1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Uingereza waleta msisimko

Sekione Kitojo7 Mei 2010

Waingereza wamelichagua bunge jipya katika uchaguzi uliofanyika hapo jana Mei 6, na kwa mara ya kwanza baada ya miongo kadha hakuna chama kilichopata wingi wa kutosha.

https://p.dw.com/p/NH1s

Waingereza wamelichagua bunge jipya katika uchaguzi uliofanyika hapo jana Mei 6. Baada ya matokeo ya mwanzo kutangazwa , kwa mara ya kwanza baada ya miongo kadha hakuna chama ambacho kimepata wingi wa kutosha. Hata hivyo chama cha kihafidhina, Conservative, chini ya uongozi wa David Cameron kimekiondoa chama cha Labour kuwa chama chenye nguvu nchini Uingereza. Lakini hii haingewezekana bila ya usaidizi wa vyama vingine.

Matokeo ya uchaguzi huo hayakushangaza. Tangu wiki kadha ilitabiriwa kuwa katika bunge la Uingereza mara hii hakuna chama kitakachopata ushindi wa moja kwa moja. Uchaguzi wa mwaka huu ulitabiriwa kuwa wa kusisimua katika muda wa miongo kadha kupita. Wengi wanajiuliza, kwanini muonekano wa kuwa hakuna mshindi wa moja kwa moja , unaonekana kuvutia zaidi. Haifahamiki iwapo suala la mzozo wa kiuchumi duniani linahusika katika uchaguzi huu. Lakini inaweza kuwa kitu kingine, ambacho kimesababisha uchaguzi huu kuwa wa vuta ni kuvute zaidi kwa Waingereza. Huenda ni katika kujaribu kuonyesha kuwa hawataki tena mfumo unaotawaliwa na vyama viwili.

Baada ya miaka 13 ya uongozi wa chama cha Labour, wapiga kura waliokuwa wakikipigia chama cha waziri mkuu Gordon Brown sasa wamechoshwa. Waziri mkuu huyo ambaye hapendezi tena , ambaye amechukua madaraka ya kiti hicho kutoka kwa mtangulizi wake Tony Blair, bila ya kushinda kupitia uchaguzi, hakuweza kutoa ushawishi wa kutosha wakati wa kampeni.

Lakini hata kiongozi wa chama cha Conservative David Cameron , ambaye ni kipenzi cha Waingereza, hakuweza kufaidika na hali hiyo ya kuaminika na wengi wa wapigakura wa Uingereza. Pia ikilinganishwa na uchaguzi wa mwaka 2005 chama hicho kimefanya vizuri na kukiondoa chama cha Labour kuwa chama chenye nguvu, lakini bado kimeshindwa kupata wingi wa kutosha bungeni kuweza kutawala peke yake.

Katika nafasi ya tatu yuko Nick Clegg, kiongozi wa chama cha Kiliberali, ambaye ameingiza hali mpya katika uchaguzi wa mwaka huu. Amepata kuungwa mkono sana pamoja na chama chake tangu baada ya mjadala uliofanyika katika televisheni na kutangazwa kwa maoni ya wapiga kura kuhusu mjadala huo, na kubadili mwelekeo, na tangu wakati huo amesababisha utabiri kuhusu mabadiliko ya mfumo wa siasa za Uingereza.

Kwanza kabisa kujitokeza tu katika televisheni nchini Uingereza hakutoshi kupata ushindi katika uchaguzi. Lakini sababu ya msingi ambayo wengi wa wapiga kura wa chama cha Kiliberali wangependa kupiga kura, lakini hawakufanya hivyo, inatokana na mfumo wa Uingereza wa chama kupata wingi wa kutosha kuweza kutawala. Bila ya mgombea kupata asilimia fulani inayokubalika kisheria, kura uliompigia inakuwa imepotea bure. Kwa hiyo wapiga kura ambao wamempigia kura mgombea ambaye ameshindwa hata kama ni idadi ya juu lakini inakuwa kazi bure. Kwa hiyo utaratibu huu chama cha Kiliberali kinataka ubadilishwe. Lakini kabla ya kufanya hivyo inabidi kushinda majimbo mengi dhidi ya wale wanaotetea utaratibu wa sasa.

Mwandishi : Irene Quaile / ZR / Sekione Kitojo.

Mhariri: