1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Northrhine-Westphalia una maana uchaguzi mkuu

Mohammed Khelef
15 Mei 2017

Baada ya CD kujipatia ushindi dhidi ya SPD kwenye uchaguzi wa jimbo kubwa la Northrhine-Westphalia, sasa nafasi ya Merkel kurejea madarakani ni kubwa zaidi.

https://p.dw.com/p/2d0Wp
Deutschland CDU zur Landtagswahl in Nordrhein-Westfalen
Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Jana wakaazi wa jimbo la Northrhine-Westphalia walipata fursa ya kuchaguwa bunge jipyahapo jana, uchaguzi ambao ulifuatiliwa nchi nzima kutokana na ukweli kuwa hili ni jimbo lenye watu wengi zaidi nchini Ujerumani na uchaguzi huu ulikuwa kipimo muhimu cha uchaguzi mkuu wa Septemba 24.

Chama cha CDU kinachoongozwa na Kansela Angela Merkel kilijipatia ushindi kwa kujikingia asilimia 33 ya kura dhidi ya chama cha SPD ambacho kilishika nafasi ya pili kwa kuwa na asilimia 31.

Hadi Jumatatu ya leo (15 Mei), CDU imo kwenye furaha kubwa, lakini hali sivyo ilivyo kwa kansela mwenyewe ambaye ameendelea kubakia na hali yake ya tahadhari, akiwambukumbusha wanachama wenzake kuwa kuna uchaguzi mkuu unakuja hapo mwezi Septemba, na bado hawajashinda.

"Duru mpya ya kampeni za uchaguzi mkuu inaanza sasa. Tutafanya tuwezalo kufanikisha kampeni kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa tarehe 24 Septemba kama tulivyofanya kwenye chaguzi za majimbo," alisema Merkel baada ya ushindi huo.

Hapana shaka, uchaguzi wa jana kwenye jimbo la Northrhine-Westphalia ni kichocheo kikubwa kwa kansela huyo na chama chake. CDU ilifanikiwa kuibwaga SDP ambayo imekuwa madarakani kwenye jimbo hili kwa muda wote tangu mwaka 1966, isipokuwa tu muhula mmoja wa miaka mitano.

Siasa za majimbo juu ya siasa za kitaifa

Hata hivyo, mwenyewe Kansela Merkel alikiri kwamba uchaguzi kwenye jimbo hili ulikuwa zaidi juu ya siasa za jimbo, ambazo zinahusu vita dhidi ya ukosefu wa ajira, uhalifu na mfumo mbaya kabisa ya elimu nchini Ujerumani.

TV-"Wahlarena" zur NRW-Landtagswahl  Sylvia Löhrmann Hannelore Kraft und Armin Laschet
Hannelore Kraft wa SPD (kushoto) alimpongeza aliyekuwa mpinzani wake, Armin Laschet wa CDU, mara baada ya kushinda uchaguzi wa Northrhine-Wesphalia.Picha: picture alliance/dpa/O.Berg

"Masuala ya siasa za kitaifa yalikuwa na nafasi yake, lakini masuala ya jimbo yalikuwa juu zaidi kwenye chaguzi hizi. Naweza kusema kuwa nusu na robo yalikuwa masuala ya kijimbo na robo tu ndiyo masuala ya kitaifa. Masuala muhimu ya jimbo yalikuwa ni elimu, usalama na hali ya uchumi," anasema Ulrich von Harlemann, profesa wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Düsseldorf.

Uchaguzi mkuu, kwa upande mwengine, utatawaliwa na masuala mengine kama vile ukosefu wa ajira, afya na ustawi wa jamii, ingawa bado fursa za Merkel kushinda zimeongezeka, kwa sababu uchaguzi huu wa Northrhine-Westphalia umekuwa pigo kubwa kwa hasimu wake - kiongozi wa chama cha SPD, Martin Schulz. 

Rais huyo wa zamani wa Bunge la Ulaya, aliyezaliwa kwenye jimbo hilo na pia kutumia muda mrefu kupiga kampeni kwenye uchaguzi huo, alikuwa amefanikiwa kupata nguvu dhidi ya Kansela Merkel tangu atangaze kugombea wadhifa wa ukansela mwezi Januari.

Lakini umashuhuri wake ulianza kushuka hata kabla ya uchaguzi wa jana, na sasa matokeo ya uchaguzi wenyewe hayakuonesha ikiwa anaweza kukisaidia chama chake kupata umaarufu zaidi.

"Jioni ya jana ilikuwa ngumu kwetu. Uongozi wa chama utakutaka na kuchambua kilichokwenda kombo. Lakini kitu kimoja kipo wazi. Tuna safari ndefu yenye vigingi mbele yetu kufikia uchaguzi wa Septemba 24. Itakuwa ngumu, lakini Social Democrat ni chama kilicho tayari kupambana," alisema mapema leo alipokutana na vyombo vya habari akiwa na uso uliosawijika.

Bado haijawa wazi ikiwa mapambano hayo yatazaa matunda. Lakini ikiwa imesalia miezi minne tu hadi tarehe ya uchaguzi mkuu na kwa kuwa kuwa wapigakura wengi wa Kijerumani hufanya uamuzi wa nani wanayempigia kura hasa ile siku na ule muda wakiwa kwenye vyumba vya kura, wataalamu wengi wanasema bado pangali na nafasi ya mambo kubadilika.

Lakini kwa sasa, haionekani kuwa ni hivyo!

Mwandishi: Daniel Pelz/Mohammed Khelef
Mhariri: Iddi Ssessanga