1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UEFA EURO 2012: Uhispania Bingwa

2 Julai 2012

Uhispania imeandika historia miongoni mwa vigogo vya soka barani Ulaya kwa kuikandika Italia mabao 4-0 na kufanikiwa kutetea taji lake la ubingwa wa mataifa ya Ulaya, UEFA EURO 2012, Jumapili (01.07.2012).

https://p.dw.com/p/15P3i
Spain's team players celebrate with the trophy after defeating Italy to win the Euro 2012 final soccer match at the Olympic stadium in Kiev, July 1, 2012. REUTERS/Kai Pfaffenbach (UKRAINE - Tags: SPORT SOCCER)
Mabingwa wa UEFA EURO 2012Picha: Reuters

Mafanikio  ya Uhispania  yameandika upya  kitabu  cha  mbinu  za  ufundi wa  kusakata  kandanda   pamoja  na  vitabu  vya  historia   ya  soka baada  ya   magoli  ya  David Silva, Jordi Alba  na  wachezaji  wa akiba  Fernando  Torres  na  Juan Mata  kuwapatia  mabingwa  hao wa  dunia  ushindi  rahisi   dhidi  ya  kikosi  cha  timu  ya  Italia  huku kikiwa  na  wachezaji  10  tu  uwanjani  kutokana  na  kuumia  kwa mchezaji  wao Thiago Mata kwa  muda  wa  dakika  30  za  mwisho.

Italy goalkeeper Gianluigi Buffon reacts after Spain's Fernando Torres scored his sides 3rd goal during the Euro 2012 soccer championship final between Spain and Italy in Kiev, Ukraine, Sunday, July 1, 2012. (Foto:Michael Sohn/AP/dapd)
Mlinda mlango Gianluigi Buffon hana la kufanya baada ya mpira kutinga wavuniPicha: AP

Prandelli  na  Del Bosque wasifu vikosi vyao

Ulikuwa  mchezo  mzuri  kwa  wachezaji  wetu, wameudhibiti  mchezo , kocha  wa  Uhispania  Vicente Del Bosque amewaambia  waandishi habari. Tunao  washambuliaji  lakini  tumeamua  kucheza  kwa kuwatumia  wachezaji  ambao  ni  wazuri  kwa  mtindo  wetu  wa uchezaji.

Kocha  wa  Italia  Cesare  Prandelli  ameongeza  kuwa , Wameandika   historia   na  wamestahili , kwa  kuwa  wana wachezaji  wengi  ambao  wana  uzoefu  mkubwa  katika  kiwango hiki na  hata  kama  hawachezi  kwa  kumtumia  mshambuliaji  wa kawaida  wanasababisha  matatizo  makubwa  kwa  timu  pinzani.

Italy's Thiago Motta grimaces in pain during the Euro 2012 soccer championship final between Spain and Italy in Kiev, Ukraine, Sunday, July 1, 2012. (Foto:Jon Super/AP/dapd)
Thiago Mota wa Italia akishikilia mguu wake kwa maumivuPicha: AP

Wakati  mchezo  safi  wa  Uhispania  umewaletea  mafanikio makubwa  yaliyostahili, kile  walichofikia  kinahitajika  kuwekwa katika  mtazamo  wa  kihistoria,  hata  kama  mtindo  wao  wa uchezaji  wa  tiki taka  wa  pasi  fupi  fupi  umekosolewa katika mashindano  haya.

Uhispania  imekuwa  timu  ya  kwanza  ya  taifa  kushinda  mataji matatu  makubwa  katika  enzi  ya  leo  baada  ya  ushindi  wao katika  kinyang'anyiro  cha  Euro  mwaka  2008  na  ushindi  wao katika  kombe  la  dunia miaka  miwili  baadaye  na  wamejiunga  na timu  ya  Ujerumani  katika  rekodi  hiyo  ya  ushindi  mara  tatu  wa kombe  la  Euro.

Mwandishi : Sekione Kitojo / 2012