1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

270710 Aufschwung Deutschland

Josephat Nyiro Charo5 Agosti 2010

Wanauchumi waonya dhidi ya kufurahia matokeo ya ukuaji wa kiuchumi yaliyotangauzwa mwezi Julai mwaka huu. Wanasema kasi ya kukua kwa uchumi huenda ikapungua katika miezi iliyobakia ya mwaka huu

https://p.dw.com/p/Obf0
Kansela wa Ujerumani, Angela MerkelPicha: AP

Uchumi wa Ujerumani umeonyesha dalili za kukua na kuimarika. Taarifa za kutia moyo kuhusu uchumi na matokoe ya shughuli za kiuchumi za kampuni mbalimbali humu nchini katika kipindi cha robo ya kwanza na ya pili mwaka huu zimezusha hali ya kufurahia katika sekta ya kiuchumi. Lakini, hata hivyo, kuna wataalam wa uchumi wanaoonya juu ya kuwa na furaha kubwa, kwani katika miezi sita iliyobakia mwaka huu kasi ya kukua kwa uchumi inaweza kupungua.

Uchumi wa Ujerumani wakati huu unaonekana unapumua, huku kukiwa na mtitiriko wa habari za kutia moyo na takwimu zikionyesha kuwa mambo ni shwari. Takwimu zilizotolewa mwezi uliopita wa Julai zimeonyesha ukuaji mkubwa wa uchumi wa Ujerumani tangu iliyokuwa Ujerumani Mashariki na Ujerumani Magharibi zilipoungana. Benki ya Ulaya ilitangaza ongezeko la mikopo katika nchi 16 wanachama wa Umoja wa Ulaya. Benki ya Ujerumani ya Deutsche Bank ilitangaza faida ya Euro bilioni 1,5. Kampuni ya programu za kompyuta ya SAP ilitangaza faida ya asilimia 15, ikiwa ni takriban Euro nusu bilioni. Na kampuni ya kutengeneza magari ya Daimler mjini Stuttgart nayo ikatangaza faida ya Euro bilioni 1,3.

Hali ya kushangilia na kutia moyo katika uchumi wa Ujerumani itategemea watumaiji bidhaa hapa nchini na inatarajiwa kuimarika msimu huu wa kiangazi. Licha ya mpango wa kubana matumizi wa serikali ya Ujerumani na ongezeko la kiwango cha fedha kinachotolewa kwa ajili ya bima ya afya, kiwango cha utumiaji bidhaa kinatarajiwa kuongezeka mwezi huu wa nane. Hayo ni kwa mujibu wa shirika la utafiti wa utumiaji biadhaa lenye makao yake mjini Nürnberg. Soko la ajira linatarajiwa kuimarika na shirika la ajira la Ujerumani limesema kuna uwezekano wa idadi ya watu wasio na ajira kupungua chini ya milioni tatu katika msimu wa mapukutiko.

Michael Grömling wa taasisi ya uchumi mjini Cologne hapa Ujerumani anasema, "Hali nchini Ujerumani kwa wakati huu ni nzuri zaidi kuliko ukweli halisi wa mambo katika uchumi. Uchumi kwa sasa bado ungali umekabwa koo na athari za msukosuko wa kiuchumi ulioikabili dunia, lakini hata hivyo kuna dalili za kuongezeka mahitaji ya bidhaa katika nchi za kigeni. Hali hiyo inaimarisha matumaini nchini Ujerumani hususan katika kampuni za sekta ya viwanda, na inatia moyo sana."

Hata hivyo, watalaam wa uchumi wameonya juu ya kufurahia mapema ukuaji wa uchumi wa Ujerumani. Taasisi ya utafiti wa kiuchumi mjini Halle imeonya kuwa uchumi wa Ujerumani huenda ukapanda kwa mwendo wa kinyonga kuelekea mwisho wa mwaka huu. Taasisi ya utafiti wa kiuchumi mjini Berlin pia imetoa ubashiri kama huo.

Hali hii inatokana na matatizo ya kiuchumi nchini Marekani na kuzorota kwa uchumi wa China ambako kunaweza kuathiri uuzaji wa bidhaa za Ujerumani katika nchi za kigeni. Pia mipango ya kufunga mikaja katika nchi za Umoja wa Ulaya.

Hata hivyo, Michel Heise, mchumi mkuu wa shirika la Allianz, anasema bado ana matumaini. "Mipango ya kubana matumizi iliyopitishwa na nchi za Ulaya si mibaya vile na haiendi mbali sana kuweza kuhatarisha kufufuka na kuimarika uchumi katika miezi ijayo na katika mwaka mzima huu wa 2010. Na hiyo kwa sehemu kubwa inatokana na kushuka kwa thamani ya sarafu ya Euro, hali ambayo katika kipindi kirefu inatarajiwa kuongeza uuzaji wa bidhaa nje ya nchi za Ulaya kwa asilimia nne. Na hilo ni jambo zuri sana kwa biashara."

Kwa upande wake, Hans Werner, mkuu wa taasisi ya uchumi mjini Munich amesema, na hapa namnukulu, "Tunaweza kupumua lakini hatuwezi kujikwamua kutokana na msukosuko wa kiuchumi," mwisho wa kumnukulu. Amesema pia kwamba kuzorota kwa uchumi katika nchi za nje ambako kunatarajiwa kupunguza uuzaji wa bidhaa za Ujerumani, na mpango wa kubana matumizi wa serikali ya Ujerumani ambao unatarajiwa kudhoofisha kampuni binafsi, ni mambo yanayomtia wasiwasi kuhusu uwekezaji wa kampuni. Uchumi hautarajiwi kukua tena kwa asilimia moja kwa sababu kampuni nyingi bado zinakabiliwa na hali ngumu kiuchumi. Na zile ambazo hazikabiliwi na changamoto haziwezi kununua mashine mpya.

Mwandishi: Wenkel, Rolf (DW Wirtschaft)/ZPR/Charo, Josephat

Mhariri: Miraji Othman