1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchunguzi wa mkutano kati ya Bush na Putin

Dreyer, Maja7 Aprili 2008

Mada kuu kwenye kurasa za wahariri hii leo ni mkutano wa mwisho kati ya marais wa Marekani na Urusi, George W. Bush na Vladimir Putin.

https://p.dw.com/p/DdN1
Marais Putin na Bush walikutana mara ya mwisho mjini SotshiPicha: picture-alliance/ dpa

Gazeti la “Handelsblatt” limechambua hivi matokeo ya mkutano huu:


“Mazungumzo yaliyofanyika huko Sotshi yalionyesha wazi mipaka ya mamlaka ya marais hawa wawili. Kinyume na maoni ya watu wengi, marais Bush na Putin hawana uhuru kufanya kama watakavyo. Rais Bush alilaumiwa huko nyumbani kwamba ameshindwa kutekeleza lengo lake la kulishawishi shirika la kujihami la Magharibi, NATO, likubali uanachama wa Ukraine na Georgia. Wala hajakubali kurudi nyuma kuhusu mpango wa kujenga mitambo ya kufyatua makombora huko Tchek na Poland. Putin pia aliathirika kutokana na mkutano wa NATO mjini Bukarest. Kwa hivyo hata yeye hakuweza kwenda mbali katika mgogoro juu ya mitambo ya kufyatua makombora ambayo Urusi inaupinga.”


Tuendelee na gazeti la “Bayerische Rundschau” ambalo linalinganisha marais hawa wawili wa Urusi na Marekani. Limeandika:


“Rais Putin ni mtu ambaye anawakilisha Urusi inayojiamini kama nchi yenye mali ghafi na ambayo itatumia utajiri huo kwa ajili ya kutekeleza sera zake za nje. Basi, usawa katika siasa za kimataifa hautegemei tena idadi ya mabomu ya kinyuklia au meli za kijeshi hapa na pale. Hususan baada ya vita vya Iraq ambapo Marekani imefahamu kwamba hata jeshi lake kubwa kabisa duniani linaweza kushindwa. Bush anaonekana kama hana nguvu na Putin amemwonyesha mwenzake wa Marekani kwamba hata wakati muda wake madakarani unapokaribia mwisho mwake, bado anaweza kunyosha misuli.”


Na zaidi juu ya uhusiano kati ya Urusi na Marekani aliandika mhariri wa “Süddeutsche Zeitung”:


“Marekani imeiacha kando Urusi katika miaka iliyopita. Hilo lilikuwa kosa. Na Urusi ilitia chumvi katika matamshi yake ya kimataifa. Hilo limeleta hatari. Basi, kwenye mkutano wao wa Sotshi, tuliona Marais Putin na Bush kuwa na wasiwasi juu ya uhusiano wao, na vilevile wamefahamu kwamba ni vigumu kubadilisha hali hiyo. Kwa vyovyote vile lakini hili ni jukumu la marais wapya wa Urusi na Marekani.”


Na hatimaye mhariri wa gazeti la “Thüringer Allgemeine” amechambua msimamo wa nchi za Ulaya juu ya marais Bush na Putin kuondoka madarakani. Ameandika hivi:


“Kimsingi, nchi za Ulaya hazisikitishwi sana na marais hawa wawili kushuka kwenye jukwaa. Wote wawili hawakupendwa sana. Mmoja kwa sababu pamoja na kuhakikisha uimara wa serikali pia ameleta tena ionekane misuli ya mamlaka. Na mwingine kutokana na kuleta uchuki badala ya maridhiano. Basi, matumaini ni makubwa kuelekea wale watakaowafuata.”