1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa serikali za mitaa nchini Misri

Miraji Othman7 Aprili 2008

Chama cha Vuguvugu la Kiislamu nchini Misri jana kilisema kwamba kitaususia uchaguzi wa leo wa serekali za mitaa.

https://p.dw.com/p/DdgL
Rais Husni Mubarak wa MisriPicha: AP

Makamo wa kiongozi mkuu wa chama hicho, Mohammed Habib, aliliambia Shirika la Habari la Ufaransa, AFP, kwamba wametoa mwito kwa watu wa Misri waususie uchaguzi huo wa serekali za mitaa kwa vile serekali ya nchi hiyo haijali juu ya haki. Chama cha Muslim Brotherhood kimepangiwa kisimamishe watetezi 20 tu baada ya serekali kuchukuwa hatua kadhaa za kukibana chama hicho na kuwabakisha wanachama wengi wa chama hicho waliotaka kupigania uchaguzi huo ndani ya magereza au kuwazuwia wasijiandishe kama watetezi.

Kinyume na hayo, chama tawala cha National Democratic cha Rais Husni Mubarak kinasimamisha mtetezi katika kila moja wapo ya viti 52,000 vya serekali za mitaa vinavowaniwa.

Asilimia 90 ya watetezi hao hawajapingwa.

Chaguzi za manispaa nadra zilivutia ushindani mkali hapo kabla, lakini uchaguzi wa mwaka huu utakuwa wa kwanza tangu kufanyika marekebisho ya katiba hapo mwaka 2005, na ambayo yalitaka watetezi wa kujitegemea kwa ajili ya uchaguzi wa urais wa nchi waungwe mkono na madiwani wa mabaraza ya manispaa. Watetezi wa urais wanahitajika waungwe mkono na si chini ya madiwani kumi kutoka kila baraza la mji katika si chini ya mikoa 14.

Habari za magazeti zinasema ni wanachama mia saba tu kati ya 1,700 wa chama cha upinzani cha Wafd walioweza kujiandikisha pamoja na wanachama 400 wa chama cha mrengo wa kushoto cha Tagammu, kukiweko malalamiko miongoni mwa wapinzani waliotaka kupigania katika uchaguzi kwamba kulikuweko vikwazo vya urasimu na pia walipigwa walipofika katika vituo vya kujiandikisha.

Kabla ya kufanyika uchaguzi wa leo kumekuweko na ukandamizaji mkubwa dhidi ya wanachama wa Muslim Brotherhood, wanachama zaidi ya 800 wa kikundi hicho walikamatwa katika wiki za karibuni.

Kikundi hicho nkimesema kwamba serekali ya Rais Husni Mubarak ina hamu ya kujiepusha na kushindwa tena katika uchaguzi mara hii, baada ya chama hicho cha Udugu wa Kiislamu kupata asilimia 20 ya viti katika uchaguzi uliopita wa bunge ambapo wanachama wake huketi bungeni kama wajumbe wanaojitegemea, kwa vile ni marufuku wao kujitambulisha na kundi hilo la Muslim Brotherhood.

Kwa mujibu wa kiongozi wa cheo cha juu wa chama hicho, Essam al-Erian, orodha ya watetezi wa chama hicho imepunguzwa kutoka 5,754 na kubakia 498, hivyo kulazimika kufikisha mashtaka 3,192 kutaka watetezi wao waliokatazwa waachiliwe washiriki kupigania uchaguzi huo.

Hata hivyo, serekali imekataa kuheshimu hukumu za korti. Bwana al-Erian alisema ni wazi kwamba chama tawala cha National Democratic hakitakabiliana na ushindani wowowte wa kweli katika uchaguzi huu. Jumuiya za kimataifa zimeilaani hatua ya serekali ya Misri kuwaandama watetezi wa upinzani.