1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Sudan waongezwa muda

Kabogo Grace Patricia13 Aprili 2010

Hatua hiyo imetangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Sudan-NEC.

https://p.dw.com/p/Mv3c
Rais wa Sudan, Omar al-Bashir akipiga kura katika uchaguzi wa vyama vingi nchini humo.Picha: AP

Uchaguzi mkuu wa Sudan ulioengezwa muda wa siku mbili leo umeingia siku yake ya tatu. Uchaguzi huo ambao ni wa kwanza kufanyika katika kipindi cha miaka 24 , ulianza Jumapili ukigubikwa na matatizo kadhaa.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Sudan-NEC, jana ilitangaza kuwa uchaguzi huo umeongezwa muda, baada ya chama kikuu cha Sudan Kusini cha Sudan People's Liberation Movement-SPLM, kutaka uchaguzi huo uongezwe muda wa siku nne. Katibu Mkuu wa chama cha SPLM, Pagan Amum, ameliambia shirika la habari la Ujerumani-DPA kuwa uchaguzi huo ulitawaliwa na matatizo ya uandikishaji wapiga kura likiwemo suala la baadhi ya majina ya wapiga kura wa Sudan Kusini kutokuwa katika orodha ya wapiga kura.

Kiasi ya wapiga kura milioni 16.5 walijiandikisha kupiga kura katika uchaguzi huo na imeelezwa kuwa matatizo hayo yamejitokeza kutokana na ukubwa wa nchi hiyo na miundombinu mibovu ya taifa hilo kubwa barani Afrika. Uchaguzi huo wa rais, wabunge na viongozi wa serikali za mitaa ambao unatarajiwa kufungua ukurasa mpya wa demokrasia nchini Sudan umesusiwa pia na vyama vikuu vya upinzani, ambavyo vimesema vinaamini kuwa uchaguzi huo utatawaliwa na udanganyifu kwa ajili ya kukipendelea zaidi chama tawala cha National Congress-NCP.

Sudan Wahlen Kandidat Salva Kiir
Kiongozi wa Sudan Kusini, Salva Kiir, akisubiri kupiga kura katika uchaguzi huo wa vyama vingi, katika kituo cha kupigia kura huko Juba.Picha: AP

Wiki iliyopita Umoja wa Ulaya uliwaondoa waangalizi wake wa uchaguzi, katika jimbo la Darfur kutokana na sababu za usalama. Waangalizi wengi wamesema kuwa uchaguzi katika jimbo hilo utagubikwa na hila kwa lengo la kumpendelea Rais aliyeko madarakani, Omar Hassan al-Bashir. Mwishoni mwa wiki iliyopita, Rais wa zamani wa Marekani Jimmy Carter, ambaye taasisi yake ni mwangalizi wa uchaguzi huo alisema kuwa ana matumaini uchaguzi huo wa kihistoria nchini Sudan utafikia viwango vya kimataifa.

Ni wazi kuwa Rais al-Bashir atashinda katika uchaguzi huo baada ya vyama hivyo vya upinzani vya Umma na SPLM, kujitoa katika kinyang'anyiro hicho. Kiongozi wa eneo la Sudan Kusini lenye utawala wa ndani Salva Kiir, anatarajiwa kushinda katika uchaguzi huo kwenye eneo hilo la kusini. Sudan bado imo katika hatua ya kuondokana na athari za vita vya muda mrefu vya wenyewe kwa wenyewe kati ya kaskazini na eneo la kusini mwa nchi hiyo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (DPAE/AFPE)

Mpitiaji: Mohammed Abdul-Rahman