1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Udugu kati ya Hamburg na Dar es Salaam

Iddi Ssessanga7 Oktoba 2014

Kwa zaidi ya miaka minne sasa miji miwili ya bandari - Hamburg na Dar es Salaam imeunganishwa katika ushirikiano rasmi wa miji dada, unaoongozwa na asasi na raia, wakijenga uelewa bora, na kuja na mawazo mapya.

https://p.dw.com/p/1DRdg
Tansania Budget
Dar es Salaam.Picha: DW/Kizito Makoye Shigela

Ushirikiano wa miji ni aina ya makubaliano ya kisheria na kijamii kati ya miji, majimbo, mikoa, wilaya, kanda au hata mataifa katika maeneo yaliyobainishwa kisiasa na kijiografia yenye lengo la kuendeleza uhusiano wa kibiashara na kitamaduni.

Dhana ya sasa ya ushirkiano wa miji, iliyoanzishwa baada ya vita vikuu vya pili vya dunia mwaka 1947, ililenga kujenga urafiki na maelewano kati ya tamaduni mbalimbali na kati ya maadui wa zamani kama hatua ya amani na maridhiano, na pia kuhamaisha biashara na utalii.

Katika zama hizi, ushirikiano wa miji unatumika zaidi kujenga mahusiano ya kimkakati ya biashara ya kimataifa baina ya miji washirika. Mratibu wa ushirikiano kati ya Hamburg na Dar es Salaam, Inken Bruns anaelezea historia ya dhana hii ya ushirkiano wa miji.

"Tulikuwa na vita vikuu viwili vya dunia na baada ya vita wanasiasa walijaribu kufanya maridhiano na mataifa jirani lakini raia waliendelea kuhasimiana. Hivyo tulianzisha ushirikiano wa miji ili tujifunze kutoka kwa kila mmoja wetu, kwamba sote ni wamoja, na kwamba tunaweza kuisha pamoja na kufanya mambo pamoja, na kwamba tukifanya kazi pamoja ni kwa manufaa yetu sote," anasema Bruns.

Alsterarkaden Hamburg Archiv 2004
Hamburg.Picha: picture-alliance/dpa/Patrick Lux

Ushirikiano kati ya Hamburg na Dar es Salaam ulianza mwaka 2010 kwa mkataba uliyosainiwa Julai mosi, na kuufanya mji wa Dar es Salaam kuwa wa karibuni zaidi na wa pekee barani Afrika kuwa na ushirikiano na Hamburg. Bruns anasema sababu za kihitoria zinafafanua ushirkiano huu, kauli inayothibitishwa na Naibu Meya wa wilaya ya Kinondoni Songoro Mnyonge.

Ukianzia kwenye ngazi ya asasi za kiraia, hasa kati ya makanisa, ushirkiano huo umepanuka katika kipindi cha miaka minne na kuhusisha maeneo mengine kama vile idara za zimamoto, sekta za afya, elimu, na hivi sasa shule.

Ipo miradi kadhaa inayofanyika katika miji yote miwili chini ya ushirikiano ikihusisha utunzaji mazingira mfano katika wilaya ya Kinondoni, maboresho ya huduma za afya katika hospitali ya Amana wilayani Ilala na ushirkiano katika sekta ya elimu. Inken Bruns anasema yapo zaidi ya makundi 30 mjini Hamburg yanayofanyakazi na mengi zaidi ya mjini Dar es Salaam.

Hamburg na Dar es Salaam hushirikiana pia katika sekta ya Afya.
Hamburg na Dar es Salaam hushirikiana pia katika sekta ya Afya.Picha: picture-alliance/dpa/Georg Wendt

Panapokuwa na ushirkiano baina ya watu au pande mbili, ushirikiano huo mara nyingi hujengwa kwa misingi ya kimaslahi ambapo kila upande unategemea kunufaika kutoka kwa mwengine. Lakini Bruns anasema kilichomuhimu katika ushirikiano baina ya Hamburg na Dar es Salaam ni kuyapa maana maisha.

"Nimeskia watu wengi wakihamasishwa na mitizamo tofauti ya Tanzania kwa ulimwengu, na kuna masuala tofauti kwa mfano namna tunavyowashughulikia wazee hapa, au nini yanafanya mashirika ya kina mama nchini Tanzania. Nadhani kuna mengi tunajifunza kutoka kwenu, anafafanua.

Naibu meya wa Kinondoni Songora Mnyonge, anasema yapo mambo mengi sana ya wao kujifunza kutoka kwa mji wa Hamburg likiwemo suala la usafi na megineyo na hivyo changamoto waliorejea nayo nyumbani baada ya maadhimisho ya wiki ya ushirkiano kati ya mji hiyo ni kubadilisha fikra za wakaazi wa jiji hilo ili waweze kubaliana na maadui wakuu wa ujinga, maradhi na umaskini, mabo amabayo anasema Wajerumani wamepigwa hatua kubwa.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga
Mhariri: Josephat Nyiro Charo