1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Udondozi wa magazeti ya Ujerumani

Josephart Charo19 Februari 2007

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo hii wamejihusisha na mwito wa kupiga marufuku uvutaji sigara ndani ya motokaa za kibinafsi. Mwito huo ulizusha mjadala mkubwa mwishoni mwa juma huku watu wakijiuliza ni kwa umbali gani serikali ya Ujerumani inatakiwa kuyaingilia maisha ya kibinafsi ya raia wake. Mada nyengine inahusu azimio la kupinga sera ya rais George W Bush wa Marekani kuelekea Irak.

https://p.dw.com/p/CHTg

Tunaanza na kupingwa kwa pendekezo la kamishna wa tume ya kupambana na madawa ya kulevya ya Ujerumani, Sabina Bätzing, la kutaka uvutaji sigara ndani ya motokaa za kibinafsi upigwe marufuku.

Gazeti la Landeszeitung kutoka mjini Lüneburg kwa maoni yake linasema serikali kuu na ya majimbo hazitaweza kuwa na sheria sawa kuhusu uvutaji wa sigara kwenye majengo na mikahawa kwani tayari tume ya kupambana na madawa ya kulevya ya Ujerumani inazungumzia marufuku ya uvutaji sigara ndani ya motokaa za kibinafsi.

Mhariri anasema bila shaka ni hatua ya kutojali kuvuta sigara ndani ya motokaa hususan watoto wakiwemo. Lakini wakati huo huo kuanzisha sheria ya kupiga marufuku uvutaji wa sigara ndani ya gari la mtu binafsi inaonekana ni hatua inayovuka mpaka.

Mhariri wa gazeti la General Anzeiger la hapa mjini Bonn amelichunguza kwa makini swala hili. Anasema polisi hivi karibuni hawatatakiwa tu kuchunguza ikiwa madereva wanaendesha magari wakiwa walevi, bali pia kuwauliza swali, je umevuta sigara? Mshukiwa wa uvutaji sigara atapimwa na jina lake kuwekwa katika orodha ya data ya wahalifu wa uvutaji wa sigara ambayo bado haijakamilika huko mjini Flensburg.

Maneno ya wazi yamesemwa pia na mhariri wa gazeti la Wiesbadener Kurier. Ni jambo la kibinafsi kuvuta sigara ndani ya gari lako au nyumbani kwako. Yeyote ambaye hana uelewa wa kutosha kumuwezesha kuwacha mwenyewe kwa hiari kuvuta sigara wakati watoto wakiwepo, hataweza kuzuiliwa hata akitozwa faini.

Mbali na kuitisha marufuku ya uvutaji sigara ndani ya gari za kibinafsi, idara ya kupambana na madawa ya kulevya ya Ujerumani ingekuwa inafanya ushauri mzuri kwa kuanzisha kampeni za hadhara za kuwahamasisha watu.

Mada ya pili iliyozungumziwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo hii ni kupingwa kwa azimio linaloupinga mpango mpya wa rais George W Bush wa Marekani kuhusu Irak. Gazeti la Dresdner Neueste Nachrichten limesema baraza la wawakilishi limemuonyesha rais Bush kadi ya manjano.

Bunge la Congress lenye idadi kubwa ya wabunge wa chama cha Democratic imelipinga pendekezo la rais Bush kutaka kutuma wanajeshi 21,500 kwenda katika uwanja wa vita nchini Irak. Hatua hiyo inaoana na maoni ya Wamarekani na kukifanya chama cha Democratic kuwa katika nafasi nzuri ya kushinda uchaguzi ujao nchini Marekani. Hata katika chama cha Republican cha rais Bush hasira kuhusu mpango wa Bush, imeendelea kuongezeka.

Mhariri wa gazeti la Abendzeitung la mjini Munich amesema wabunge saba wa chama cha Republican wamepiga kura kumpinga rais wao. Idadi hiyo inajumulisha wabunge watano zaidi ikilinganishwa na wiki mbili zilizopita ambapo wabunge wawili pekee waliupinga mpango huo wa rais Bush.

Baada ya azimio hilo, chama cha Democratic kinabakia chombo muhimu kitakachouzuia mpango wa rais Bush. Bush anatakiwa kuliomba bunge la Congress liidhinishe dola milioni 141.7 kwa ajili ya wanajeshi zaidi watakaokwenda Irak. Mhariri ameuliza, ´Je itakuwaje ikiwa wabunge watakataa kuidhinisha pesa hizo zitolewe?´