi"-kuanzia kuondowa vikosi vya Marekani nchini Iraq,kupitia mwito wa kuzungumza na waislam hadi azma ya kuanzisha enzi mpya pamoja na Urusi.Na amejifunza pia kwamba siasa daima inafuata masilahi na sio dhamiri njema.Kutokana na mgogoro mkubwa wa fedha ulimwenguni na majanga tofauti kuanzia Afghanistan kupitia Pakistan hadi kufikia Afrika na Iran,ulimwengu utabahatika ukimpata mwanasiasa kama Obama anaeitambua hali halisi ya mambo namna ilivyo badala ya Romney ambae makosa pengine hatoweza kuyaepuka.

USA Kapitol in Washington
Jengo la Kapitol mjini Washington-makao makuu ya baraza la Congress la MarekaniPicha: picture-alliance/dpa

Hata gazeti la "Lübecker Nachrichten" linahisi ni muhimu kwa Obama kuendelea na mhula wa pili licha ya kasoro zilizoko.Gazeti linaendelea kuandika:

Mshindi huyo wa tuzo ya amani ya Nobel amekuja kuwa rais pekee aliyetuma madege chungu nzima yasiyoendeshwa na marubani na yanayouwa.Hajafanikiwa kuondowa fedheha ya Guantanamo,kila mmarekani mmoja kati ya sita anategemea msaada wa chakula na asili mia kumi ya wananchi wanamiliki asili mia 75 ya utajiri wa nchi hiyo.Licha ya yote hayo lakini ni muhimu aendelee na wadhifa wake madarakani.Marekani na wakaazi wake milioni 310 ni nchi iliyogawika.Romney akichaguliwa kuwa rais, mwanya huo utazizi kupanuka.

Angela Merkel Philipp Rösler FDP CDU Regierung Koalition
Kansela Angela Merkel (kulia) na mwemyekiti wa chama cha FDP Philipp RöslerPicha: dapd

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamezungumzia pia kuhusu mkutano wa viongozi wa vyama vitatu vinavyounda serikali kuu ya muungano mjini Berlin:kansela Angela Merkel wa chama cha CDU,Horst Seehöfer wa chama cha CSU na Philipp Rösler wa chama cha FDP.Gazeti la "Neue Osnabrücker Zeitung" linaandika:

"Kishindo cha ufanisi na matarajio ya uchaguzi mkuu msimu wa mapukutiko mwakani ndiyo mambo yaliyogubika mkutano wa viongozi katika ofisi ya kansela.Uwezo wa serikali ya muungano wa vyama vya CDU/CSU na waliberali ndio unaowekewa suala la kuuliza na wakati huo huo uwezo wa kansela Angela Merkel.Kwasababu wananchi wamechoshwa kila wakati kusikia hadharani mivutano kati ya CDU na washirika wake wadogo-CSU na FDP.Ni sawa kwamba maoni tofauti katika serikali ya vyama vitatu ni jambo la kawaida katika mfumo wa kidemokrasi.Hata hivyo wananchi wanataka kuona matokeo bayana-na mara nyingi hayaonekani.Wakati wa muungano wa CDU/CSU na SPD hali ilikuwa bora zaidi.Si hasha kwa hivyo kama watu wanatamani tena enzi hizo.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri:Yusuf Saumu