1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchambuzi wa Magazeti ya Ujerumani

3 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/CW1R

Mada iliyogonga vichwa vya habari katika magazeti ya Ujerumani leo hii ni uchaguzi wa bunge uliofanywa nchini Urusi siku ya Jumapili.Tangu mwanzoni shutuma za kufanywa udanganyifu katika uchaguzi wa bunge nchini Urusi ziliashiria kuwa mgombea mkuu Vladimir Putin atachomoza kama mshindi.Alipopiga kura yake,Putin alikuwa katika hali ya furaha.Lakini huku Ujerumani yadhihirika kuwa uhariri wa mtazamo mmoja unamchafulia Putin furaha yake.

Kwa mfano mhariri wa LANDESZEITUNG kutoka Lüneburg anasema:

Mshindi amepatikana na hata mshindwa pia. Kwani idadi kubwa ya kura zilizopigwa na Warusi kwa chama cha Rais Vladimir Putin cha „United Russia“ ni pigo kwa demokrasia katika nchi iliyo kubwa kabisa duniani.Putin ameufanya uchaguzi wa bunge kuwa kura ya maoni ya kupanga upya wadhifa wa rais atakaefuata.Mfumo wa mabavu unapewa sura ya kidemokrasia.Mara kwa mara Putin ametamka kuwa hatokwenda kinyume na katiba.Lakini chama chake kikidhibiti bungeni,Putin huenda akatumia wingi huo kufanya mageuzi ya katiba.

Na FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG linasema:

Viongozi wa Kremlin tangu hapo mwanzoni walihakikisha kuwa wapiga kura hawatokuwa na chaguo jingine isipokuwa kuwapatia viongozi hao matokeo waliotazamia.Rais Putin kama mgombea mkuu wa chama cha United Russia,aliufanya uchaguzi wa bunge kuwa kura ya maoni kuhusu umaarufu wake binafsi.Kwa ufupi ni kwamba Putin,anataka kutumia matokeo ya uchaguzi kujipa haki ya kimaadili kujipatia usemi mkubwa zaidi katika siasa za Urusi,baada ya kumalizika kwa awamu yake ya pili kama rais.

Kutoka Berlin gazeti la TAGESZEITUNG likichunguza kilichosababisha matokeo kama hayo linaeleza hivi:

Kuna sababu nyingi kwanini wapiga kura wengi na hasa vijana walitoa kura zao kwa Putin. Kiongozi huyo alifanikiwa kujitokeza kama mwanasiasa pekee anaeweza kudhamini utulivu nchini Urusi.Wakati huo huo,watu wazima waanaamini kuwa kupiga kura ni wajibu wa kiraia. Putin pia hutazamwa kama ni kiongozi aliefanikiwa kuimarisha tena msimamo wa Urusi katika jumuiya ya kimataifa.Vile vile uchumi uliofumuka, ukisaidiwa na kuongezeka kwa bei za gesi na mali ghafi umemuimarisha zaidi Putin.

Sasa hebu tutupie jicho gazeti SÜDDEUTSCHE ZEITUNG:

Mhariri wa gazeti hilo anasema;Putin ni bingwa kuweka siri,yeye hupenda kushtusha.Hapo kabla hakuna anaepaswa kujua iwapo Putin anataka kuwa rais wa bunge,waziri mkuu au,kwa kuibadili katiba atarejea tena kama rais wa taifa.Wananchi mara kwa mara wamekumbana na propaganda kuwa Putin ndio anaeweza kudhamini utulivu bila ya kuitumbukiza nchi katika hali ya machafuko. Kinachotisha ni kwamba Putin mwenyewe anaamini hivyo,lamalizia Süddeutsche Zeitung.