1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wafanyika Ivory Coast

1 Novemba 2010

Wananchi wa Ivory Coast jana wamepiga kura katika hali ya amani wakati wa uchaguzi wa urais wenye lengo la kuliunganisha tena taifa hilo liliyogawanyika sehemu mbili kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe

https://p.dw.com/p/PvKV
Rais wa Ivory Coast Laurent GbagboPicha: AP

Uchaguzi huo ambao ni muhimu katika taifa hilo linaloongoza kwa kulima zao la kakao duniani, unafanyika baada ya kuahirishwa mara sita kutokana na mvutano wa kisiasa uliosababishwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya mwaka 2002 na 2003. Wapinzani wakuu wa rais aliyeko madarakani, Laurent Gbagbo ni Henri Konan Bedie, ambaye ni rais wa zamani wa nchi hiyo aliyeondolewa madarakani katika mapinduzi ya mwaka 1999 na Alessane Outtara, waziri mkuu wa zamani na afisa wa Shirika la Fedha la kimataifa-IMF.

Wachambuzi wengi wanaoufatilia uchaguzi huo wanasema kuwa Rais Gbagbo anapewa nafasi kubwa ya kushinda katika uchaguzi huo. Akizungumza baada ya kupiga kura, Rais Gbagbo alisema ana furaha kuwa uchaguzi umefanyika kama ilivyopangwa. Wakati baadhi ya vituo vya kupigia kura vilifungwa majira ya saa 11 za jioni kama ilivyopangwa, tume ya uchaguzi ilisema kuwa vituo vingi vilichelewa kufunguliwa kwa saa mbili au zaidi kutokana na matatizo ya kukosekana kwa vifaa vya kupigia kura. Hatua hiyo ilisababisha kuongezwa muda wa kuvifunga ili kuhakikisha muda wa masaa 10 uliotengwa kwa vituo vya kupigia kura kuwa wazi unatimia.

Akizungumza na shirika la habari la Reuters, katika eneo la kaskazini linaloshikiliwa na waasi la Bouake, msemaji wa tume ya uchaguzi ya Ivory Coast, Bamba Yacouba alisema kuwa idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura nchi nzima inakadiriwa kuwa kati ya asilimia 60 na 70. Maafisa wa uchaguzi wameiambia Reuters kuwa watu waliojitokeza kupiga kura katika mji mkuu, Abidjan ni asilimia 75 au zaidi. Mwangalizi mkuu katika uchaguzi huo kutoka ubalozi wa Japan, Ono Tomoyuki amesema watu waliojitokeza kupiga kura Bouake, mji wa pili kwa ukubwa ni karibu asilimia 80.

Matokeo ya awali yanatarajiwa kutangazwa katika kipindi cha siku tatu zijazo, ingawa huenda matokeo hayo yakatangazwa ifikapo leo mchana, huku kukiwa na hofu ya wagombea kujitangaza wenyewe kuwa waashindi. Kulingana na ufuasi wa wagombea hao kwa kuzingatia maeneo na makabila, huenda ushindi wa moja kwa moja usipatikane katika awamu ya kwanza ya uchaguzi huo, na hivyo kuwa na maana kwamba awamu ya pili ya upigaji kura huenda ikafanyika tarehe 28 ya mwezi huu wa Novemba.

Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa chenye wanajeshi 9,500 kikisaidiwa na mamia ya wanajeshi wa Ufaransa tayari kimejiandaa iwapo kutatokea vurugu zozote zile. Hata hivyo, Kamanda wa kikosi hicho, Meja Jenerali Abdul Hafiz amesema watu wamejitokeza kwa wingi kupiga kura na kulikuwa na hali ya amani na utulivu katika vituo vya kupigia kura mjini Abidjan.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE)

Mhariri:Josephat Charo