1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Udondozi wa magazeti ya Ujerumani

Josephat Charo5 Oktoba 2006

Kuahirishwa tena kukamilika kwa dege kubwa la abiria ya aina ya A380 kumeitumbukiza kampuni ya Airbus katika tatizo kubwa na kuzusha hofu ya kupotea nafasi za ajira. Serikali kuu ya Ujerumani na serikali za mikoa zinataka nafasi za kazi zilindwe. Wahariri wa magezeti ya Ujerumani leo wamezingatia makosa ya kampuni ya Airbus.

https://p.dw.com/p/CHUl

Likituanzia udondozi wa leo gazeti la Badische Tagblatt kutoka Baden- Baden limeandika: Shina la tatizo la kampuni ya Airbus ni uhusiano kati ya masilahi ya kiuchumi na ya kisiasa.

Uwezo wa kuendelea kuwakilisha na kuzingatia serikali mbalimbali kuna jukumu kubwa katika kazi ya kutengeza sehemu tofauti za ndege. Kisiasa hiyo ni halali, lakini kiuchumi ni makosa kwani ni kwa kutumia vifaa vizuri vyenye bei za kuvutia kutakakosaidia ndege kudumu kwa muda mrefu katika soko la kimataifa.

Mhariri wa gazeti la Nordsee la Bremerhaven, anasema tatizo la kampuni ya Airbus safari hii halikusababishwa na hali ngumu katika soko la ndege, kama ilivyokuwa miaka ya 90 katika mpango wa kukarabati na kuuza ndege.

Wakati huu ni kinyume cha yale yaliyotokea wakati huo – kukabiliana na idadi kubwa ya maombi ya mashirika ya ndege yanayotaka kununua dege la abiria la Airbus, hali iliyosababishwa na kosa la viongozi wa kampuni ya Airbus.

Kampuni hiyo ilitaka kutengeza ndege 430, idadi kubwa kabisa katika historia ya kampuni hiyo. Wanaomiliki hisa katika kampuni ya Airbus walifurahi tangu mwaka jana kwamba wangeweza kupata faida kubwa. Tatizo hili lililosababishwa na utawala wa Airbus haliwezi na halitakiwi kukabiliwa.

Mhariri wa gazeti la General Anzeiger anasema tatizo la kampuni ya Airbus ni tatizo la ndani na linajumuisha uongozi, wanaomiliki hisa na wafanyakazi viwandani. Mipango ya kupunguza matumizi inayotarajiwa kutekelezwa, inatakiwa kupunguza hasara ya mabilioni ya fedha.

Mengi yanaendelea katika kampuni ya Airbus lakini baya zaidi ni kuahirishwa kwa mara ya tatu kukamilishwa kwa dege aina ya A380. Hatua hiyo haijawakasirisha tu wateja bali pia imeiharibia sifa kampuni ya Airbus.

Gazeti la Ostsee la mjini Rostock linasema wenye dhamana katika mzozo wa Airbus sio akina Otto wa mjini Hamburg wala akina Pierres wa mjini Toulouse wanaotengeza ndege hiyo, bali ni kosa la meneja.

Mpango wa kupunguza matumizi ambao kiongozi mpya wa Airbus Christian Streiff anataka kuutumia kuikwamua kampuni hiyo, ungeweza kuzuia hasara kama ungepangwa vizuri na kuanza kutumika mapema. Mradi wa dege la A380 unamuweka Streiff katika hali ngumu na unaihatarisha kampuni.

Mhariri wa gazeti la Frankfurter Allgemeine amesema safari ya ndege inayoruka juu sana angani imegeuka kuwa safari ya kuteremka chini kwa kasi kubwa, ambayo sasa inahatarisha kampuni ya EADS, iliyoianzisha kampuni ya Airbus. Uongozi wa kampuni ya Airbus na EADS tayari ulibadilishwa, lakini mara kadhaa imebidi kukamilika kwa dege la A380 kuahirishwe.

Hatua hii itagharimu zaidi ya euro bilioni tano na ndiyo maana matumizi lazima yabanwe. Kwa kampuni ya Ulaya ni vigumu mno kwa kampuni ya kisiasa inayotaka kuwa kinyume na maana yake ya kijeshi kuweza kulifanikisha jambo hilo .