1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani

P.Martin12 Desemba 2006

Uamuzi uliopitishwa na mahakama kuongeza pensheni ya rais wa zamani wa Benki Kuu ya Ujerumani,Ernst Welteke:na kifo cha dikteta wa zamani wa Chile Augusto Pinochet,ni mada kuu mbili za magazeti ya Ujerumani leo hii.

https://p.dw.com/p/CHUE

Basi kwanza tunaanza na Ernst Welteke ambae miaka miwili na nusu ya nyuma alilazimika kuondoka madarakani kama rais wa Benki Kuu ya Ujerumani baada ya kukiri kuwa Dresdner Bank ilimlilipia gharama za kukaa katika hoteli ya anasa ya Adlon mjini Berlin pamoja na familia yake.Gazeti la STUTTGARTER NACHRICHTEN likiandika juu ya Weltke aliekwenda mahakamani kudai nyongeza ya pensheni yake linasema:

“Kwa mara nyingine tena suala la pensheni limechukua nafasi ya mbele magazetini baada ya Welteke wa chama cha Social Demokratik,kushtaki mahakamani kuwa pensheni yake ya Euro elfu nane kwa mwezi itamlazimisha kupunguza maisha yake ya anasa.Mkuu huyo wa zamani wa benki amefanikiwa kortini,hata ikiwa amepata sehemu tu ya kile kitita alichotaka.Je,hatua iliyochukuliwa na Welteke kwenda mahakamani itaanzisha mtindo mpya kwa wapokeaji pensheni wote na wale wanaopokea msaada wa serikali ili kuweza kuishi? Hilo ni suala linauliza na Stuttgarter Nachrichten.

Gazeti la NORDBAYRERISCHE KURIER likikejeli linasema:

“Sasa Ernst Welteke anaruhusiwa kuwa na maisha ya anasa kwa gharama ya taifa.”

Kwa upande mwingine gazeti la OFFENBURGER TAGEBLATT linasema Welteke ni mtu mwenye tamaa kubwa.Uamuzi uliopitishwa mahakamani huenda ukawa ni sawa kisheria,lakini umesababisha hasara kubwa ya kisiasa.Kwani raia watazidi kuamini kwamba wakubwa katika sekta za kisiasa na biashara wanaweza kuishindilia mifuko yao na raia wa kawaida ndio wanaopaswa kulipia gharama hizo.”

Sasa hebu tutupie jicho mada nyingine.Maoni ya raia yanatofautiana kuhusu kifo cha dikteta wa zamani wa Chile Augusto Pinochet.Wafuasi wake, wana msiba na wapinzani wake,wanafurahia kifo cha dikteta huyo wa zamani.Magazeti ya Ujerumani yakishughulikia mada hiyo,TAGESPOST linasema: “Sasa ndio amefariki,bila ya kuwajibika mbele ya mahakama-jambo linaloacha uchungu mkubwa kati ya wahanga wengi.Lakini kifo chake pia kinatoa nafasi ya kuwa na majadiliano ya kinagauabaga kuhusu wakati wa zamani.Kwa mfano,rais Michelle Bachelet wa Chile alieshika madaraka tangu mwezi Machi na ambae yeye binafsi ni muhanga wa udikteta wa Pinochet,anaweza kutoa mchango mkubwa katika utaratibu huo.”

Na gazeti la DRESDNER NEUESTE NACHRICHTEN linaamini:

“kuna sababu nyingi kwanini Pinochet hakuwahi kuadhibiwa.Linasema,sababu moja muhimu,inahusika na Chile yenyewe,kwani hata baada ya mapinduzi, udemokrasia uliendelea kuwa na mgawiko.Hofu kuhusu msimamo utakaochukuliwa na jeshi pamoja na uoga wa kutonesha upya vidonda vya zamani,ni mambo yaliozuia msimamo mmoja wa kitaifa kupatikana kuhusu hatua ya kuchukuliwa,dhidi ya mdhalimu huyo.Ikumbukwe kuwa utaratibu wa kukabiliana na udikteta wa Pinochet,humaanisha hata zile sababu za mapinduzi,zinapaswa kujadiliwa wazi wazi.” lamalizia Dresdner Neueste Nachrichten.