1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchumi: Dola ya Marekani yaendelea kudidimia

Mwakideu, Alex14 Machi 2008

Mfumuko wa bei katika nchi 15 wanachama wa Umoja wa Ulaya ulibadilishwa na kufikia asilimia 3.3 mwezi wa Februari

https://p.dw.com/p/DOey
Fedha za Marekani na UlayaPicha: AP

Mfumuko wa bei katika nchi 15 wanachama wa Umoja wa Ulaya ulibadilishwa na kufikia asilimia 3.3 mwezi wa Februari. Kufuatia mabadiliko hayo kiwango cha bei kwa mnunuzi kila mwaka kimesukumwa mbali na lengo la Banki kuu ya Ulaya la asilimia 2. Bei ya dhahabu nayo imefikia dola elfu moja kwa wakia jambo ambalo halijawahi kutokea. Hali hii inaathiri uchumi wa mataifa mbali mbali ulimwenguni yakiwemo ya Africa.


Ripoti kutoka kwa ofisi za makadirio za Umoja wa Ulaya zinaonyesha kwamba mfumuko wa bei katika eneo la ulaya ulifikia asilimia 3.2 mwezi jana. Hicho kikiwa ni kiwango cha juu zaidi tangu kuanzishwa kwa fedha za Euro january mwaka wa 1999.


Lakini kupanda kwa bei za vyakula na mafuta kumechangia zaidi hali hii haswa ikiangaziwa kwamba kiwango cha februari kilipanda kutoka asilimia 3.2 kiwango cha januari.


Mwaka uliopita mfumuko wa bei ulaya ulikuwa wa asilimia 1.8.


Ishara za kupanda kwa gharama za maisha ulimwenguni zimeziweka banki kuu mbali mbali ulimwenguni katika hali ya sinto fahamu.


Wiki hii dola ilishuka na kufikia kiwango cha chini na kubadilishana na euro kwa dola 1.5. Bei ya dhahabu nayo imepanda na kufikia dola elfu moja kwa wakia. Huku kukiwa na wasi wasi kwamba uchumi mzuri wa Marekani wenye mashikamano na ulimwengu huenda ukaanguka na kuuweka ulimwengu mzima katika hali mbaya kiuchumi.


Wakati huo huo kuanguka kwa dola kumesababisha kupanda kwa bei ya mafuta ambayo wiki hii yamepanda kwa kiasi kikubwa na kuuzwa kwa dola 111 kwa pipa.


Haya yote yamesababisha kupanda zaidi kwa gharama ya maisha.


Licha ya kupanda kwa gharama ya maisha kwa nchi 15 wanachama wa Umoja wa Ulaya mfumuko wa bei kwa nchi mpya zilizojiunga na Umoja huo kutoka ulaya ya kati na ulaya mashariki ulifikia asilimia 3.4 mwezi februari. Hali hiyo ikiwa ni sawa na hali ya januari.


Dola ya Marekani ilishuka na kubadilishwa kwa chini ya yen mia moja kwa siku ya pili mfululizo.


wakati huo huo imekuwa ikibadilishana na pauni kwa dola 2.


Wasi wasi kuhusu uchumi wa Marekani umewapelekea wawekezaji kuanza kununua dhahabu badala ya hisa za makampuni na dola za marekani.


Tangu mwanzoni mwa mwaka thamani ya dhahabu imepanda kwa asilimia 20 baada ya kupanda kwa asilimia 37 mwaka wa 2007.


Wadadisi wa maswala ya uchumi wanasema kwamba bei ya dhahabu itaendelea kupanda iwapo dola ya Marekani na kukua kwa uchumi wa nchi hiyo kutaendelea kuingia kudidimia.


Dhahabu hupimwa na kuuzwa kwa viwango vya wakia. Wakia mmoja unatoshana na gramu 31.1035.