1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa ina mtihani mkubwa dhidi ya Ukraine

18 Novemba 2013

Mechi za mchujo za kufuzu katika Kombe la Dunia nchini Brazil zinarudi tena, ambapo Ufaransa inakabiliwa na jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa haikosi nafasi ya kushiriki katika michuano hiyo tangu miaka 20 iliyopita.

https://p.dw.com/p/1AKFZ
Wachezaji wa Ufaransa wanafahamu kibarua kinachowasubiri
Wachezaji wa Ufaransa wanafahamu kibarua kinachowasubiriPicha: afp

Hakuna timu yoyote ya Ulaya ambayo imewahi kufuzu kwa Kombe la Dunia kupitia mechi za mchujo, baada ya kushindwa mkondo wa kwanza magoli mawili kwa sifuri. Ufaransa iliduwazwa na Ukraine kwa kufungwa mabao mawili bila jawabu Ijumaa iliyopita, hiyo ikiwa na maana kuwa vijana hao wa kocha Didier Deschamps watahitaji kuonyesha mchezo wa kiwango cha juu katika mchuano wa marudiano hapo kesho.

Baada ya kushinda raundi ya kwanza ya vita kati yake na Zlatan Ibrahimovic wakati alipopachika wavuni bao la kichwa na lililoipa Ureno ushindi wa goli moja kwa sifuri dhidi ya Sweden, Christiano Ronaldo ana matumaini kuwa anaweza tena kuwa shujaa katika uwanja wa kitaifa wa Sweden hapo kesho. Zlatan alishindwa kutamba mjini Lisbon na anataraji kuwa mambo yatakuwa tofauti katika mkondo wa pili. Ugiriki wako katika nafasi nzuri baada ya ushindi wao wa mabao matatu kwa moja dhidi ya Romania katika mkondo wa kwanza, wakati nao Iceland wakiyaweka hai matumaini yao ya kushiriki kwa mara ya kwanza kabisa katika Kombe la Dunia baada ya kulazimisha sare ya kutofungana goli dhidi ya Croatia.

Khedira auguza jeraha la goti

Huenda ukawa ni mchuano tu wa kirafiki wa kujipima nguvu na pia kuwapa wakufunzi wa timu zote mbili fursa ya kuvitathmini vikosi vyao na kujua uwezo wa wachezaji, lakini pia, mechi ambayo inawaleta pamoja watani wa jadi.

Kiungo wa timu ya Ujerumani Sami Khedira anauguza jeraha la goti
Kiungo wa timu ya Ujerumani Sami Khedira anauguza jeraha la gotiPicha: DFB

Matarajio ya Uingereza, ya kufanya vyema katika dimba la kombe la dunia yatamulikwa tena hapo keshi wakati watakaposhuka dimbani na watani wao wa jadi Ujerumani katika uwanja wa nyumbani Wembley. Vijana hao wa Kocha Roy Hodgson waliduwazwa na Chile Ijumaa iliyopita kwa kurambishwa magoli mawili kwa sifuri, kikiwa ni kichapo chao cha kwanza katika mechi 10 za mwisho.

Matayarisho ya kocha wa Ujerumani Joachim Löw siyo tu kwa mchuano huo bali kwa tamasha la kombe la dunia wiki iliyopita yalipata pigo kutokana na habari za jeraha la Sami Khedira. Kiungo huyo wa Real Madrid alifanyiwa upasuaji wa jeraha la goti na huenda akawa mkekani kwa miezi sita. Kocha Löw alielezea matumaini kuwa nyita huyo huenda akapona katika muda unaofaa kabla ya tamasha la Brazil. "Tumehuzunishwa kwa sababu katika miaka yangu ya nyuma, tangu mwaka wa 2004, nikiwa hapa sikumbuki kama pamewahi kutokea jeraha baya kama hili. Na kwa Sami ambaye kwetu ni mchezaji muhimu, jeraha lake ni pigo kwetu"

Ujerumani ilitoka sare ya goli moja kwa moja na watani wao Italia Ijumaa. Kando na Khedira, wachezaji wawili wa Bayern Munich Nanuel Neuer na Philipp Lahm, nahodha, pia wamewachwa nje ya kikosi kitakachopambana na England. Pia Löw amempumzisha mchezaji wa Arsenal Mesut Özil. Mlinda lango wa Borussia Dortmund Roman Weidenfeller atavaa glovu za Neuer. Löw anasema "Franz Beckenbauer aliwahi kusema “tunauita mchuano wa mafahali wawili. Kucheza wuanjani Wembley ni kitu kizuri sana mbele ya mashabiki 80,000 au 85,000. hiyo pekee ni motisha ya kutosha na Uingereza bado ni mojawapo ya timu kubwa".

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters

Mhariri:Yusuf Saumu