1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchumi wa Ujerumani waonyesha ni imara

16 Januari 2013

Makadirio ya kiuchumi,uchaguzi katika jimbo la Lower Saxony na bingwa wa zamani wa dunia wa mbio za baskeli,Tour de France,Lance Amstrong,kukiri ametumia madawa ya kuimarisha misuli

https://p.dw.com/p/17KlC
Kiwanda cha magari ya BMW huko Dingolfing,kusini mwa UjerumaniPicha: picture-alliance/dpa

Tuanzie lakini na makadirio ya ukuaji wa kiuchumi nchini Ujerumani. Gazeti la "Landeszeitung" linaandika:"Rais wa baraza la Umoja wa Ulaya, Hermann Van Rompuy, aliashiria muda mfupi kabla ya sikukuu za Krismasi "janga baya zaidi limeachwa nyuma ". Kama kauli hiyo itakuwa na maingiliano na maendeleo ya kiuchumi ya Ujerumani mnamo miezi ijayo, itategemea na hatima ya mambo mawili. Kama uchumi wa China hautapooza, basi nafasi itakuwa nzuri. Lakini hilo pekee halitoshi: Pale tu ambapo Wademokrats na Warepublican nchini Marekani watakapokubaliana mwishoni mwa mwezi ujao wa Februari, kupandisha kiwango cha juu cha madeni ya serikali cha dola bilioni 16.4, ndipo shughuli za makampuni ya magari ya Ujerumani zitakapoendelea kuwa nzuri nchini Marekani. Angalao kwa muda mfupi ujao.

Pengo kati ya Mashariki na Magharibi bado halijapungua

Gazeti la "Sächsische Zeitung" linalinganisha hali ya kiuchumi kati ya sehemu ya mashariki na ile ya magharibi ya Ujerumani. Gazeti linaendelea kuandika:Kuna kisichobadilika kwa vyovyote vile; naiwe shughuli za kiuchumi zinaimarika au zimetuwama. Mwanya kati ya shughuli za kiuchumi katika eneo la mashariki na magharibi ya Ujerumani haupunguwi. Miaka mitatu ya maendeleo ya kiuchumi haijasaidia kuharakisha utaratibu wa kuinua shughuli za kiuchumi katika sehemu ya mashariki na kwa mwaka huu mpya wadadaisi wanaashiria ukuaji mdogo tu wa kiuchumi ambao utakuwa wa aina moja, magharibi na mashariki pia.

Symbolbild Wahlurne
Kituo cha upigaji kura mjini HannoverPicha: picture-alliance/dpa

Mada nyengine iliyogonga vichwa vya habari vya magazeti ya Ujerumani hii leo inahusiana na uchaguzi ujao katika jimbo la Lower Saxony. Gazeti la "Rhein-Neckar Zeitung" linaandika:"Uchaguzi katika jimbo la Lower Saxony umevitumbukiza vyama vyote katika hali ya wasiwasi. Chama cha FDP kwa sababu kinatapia uhai wake wa kisiasa, SPD kwa sababu utakuwa mtihani wa mwanzo kupima umashuhuri wa mgombea wao wa kiti cha kansela. Na CDU kwa sababu, ingawa wataendelea kuwa chama chenye nguvu, lakini pengine wasiweze tena kutawala. Matokeo yake ni kwamba kila upande unatapatapa.

Michezo na madawa ya kuimarisha misuli

BdT: Lance Amstrong gewinnt zum siebten Mal die Tour de France 2005
Lance Amstrong ,aliposhinda kwa mara ya saba mashindano ya baiskeli ya Tour de France July mwaka 2005Picha: AP

Na hatimaye michezo na madawa ya kuimarisha misuli. Kisa hicho kimemkumba mshindi wa zamani wa mbio za baiskeli, Tour de France , Lance Amstrong. Jana alikuwa na mahojiano na mtangazaji mashuhuri wa televisheni nchini Marekani Oprah Winfrey. Gazeti la Berliner Morgenpost linaandika

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Marekani, Lance Amstrong amekiri kwamba amekuwa kwa miaka kadhaa akitumia madawa ya kuimarisha misuli. Mahojiano aliyoyafanya na mtangazaji mashuhuri kabisa, Oprah Winfrey, yatatangazwa kesho Alhamisi. Inasemekana mwanaspoti huyo aliyepokonywa mataji yote saba ya Tour de France tangu Oktoba mwaka jana, ameungama wakati wa mahojiano hayo, kwamba ameanza kutumia madawa ya kuimarisha misuli tangu miaka ya 90.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Josephat Charo