1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Udugu wa Kiislamu watangaza ushindi Misri

18 Juni 2012

Mamia ya wafuasi wa Udugu wa Kiislamu wamekusanyika katika uwanja wa al-Tahrir mjini Cairo kusheherekea baada ya chama hicho kutangaza ushindi katika uchaguzi wa rais.

https://p.dw.com/p/15H2m
epa03267819 Egyptian presidential candidate Mohammed Morsi (C) gestures after casting his vote for the run-off presidential elections at a polling station in Sharqiya, 140 km north east Cairo, Egypt, 16 June 2012. Some 50 million people are eligible to vote in the two-day poll to pick a successor to former president Hosni Mubarak, who was deposed in a popular revolt last year. The two contenders; Muslim Brotherhood candidate, Mohammed Morsi, and Mubarak's last PM, Ahmed Shafik, failed to secure an outright majority in the first round last month. EPA/STR
Präsidentenwahl in Ägypten Mohammed MursiPicha: picture-alliance/dpa

Chama cha Udugu wa Kiislamu kimeripoti kwenye tovuti yake kwamba mgombea wake Mohamed Mursi amejipatia asilimia 52 katika uchaguzi huo uliofanyika kwa siku mbili mwishoni mwa juma baada ya asilimia 95 ya kura kuhesabiwa kutoka vituo vya kupiga kura.

Mursi, profesa wa uhandisi, alisimama dhidi ya Ahmed Shafiq, kamanda wa zamani wa kikosi cha anga, ambaye alitumika kwa muda mfupi kama waziri mkuu wakati wa utawala wa Mubarak.

Katika hotuba aliyoitowa kwa njia ya televisheni mapema leo hii, Mursi amesisitiza ahadi yake ya kujenga taifa la Misri la kisasa chini ya misingi ya kiraia, na amesema kwamba hatotaka kulipiza kisasi au kujaribu kuwaandama wapinzani wake. Ameuambia mkutano wa waandishi wa habari ulioonyeshwa kwenye televisheni kwamba atakuwa rais kwa Wamisri wote - Waislamu na Wakristo.

Mgombea urais waziri mkuu wa zamani Ahmed Shafiq
Mgombea urais waziri mkuu wa zamani Ahmed ShafiqPicha: picture-alliance/dpa

Mursi, ambaye anaongoza chama cha Udugu wa Kiislam cha Uhuru na Haki, ametowa wito kwa Wamisri kuungana kuwa kitu kimoja ili kujenga mustakbali mzuri utakaokuwa na uhuru, demokrasia, maendeleo na amani. Amesema ujumbe wake ni wa amani kwa kila mtu duniani.

Ahmed Sarhan, msemaji anayesimamia kampeni ya Shafiq, amesema ni asilimia 40 tu ya kura zimehesabiwa na ameituhumu kambi ya Mursi kwa kutumia vibaya vyombo vya habari kwa manufaa yake.

Amesema tangazo hilo la upande mmoja ni jaribio la kuwadangaya wananchi.Kwa mujibu wa tume ya uchaguzi matokeo rasmi ya uchaguzi huo yanatarajiwa kutangazwa Alhamisi.

Shafiq anaonekana kama mabaki ya utawala wa Mubarak wakati wale wanaomkosoa Mursi wanasema Udugu wa Kiislamu wenye ushawishi mkubwa nchini Misri unataka kuanzisha taifa la kidini.

Baraza la kijeshi nchini humo jana usiku lilitowa waraka wa katiba wenye kuwapa madaraka ya shughuli za bunge hadi hapo bunge jipya litakapochaguliwa.

Majenerali hao watakuwa wabunge,watadhibiti bajeti na wataamuwa nani wa kuandika katiba ya kudumu ambayo itatowa ufafanuzi wa mustakbali wa nchi hiyo.

Mwandishi: Mohamed Dahman/dpa

Mhariri: Miraji Othman