1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchumi wa Ujerumani na Ufaransa waimarika

P.Martin16 Julai 2007

Uhusiano wa kiuchumi kati ya Ujerumani na Ufaransa ni wa karibu sana.Kwa uchumi wa Ujerumani,Ufaransa ni mshirika muhimu kabisa wa biashara.Hali kadhalika,katika uchumi wa Ufaransa makampuni ya Kijerumani huchukua nafasi ya kwanza kama wateja na wagavi.

https://p.dw.com/p/CHAv

Uchumi wa Ufaransa unanufaika sana kwa sababu ya hali nzuri ya kiuchumi nchini Ujerumani,kwani uwekezaji na uagiziaji wa bidhaa umeongezeka kwa nguvu.Mwaka uliopita mauzo ya nje ya Ufaransa nchini Ujerumani yaliongezeka kwa asilimia 18.Wakati huo huo biashara ya Ujerumani nchini Ufaransa iliongezeka kwa asilimia 9 ikiwa ni sawa na Euro bilioni 86.Na kuna kila ishara kuwa biashara kati ya madola makuu mawili ya uchumi barani Ulaya itazidi kukua.

Lakini hesabu zaonyesha kuwa biashara ya Ujerumani ina ziada ya takriban Euro bilioni 23.Hata katika biashara na nchi za kigeni, Ujerumani ina ziada kubwa,wakati ambapo Ufaransa huonyesha dhahiri kuwa kuna nakisi katika biashara yake na nchi za kigeni.

Kwa maoni ya Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy, kuongezeka kwa thamani ya Euro ni kitisho kwani bidhaa kutoka nchi zinazotumia Euro ni ghali katika masoko ya kimataifa.Kwa hivyo,anashauri kuwa thamani ya Euro ipunguzwe panapofanywa biashara na nchi zilizo nje ya eneo linalotumia Euro.Sarkozy anasema,serikali zinapaswa kuwa na usemi mkubwa zaidi katika maamuzi ya Benki Kuu ya Ulaya,jambo linalokataliwa kabisa na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel.

Kwa maoni ya Merkel kilicho muhimu kabisa ni kuulinda umma dhidi ya mfumuko wa bei.Vile vile anasema,ni muhimu sana kwa Benki Kuu ya Ulaya kuwa na uhuru na kutoingiliwa kisiasa.

Sekta muhimu kabisa za biashara kati ya Ujerumani na Ufaransa,ni uhandisi,uwekezaji,vifaa vya elektroniki,kemia na magari.Lakini sekta inayozidi kuwa na umuhimu tangu miaka michache iliyopita inahusika na usafiri wa ndege yaani makampuni ya Airbus na Eurocopter pamoja na makampuni mengine yanayotengeneza sehemu zinazohitajiwa na shirika kuu la misafara ya ndege ya Ulaya-EADS ambalo ni mzazi wa Airbus.

Mivutano kati ya Ujerumani na Ufaransa ndani ya kampuni hiyo ya Ulaya,imelaumiwa kuwa ndio imechangia kuchelewesha kuwasilishwa kwa wakati, ndege kubwa kabisa duniani-Airbus 380 kwa mashirika yaliyoagizia ndege hizo.

Lakini hivi punde,shirika hilo limetangaza mageuzi ya kurahisisha usimamizi kati ya mataifa mawili.Wakati huo huo,Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy wanakutana katika makao makuu ya Airbus mjini Toulouse,kusini magharibi ya Ufaransa.Mbali na suala la EADS,viongozi hao pia watajadiliana sera ya uchumi ya Ulaya pamoja na ukosoaji wa hivi karibuni wa Sarkozy kuhusu nguvu ya sarafu ya Euro.