1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchambuzi wa Magazeti ya Ujerumani

P.Martin4 Juni 2007

Nchini Ujerumani mada iliyogonga vichwa vya habari magazetini ni zile ghasia zilizozuka mjini Rostock kando ya maandamano ya wanaharakati wanaopinga utandawazi.

https://p.dw.com/p/CHSo

Tukianza na gazeti la huko huko Rostock kulikozuka ghasia hizo,OSTSEE-ZEITUNG linasema:

“Mamia ya raia na polisi waliojeruhiwa;watu wanaokimbia;vizuizi na magari yaliyotiwa moto; hayo ni mambo yaliyoshuhudiwa hata kabla ya kufunguliwa mkutano wa kilele wa nchi nane tajiri zilizoendelea kiviwanda G-8.Ni dhahiri kuwa tunahofia hizo siku zinazokuja.Mji wa Rostock, ndio umepigwa na bumbuazi."

BERLINER ZEITUNG nalo likiendelea na mada hiyo hiyo,linasema:

“Yaliyotokea mjini Rostock si pigo kwa polisi tu bali hata utaratibu wa amani wa baadhi kubwa ya wapinzani wa utandawazi,sasa umegubikwa na ghasia za siku ya Jumamosi.Kinachogombewa na wapinzani wa utandawazi ni halali,lakini nani anaezungumzia ukweli huo,baada ya fujo za Rostock?” lauliza Berliner Zeitung.

Kwa upande mwingine ALLGEMEINE ZEITUNG linalochapishwa Mainz linasema:

“Wale waliofanya ghasia kwa makusudi mjini Rostock,si waandamanaji bali ni wahalifu,kwa kweli ni magaidi.Kwa maoni ya Allgemeine Zeitung,wanaosikitisha hasa ni polisi wanaopaswa kubakia shuari licha ya hatari zinazowakabili na hujikuta wakikosolewa kwa kila kinachokwenda mrama." Likiendelea linasema:

“Kinachohitajiwa ni kufikiriwa upya hatua za kisheria zinazopaswa kuchukuliwa dhidi ya wafanyaghasia:Ikiwa katika siku zijazo,watu wa aina hiyo watapewa adhabu ya kifungo cha kama miaka minane hadi kumi,pindi ghasia zao zitamjeruhi mtu vibaya sana,basi baadhi yao huenda wakajitenga kabisa na ghasia za aina hiyo.”

Hata wapinzani wa utandawazi wanaotetea amani wanakosolewa kidogo na gazeti la MÜNCHENER MERKUR.Kwa maoni ya gazeti hilo,

”Wanaharakati hao bora wafikirie hatua za kuchukuliwa kufuatia ghasia zilizotokea Rostock,kwani wamechelewa mno kujitenganisha na wafanya ghasia.Mwito wao wa kutaka kuondosha njaa barani Afrika ni kitendo kinachostahili kuheshimiwa, lakini kutumaini kuwa ghasia hazitotokea ni upuzi sawa na kudhani kwamba kuzuia mkutano wa kilele wa G-8,kutasuluhisha tatizo la umasikini.Sasa maandamano yote ndio yametiwa doa.”

Tunamalizia kwa kukumbuka mashindano ya Kombe la Dunia la Kandanda.Gazeti la BRAUNSCHWEIGER ZEITUNG linatukumbusha hivi:

“Ni takriban mwaka mmoja uliopita,yalipoanza mashindano ya Kombe la Dunia nchini Ujerumani. Ulimwengu mzima ulikaribishwa kwa bashasha na furaha.Sasa,Ujerumani inatazamwa tena na dunia nzima.Lakini safari hii wanachoona ni waya mrefu wa senyenge.Ulimwengu unaona mabomba ya maji, ngumi,marungu na mawe yakirushwa.Kundi dogo la watu waliojaa hisia za chuki na kusababisha fujo, wamejitokeza mbele na kugubika maelfu ya watu walioandamana kwa amani.” lasikitika Braunschweiger Zeitung.