1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Ujerumani jumapili hii:

22 Septemba 2009

Ni vyama gani vitaunda serikali ?

https://p.dw.com/p/JmDs
Bibi Angela Merkel na mpinzani wake Steinmeier.Picha: AP

Siku chache kabla ya uchaguzi mkuu wa Bunge la Ujerumani, Jumapili hii, Septemba 27, uvumi unazidi kuzagaa kuhusu serikali gani ya muungano wa vyama itaibuka. Vyama mbali mbali vya kisiasa vinavyogombea uchaguzi huu, vimebainisha utayarifu wao wa kuunda serikali hiyo ya mseto na chama kimojawapo au vyama .

Kwa muujibu wa uchunguzi wa maoni, serikali ya muungano inayopata uzito na ambayo yaweza kujipatia viti vingi vya kutawala na ingeridhisha matakwa ya wengi wanaogombea uchaguzi huu ni ile: kati ya muungano wa vyama vya kihafidhina vya CDU/CSU na Free Democratic Party (FDP)-chama cha kiliberali.

Ikitokea mfumo huu hautawezekana , Ujerumani itakabiliwa na msukosuko wa kuunda serikali.Hapo tena yamkini serikali ya sasa ya muungano wa vyama vikuu kati ya CDU/CSU -vinavyoongozwa na Kanzela Angela Merkel na chama cha kijamaa cha Socila Democratic Party (SPD) kikiongozwa na waziri wa nje Bw.Frank- Walter Steinmeier, ni ufumbuzi pekee:

Chama gani kingependa kuunda serikali na chama au vyama gani, wapigakura wa Ujerumani wanajua kitambo.Lakini kutokana na mwanya uliopo kati ya kambi ya vyama vya kihafidhina (CDU/CSU) na waliberali FDP upande mmmoja ; na kambi ya mrengo wa shoto ya SPD,chama cha LINKE na cha walinzi wa mazingira KIJANI kwa upande wapili unazidi kuwa mdogo, upande wowote ule hautaweza kuunda serikali isio-rega-rega.Tayari chama cha kijamaa cha SPD kimeshabainisha tofauti wazi katika sera za nje na za usalasma kwenye serikali ya muungano na chama cha LINKE-cha mrengo wa shoto zaidi.Jambo hilo alilisitiza Kiongozi wa SPD Bw. Franz Munterfering,wiki tu kabla ya uchaguzi wa jumapili hii.

"Kwa maoni yetu ,vyama vyote vyengine vya kidemokrasia, kimsingi ,vinaweza kuunda serikali ya muungano.Yule anaejitenga na muungano wa aina hiyo,huyo anabidi kutambua nini anaitakia nchi hii."

Katika daraja ya kimkoa,chama cha SPD tayari kimeunda serikali ya muungano na chama cha mrengo wa shoto zaidi cha LINKE na hii tena tangu 2002 katika jiji kuu la Berlin.

Serikali ya mfumo wa vyama vitatu ya muungano kati ya vyama hivyo 2 na kile cha walinzi wa mazingira -KIJANI- inapangwa kuundwa katika mikoa ya Saarland na Thüringen ambako kufuatia matokeo ya chaguzi za mikoa huko mwishoni mwa mwezi uliopita wa August, majadiliano yanafanyika.

Kuhusu uwezeklano wa serikali inayoitwa ya vyama vinavyopepea bendera nyekundu kwa nyekundu-Rot-Rot pamoja na walinzi wa mazingira-KIJANI, ndio upatu anaoupiga meneja wa chama cha mrengo wa shoto cha LINKE,Dietmar Bartsch.Anasema kwamba, wanataka hivi sasa vyama hivyo vitatu vianze kujadiliana sera zao na kuunda serikali ya muungano itakayoongoza mabadiliko ya siasa huko Thüringen na mwishoe, isalie kuamua nani anashika wadhifa gani .

Mada ya nani anakamata wadhifa gani ni nyeti kwa chama cha SPD ,kwavile hakiko tayari kumuona mjumbe wa chama cha mrengo wa shoto zaidi-DIE LINKE, anaongoza serikali ingawa kinaongoza kwa viti kuliko SPD.

Shabaha sawa na hiyo anaifuata mwenyekiti wa chama cha kiliberali cha FDP , Guido Westerwelle.Katika kikao maalumu cha chama chake ,mwishoni mwa wiki alibainisha wazi na bila ya kupingwa lengo la kampeni yake: Kuunda serikali na wahafidhina-CDU-CSU tu.FDP chini ya usukani wake, haitaridhia kabisa kujiunga na serikali ya rangi za taa za majiani: Nyekundu-Manjano na kijani.