1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani

P.Martin5 Machi 2007

Miongoni mwa mada kuu zitakazojadiliwa katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya juma lijalo, ni sera ya umoja huo kuhusu ulinzi wa mazingira.

https://p.dw.com/p/CHTa

Na wahariri wa magazeti ya Ujerumani pia wamejishughulisha na suala hilo.

Tunaanza na gazeti la NÜRNBERGER ZEITUNG linalosema:

„Kamishna wa viwanda wa Umoja wa Ulaya,bwana Günter Verheugen anatetea viwanda vya magari vya Ulaya,hasa vile vya Ujerumani.Viwanda hivyo vina haki ya kuwa na fahari ya kutengeneza magari yalio bora kabisa duniani.Msimamo huo haumpatii sifa katika makao ya mjini Brussels,lakini jinsi anavyotetea viwanda hivyo,mtu angependa kuona bidii ya aina hiyo miongoni mwa wanasiasa wa mjini Berlin.Badala yake viongozi hao wanajitosa katika wimbi jipya la kulaani magari,kuwa yanachafua mazingira.“

Mada hiyo ya mazingira imeshughulikiwa pia na gazeti la LANDESZEITUNG linalosema:

„Hakuna siku inayopita bila ya wanasiasa kukumbusha hatari ya kutokea maafa ya mazingira. Hushauri iwepo sheria itakayoweka kiwango cha mwendo wa magari;wakati wa livu utumiwe humu nchini badala ya kusafiri nchi za ngambo.Lakini mapendekezo hayo hasa huwalenga wanunuzi.Maafa ya mazingira ni mtihani mkubwa kwa wanasiasa:Wajumbe halisi wa umma,husimama kidete mbele ya mashirika makuu yenye usemi.“

Kwa upande mwingine,KÖLNISHE RUNDSCHAU linashauri iwepo midahalo badala ya kuwa na sheria kali.Kwa maoni yake,binadamu wanazidi kuelewa kuwa mageuzi ya hali ya hewa duniani,huathiriwa na vile kila mmoja wetu anavyoishi.Binadamu wameshatambua ukweli wa mambo,kwa hivyo hakuna haja ya kutumia mabavu au sivyo ujumbe huo utapingwa.Mtu binafsi anaweza kuchukua hatua za kusaidia mazingira.Kwa mfano,anaekwenda kazini kwa treni badala ya kutumia gari na huipasha moto nyumba yake kwa njia ya busara,basi anaweza pia kwenda mapumzikoni nchi za ngámbo kwa njia ya ndeg,bila ya kuwa na hisia mbaya.Sheria zinazolenga tu hisia,hukera.“

Sasa tutazame mada nyingine iliogonga vichwa vya habari katika magazeti ya leo nchini Ujerumani.

Pendekezo la waziri wa familia wa Ujerumani, Ursula von der Leyen,kuongeza idadi ya nafasi za kuwatazama watoto wadogo linaendelea kuzusha mabishano makali katika serikali ya mseto nchini humu.

Kwa maoni ya gazeti la LAUSITZER RUNDSCHAU,juhudi ya waziri wa familia imekitia wasiwasi mkubwa chama cha Social Demokratik SPD,hadi kumfanya kiongozi kama Franz Müntefering kusahau maadili yake kuhusika na serikali ya mseto na kumshambulia mshirika wa muungano mkubwa-mtu atadhani kuwa yupo upande wa upinzani.Suala linaloulizwa pesa za kugharimia nafasi mpya zipatazo 500,000 katika vituo vya kuwatazama watoto wadogo,zitatoka wapi?

Kwa maoni ya waziri mkuu wa jimbo la Bayer,bwana Edmund Stoiber serikali ya Shirikisho ndio izisaidie serikali za majimbo hadi mwaka 2010 kwa kuzipatia asilimia 0.5 ya pato la kodi ya ongezeko la bidhaa lamalizia STUTTGARTER ZEITUNG.