1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Udugu wa Kiislamu kuwasaidia wapinzani Syria

Admin.WagnerD17 Julai 2012

Rais wa Urusi, Vladimir Putin, amemwambia mpatanishi wa amani wa mzozo wa Syria, Kofi Annan, kuwa atafanya awezalo kuunga mkono mpango wa Umoja wa nchi za Kiarabu wa kumaliza ghasia Syria.

https://p.dw.com/p/15ZBb
Mpatanishi wa mgogoro wa Syria, Kofi Annan
Mpatanishi wa mgogoro wa Syria, Kofi AnnanPicha: Reuters

Na Chama cha Udugu wa Kiislamu kimewaahidi msaada raia wa Syria huku kikiwataka kuamka na kuwaunga mkono waasi waliokwama katika mapambano dhidi ya vikosi vya jeshi la Rais Bashar al- Assad mjini Damascus.

Mwanzoni mwa mkutano wa Kremlin, Putin ameyasema hayo na Kofi Annan amemwambia Putin kuwa mzozo wa Syria umefikia mahali pabaya. Ziara hii ya Annan tangu mwezi Mei inakuja siku moja kabla ya mataifa ya magharibi kupanga kulipiga kura ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, linalotishia kuiwekea vikwazo serikali ya Syria.

Raia wakiandamana Tremseh, Syria kupinga mashambulizi yanayoelekezwa dhidi ya raia.
Raia wakiandamana Tremseh, Syria kupinga mashambulizi yanayoelekezwa dhidi ya raia.Picha: Reuters

Chama cha Udugu wa Kiislamu chapania kuwasaidia wapinzani Syria

Kwa upande wake, Chama cha Udugu wa Kiislamu chenye ushawishi mkubwa nchini Syria kimesema raia wa Syria wanalazimika kutumia wakati huu wa kihistoria kuwasaidia waasi wanaopigana vita na askari wa jeshi la Syria mjini Damascus kwa siku ya tatu mfululizoKatika taarifa yake, chama hicho kimewataka raia kujiandaa kuwa askari katika uwanja wa mapambano, kwani watapata ushindi kwa mikono yao wenyewe.

Aidha, chama hicho kimewaomba wananchi kufanya maandamano ya amani mchana na usiku kuipinga serikali sanjari na kuwaunga mkono waasi hao wenye silaha.

Taarifa hii inakuja kufuatia tangazo la Jeshi Huru la Syria, iliotolewa hapo jana kuwa limefanya operesheni kabambe iliyoipa jina "Volcano na tetemeko la ardhi la Damascus nchini Syria".

Umoja huo wa askari waliojitenga na jeshi la serikali ya Syria unajiandaa kumaliza mkutano mkuu wa siku mbili mjini Istanbul, Uturuki uliolenga kuusaidia upinzani Syria.

Rais wa Urusi, Vladmir Putin anasema yuko tayari kuunga mkono juhudi za kumaliza vita Syria.
Rais wa Urusi, Vladmir Putin anasema yuko tayari kuunga mkono juhudi za kumaliza vita Syria.Picha: AP

Damu yazidi kumwagwa katika viunga vya Syria

Mapigano yanaripotiwa kuendelea sehemu mbalimbali za Syria, kama anavyoeleza hapa msafiri mmoja aliyekuwa akielekea Uturuki hii leo"Tumetoka katika kijiji cha Atma. Nimewaleta watoto wawili hapa waliojeruhiwa. Mmoja wao amekwishapoteza maisha. Walijeruhiwa katika mripuko uliotokea kijijini hapo"

Kufuatia kadhia hiyo, msemaji wa serikali ya Iraq, Ali Dabbagh, amewaomba raia wa nchi hiyo kurejea makwao kufuatia mashambulizi yanayoelekezwa kwao.

Na Uturuki imesema brigedia mkuu na maofisa wengine wa jeshi ni miongoni mwa Wasyria 1,280 walioingia Uturuki wakikimbia vita nchini Syria.

Mwandishi: Pendo Paul

Mhariri: Miraji Othman