1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa rais wacheleweshwa Nigeria,

8 Februari 2015

Nigeria imeahirisha uchaguzi wa Rais kutokana na sababu za kiusalama wakati mzozo wa Boko Haram unaongezeka, ukitoa fursa kwa chama tawala wakati kikikabiliwa na changamoto kali kutoka kwa upinzani.

https://p.dw.com/p/1EXqZ

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amesema nchi yake imevunjwa moyo na uamuzi wa Nigeria wa kuuahirisha uchaguzi wa Rais.Lakini Waziri Kerry ametoa mwito wa kudumisha utulivu nchini Nigeria.

Ucheleweshaji wa wiki sita umetangazwa baada ya wakuu wa usalama kusema jeshi linahitaji muda zaidi kuweka hali ya usalama katika maeneo yaliyoko chini ya udhibiti wa kundi la magaidi wa Boko Haram, la Waislamu wenye itikadi kali ambao wanadhibiti maeneo kadhaa kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Wahlkampf in Nigeria 2015 Goodluck Jonathan
Msafara wa kampeni ya rais Goodluck JonathanPicha: picture-alliance/AP Photo/S. Alamba

Uchaguzi wa Rais na bunge sasa utafanyika Februari 28 badala ya Februari 14 kama ilivyopangwa hapo awali, amesema Attahiru Jega, mwenyekiti wa tume huru ya taifa ya uchaguzi (INEC).Uchaguzi wa magavana na wabunge kwenye majimbo utafanyika Aprili 11, ameongeza kusema.

Washauri wa usalama

Jega amesema wakuu wa usalama wameshauri kwamba uchaguzi uahirishwe kwa wiki sita wakati operesheni za jeshi katika maeneo ya kaskazini mashariki zimesababisha upungufu wa wanajeshi ambao watalinda usalama wakati wa uchaguzi.

Wahlkampf in Nigeria 2015
Mwanamke akipita katika mabango ya kampeni ya uchaguzi NigeriaPicha: Reuters/A. Sotunde

"Iwapo usalama wa wafanyakazi, wapigakura, wachunguzi wa uchaguzi na vifaa vya uchaguzi hauwezi kuhakikishwa, maisha ya vijana wasio na hatia pamoja na wanawake yatakuwa hatarini na uwezekano wa uchaguzi huru na wa haki na wa kuaminika hautakuwapo," amewaambia waandishi habari.

Rais Goodluck Jonathan anakabiliwa na uchaguzi mgumu kwa sababu mgombea mkuu wa upinzani ni kiongozi wa zamani wa kijeshi Muhammadu Buhari.

Lakini kwa kuwa kampeni sasa zimerefushwa, mchambuzi wa masuala ya kisiasa Dawn Dimolo wa shirika la ushauri la Africa practice amesema chama cha Jonathan cha People's Democratic Party (PDP) kinaweza kufaidika.

Wahlkampf in Nigeria 2015 Muhammadu Buhari
Muhammadu Buhari mgombea wa upinzaniPicha: AFP/Getty Images/P. Utomi Ekpei

Chama cha PDP, ambacho hakijaondoka madarakani tangu Nigeria irejee katika utawala wa kiraia mwaka 1999, kinafaidika na kuwa na Rais aliyeko madarakani pamoja na upatikanaji wa fedha nyingi kuliko chama cha Buhari cha All Progresives Congress (APC).

Ucheleweshaji wa kupiga kura utakiwezesha chama cha PDP kuvutia kura zinazotarajiwa lakini kunaweza pia kuimarisha chama cha APC, ambacho mara kadhaa kimeishutumu serikali kwa kujaribu kuvuruga uchaguzi huo, amesema Dimolo.

Wanigeria watakiwa kuwa watulivu

Mwenyekiti wa taifa wa chama cha APC John Odigie-Oyegun ameuita uchelewesho huo "hatua kubwa ya kurejesha nyuma demokrasia nchini Nigeria" na "ya uchokozi mno".

Wahlkampf in Nigeria 2015 Goodluck Jonathan
Mkutano wa kampeni ya rais Goodluck JonathanPicha: AFP/Getty Images/P. Utomi Ekpei

Lakini ameongeza: "Natoa wito kwa nguvu zote kwa Wanigeria wote kuwa watulivu na kujiepusha kufanya ghasia na kitendo chochote ambacho kitaongeza hali hii iliyojitokeza ambayo haikutarajiwa."

Vikosi vya jeshi la Nigeria, vikiungwa mkono na wanajeshi kutoka Chad, Cameroon na Niger, hivi karibuni vimeanza operesheni ya pamoja ya kupambana na kundi la Boko Haram wakati mzozo huo ukipanuka na kuvuka mipaka ya Nigeria.

Anschlag in Gombe, NIgeria 02.02.2015
Shambulio lililofanywa na wapiganaji wa Boko Haram katika mji wa GombePicha: Reuters/Afolabi Sotunde

Tangu mwaka huu kuanza, kundi hilo la Boko Haram limeongeza mashambulizi yake, kwa sehemu ikiendeleza ukandamizaji wa hatua za demokrasia, ambazo inaziona kuwa ni kinyume na Uislamu.

Jega hapo kabla amekiri kuwa uchaguzi hautafanyika katika maeneo ambayo yako chini ya udhibiti wa kundi hilo la Kiislamu, na kuzusha maswali juu ya iwapo wale waliokimbia mapigano wataweza kupiga kura.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Caro Robi