1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Rais Zimbabwe

Daniel Pelz (DW Afrika)4 Machi 2008

Mgawanyiko miongoni mwa vigogo waanza kujitokeza wazi.

https://p.dw.com/p/DHvi
Rais Robert Mugabe.Picha: AP

Wakongwe wawili wa vita vya ukombozi wa Zimbabwe wamejitokeza kumuunga mkono Waziri wa fedha wa zamani Simba Makoni mwenye umri wa miaka 57, ambaye alitangaza kuwa atasimama akiwa mgombea huru dhidi ya Rais Robert Mugabe, kiongozi aliyeitawala nchi hiyo tangu uhuru 1980, sasa akiwa na umri wa miaka 84.

Makoni aliyefukuzwa chama kwa sababu ya uamuzi huo, anaungwa mkono na wakongwe wa vita vya ukombozi, Edgar Tekere aliyewahi kuwa katibu mkuu wa chama tawala ZANU-PF na ambaye alifukuzwa pia chama mwaka jana. Tekere alitokeza pamoja na Bw Makoni katika kampeni moja wapo mjini Harare.

Mwengine ni waziri wa zamani wa mambo ya ndani Dumiso Dabengwa na ni mwanasiasa wa kwanza wa ngazi ya juu wa ZANU PF kujiunga na upande wa Makoni.

Hata hivyo zile fununu kwamba makamu wa rais Joyce Mujuru angetangaza kumuunga mkono Makoni, zilifikia kikomo chake baada ya Bibi Mujuru kuamaua kumuunga mkono Rais Mugabe. Awali kulia na uvumi kwamaba Makoni akiungwa mkono sio tu na Makamu huyo wa rais bali pia na mumewe Solomon Mujuru, mkuu wa zamani wa majeshi .

Kwa upande mwengine Bw Makoni amepata uungaji mkono wa vyama viwili vya kisiasa vya upinazani ZANU-Ndonga na Movement for Democratic Change-MDC, kundi lililojitenaga na MDC ya Bw Morgan Tsvangirai ambaye hadi asasa akionekana kuwa ndiye mpinzani mkubwa wa rais Mugabe.

Tsvangirai alishindwa na Mugabe katika uchaguzi 2002 ambao ulitajwa kna waangalizi wa ndani na nje kuwa wa udanganyifu na kuingiza Zimbabwe katika mgogoro wa kisiasa. Tsvangirai pia ni mgombea katika uchaguzi huu ujao. Kundi lake la MDC lina ungwa mkono zaidi maeneo ya mijini.

ZANU-Ndonga ina ngome yake kuu katika wilaya ya Chipinge wakati MDC kundi lililojitenga lina uungaji mkono zaidi katika eneo la kusini la Matabeleland ,mkoa ambao mji wake mkuu ni Bulawayo.

Akifungua kampeni yake, Makoni amekosoa vikali uendeshaji mbaya wa mashirika ya serikali na akaahidi kuwashughulikia wale waliojirundikizia amashamba chini ya mpango wa marekebisho wa rais Mugabe ambao umeiingiza Zimbabwe katika hali mbaya ya Kiuchumi. Hata hivyo MDC ya Bw Tsvangirai inasema Makoni pia anabeba jukumu la hali mbaya ya uchumi kwani alikua waziri wa fedha hapo kabla katika utawala huo huo wa Mugabe.

Kwa upande wake Rais Mugabe anatumai kupata ridhaa ya wananchi aweze kutawala kwa mhula wa sita kama anavyosema mwenyewe, licha ya kwamba hali ngumu imesababisha sasa ughali wa maisha kufikia kiwango cha asili mia 100, kikiwa kikubwa kabisa duniani.

Baadhi ya Wazimbabwe wanasema hawajui kiatakachotokea ikiwa Mugabe atafanya udanganyifu katika uchaguzi huo na wakiitazama hali yao wanasema ni mbaya hata kuliko Kenya baada ya machafuko ya karibuni yaliotokana na uchaguzi.

Pamoja na hayo Chris Maroleng, mtaalamu katika taasisi ya usalama nchini Afrika kusini anasema upinzani nchini Kenya umetoa changa moto kwa vyama tawala, akisisitiza kuwa "Ni wazi kwamba mfano wa Kenya na upinzani nchini Kenya kwa vyama vya upinzani vya Afrika huenda ukawa ni mzigo mzito kwa chama tawala ZANU-PF nchini Zimbabwe. Nafikiri wanataka kuwavunja moyo wanachama wa jumuiya za kiraia au maafisa wa upinzani wanaozingatia kukabiliana na ZANU.-PF mabarabarani."

Kwa wakati huu hatima ya Wazimbabwe imo mikononi mwao katika uchaguzi wa tarehe 29 mwezi huu. Kwa sasa nchi hiyo inaendelea kukumbwa na uhaba mkubwa wa umeme na baadhi ya maeneo yakikosa umeme kwa muda wa hadi masaa 10, mbali na uhaba wa chakula na mahitaji mengine muhimu.

Mugabe bado anashikilia ana kila sababu ya kuendelea kuwaongoza wazimbabwe na amewataja wapinzani wake Morgan Tsvangirai kuwa kibaraka wa nchi za magharibi na Simba Makoni kahaba wa kisiasa.