1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Mauritania waelekea awamu ya pili

Josephat Charo12 Machi 2007

Uchaguzi wa rais nchini Mauritania unaelekea awamu ya pili huku wagombea wote wakiwa washindwa kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura zinazohitajika kushinda uchaguzi huo.

https://p.dw.com/p/CHIM
Wafuasi wa mgombea urais wa Mauritania Ahmed Ould Daddah
Wafuasi wa mgombea urais wa Mauritania Ahmed Ould DaddahPicha: AP

Mauritania inaelekea katika awamu ya pili ya uchaguzi wa rais hii leo huku wagombea wawili wa wadhifa wa urais wenye nafasi kubwa ya kushinda wakishindwa kupata kiwango cha kura kinachohitajika kushinda. ´Tunaelekea awamu ya pili ya uchaguzi,´ amesema afisa mmoja wa wizara ya maswala ya ndani nchini Mauritania ambaye hakutaka jina lake litajwe. Hayo ni kwa mujibu wa matokeo ya awali kutoka mikoani huku asilimia 86 ya kura zote zilizozopigwa zikiwa tayari zimehesabiwa. Raundi ya pili ya uchaguzi huo huenda ikafanyika mnamo tarehe 25 mwezi huu.

Wagombea wawili wa urais wamejiongezea uwezo wao wa kushinda uchaguzi huo hii leo dhidi ya wagombea 17 wa wadhifa wa urais uliofanyika jana nchini Mauratania, lakini hakuna aliyefikisha asilimia 50 ya kura zinazohitajika kupata ushindi wa moja kwa moja.

Kwa mujibu wa afisa katika wizara ya mambo ya ndani nchini Mauritania ambaye hakutaka jina lake litajwe, Sidi Mohamed Ould Cheikh Abdallahi, mwenye umri wa miaka 68, mwanasiasa maarufu ambaye ameshikilia nyadhifa mbalimbali katika wizara kadhaa nchini humo, anaongoza kwa kiasi kinachozidi asilimia 23 ya kura zote. Kiongozi huyo anafuatiliwa kwa karibu na mwanasiasa mkongwe, Ahmed Ould Daddah, mwenye umri wa miaka 64, akiwa amepata asilimia 21 ya kura. Gavana wa zamani wa benki kuu ya Mauritania, Zeine Ould Zeidane, amepata asilimia 15 ya kura.

Uchaguzi wa jana ulikuwa wa amani hadi watu waliokuwa wamejihami na bunduki walipofyatua risasi na kumuua afisa wa usalama usiku wa kuamkia leo. Msemaji wa tume ya waangalizi ya Umoja wa Ulaya amesema uvamizi wa kituo hicho cha kuhesabia kura umefanywa katika mji ulio karibu na mpaka wa kusini na Senegal.

Wapigaji kura walijitokeza katika vituo vya kupigia kura wakiwa na matumaini makubwa kwamba uchaguzi huo utamaliza miongo ya utawala wa kijeshi nchini Mauritania, ambako hakujakuwa na mabadiliko ya utawala kupitia uchaguzi katika kipindi cha miaka 47. Thuluthi moja wa Wamauritania milioni 3.1 walijiandikisha kupiga kura katika uchaguzi wa jana na imekadiriwa kuwa wapigaji kura zaidi ya asilimia 60 walishiriki katika zoezi zima la upigaji kura.

Waziri wa maswala ya ndani wa Mauritania, Mohamed Ahmed Ould Mohamed Lemine, alisema jana mjini Nouakchott kwamba idadi kubwa ya watu waliojitokeza kupiga kura inadhihirisha kuwa wananchi wamefurahia uchaguzi huo wa kwanza wa rais kwa misingi ya demokrasia. Uchaguzi wa jana unaashiria hatua ya mwisho ya Mauritania kurejea katika utawala wa kiraia.